Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika hoja hii ya afya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na maendeleo ya jinsia. Kwa kuwa Benki ya Wanawake iko katika maeneo machache, naiomba Wizara kuhakikisha kuwa Benki ya Wanawake inakwenda katika mikoa yote na kwa namna ya pekee naomba benki hii ianzishwe katika Mkoa wa Njombe kwenye Wilaya hata tatu za Makete, Njombe na Ludewa kwa kuwa benki hii itawanufaisha wanawake wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia, kumekuwa na matendo yaliyokithiri ya unyanyasaji wa wanawake kwa kupigwa na waume zao katika familia nyingi. Naiomba Serikali isimamie sheria hiyo. Pia kumekuwa na ukatili dhidi ya watoto na hasa watoto wa kike ambapo wamekuwa wakibakwa na hasa katika Mkoa wa Njombe. Naomba Wizara ishughulikie suala hili na kuhakikisha ukatili huo unatokomezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma za ustawi wa jamii, kwa kuwa kumeendelea kuwa na wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Serikali isaidiane na wadau mbalimbali wanaojitolea kuwahudumia watoto hao kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kutoa huduma bila kuwakatisha tamaa kwa kuwatoza kodi wakati wanatoa huduma kwa watoto hao. Kwa mfano vituo vya watoto yatima visitozwe kodi yoyote. Pia wanapokuwa na vyombo vya usafiri wasitozwe mapato, pia vituo hivyo vimekuwa vikiomba leseni pamoja na kuwa vigezo vyote lakini wamekuwa hawapewi leseni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba Serikali ikague vituo vyote nchini ambavyo vinakidhi vigezo wapewe leseni. Pia vituo vinavyofanya kazi vizuri basi wapewe motisha kwa kupata ruzuku. Hivyo naomba bajeti ya Wizara iongezwe ili kitengo hiki cha ustawi wa jamii kifanye kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya ya mama na mtoto; vifo vya akina mama wanaojifungua 556 kwa kila vizazi 100,000 ni idadi kubwa sana. Naiomba Wizara kufuatilia kwa ukaribu tatizo hilo na kuendelea kubaini vyanzo vya vifo hivyo na kutatua changamoto zinazogundulika kuwa ndivyo visababishi. Mfano katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Hospitali ya Kibena ambayo ni Hospitali ya Mkoa ya muda watoto wanaozaliwa njiti ni wengi lakini kutokana na kutokuwa na vifaa vya kuwatunzia watoto hao, wanapoteza maisha. Pia hawana x-ray. Naiomba Serikali itusaidie Wananjombe kuboresha Hospitali ya Kibena ili kuwaokoa wanawake wanaojifungua watoto na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la UKIMWI; watu wanaoishi na VVU wana changamoto kubwa za kupata septrin ambazo zingewasaidia sana kutopata magonjwa nyemelezi na watu hawana fedha za kununua dawa hizo. Naiomba Serikali kuwakatia bima za afya ili kunusuru maisha yao. Maana wakiwa na bima ya afya wanaweza kutibiwa bila matatizo na hivyo itasaidia kurefusha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba Serikali kufuatilia suala la mila potofu zinazosababisha UKIMWI uendelee kwa kasi katika Mkoa wa Njombe. Tatizo ni kurithi wajane na mikutano ya mapangoni ambako wanajamiiana bila kujali kama ni ngono salama au laa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iboreshe maslahi ya wafanyakazi kama call allowance na posho nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.