Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi jioni ya leo kupata nafasi hii kuchangia. Naomba kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja iliyoletwa mbele yetu na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana. Naomba niungane na Wabunge wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake. Baada ya kupongeza naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Serikali inayoongozwa na CCM kwa nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunaanza kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kalambo, naomba kasi hii ambayo imeoneshwa tusije tukasita hata kidogo, tuhakikishe kwamba tunaenda kuimalizia kabisa na itumike ili kuwasaidia Watanzania walio Mkoa wa Rukwa na hususani Wilaya ya Kalambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia wenzangu wakiwa wanamshukuru Mheshimiwa Waziri, wamepata ambulance ni jambo jema, naamini zamu nyingine na sisi Kalambo tutakumbukwa, ili kuunga jitihada za Mbunge huyu ambaye anaongea, maana ameweza kusababisha zikapatikana ambulance tatu. Ni wakati muafaka Serikali ikaniunga mkono ili tuokoe wananchi walioko Wilaya ya Kalambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matatizo ambayo tunayo makubwa wenzangu wamesema kuhusiana na suala zima la ukosefu wa watumishi pamoja na vifaa tiba na vitendanishi. Kama kuna maeneo ambayo yana tatizo kubwa ni pamoja na Wilaya ya Kalambo na ni kwa sababu kimsingi mikoa ya pembezoni imekuwa disadvantaged kwa kipindi kirefu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati wanapanga ikama ya safari hii naomba aitazame kwa jicho la huruma Wilaya ya Kalambo, tunahitaji kuziba pengo kubwa sana la upungufu wa watumishi katika kada hii ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wenzangu nami nilirudie. Ni matarajio yetu kwamba tunapoongea na Serikali tunaongea nayo kwa ujumla wake na mpango mzima wa kubadilisha utaratibu wa circle ya bajeti ni ili kama kuna jambo ambalo halikupita katika Wizara husika tunapokuja kuhitimisha bajeti basi tuhakikishe jambo hilo linakuwa addressed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna hili suala zima la ujenzi wa vituo vya afya pamoja na kumalizia zahanati. Katika hali ya kawaida iko chini ya TAMISEMI lakini TAMISEMI na Wizara ya Afya ni Serikali moja na Serikali yenyewe inatokana na CCM, kwa hiyo tunaongea na Serikali ya CCM. Mlikuja kwenye Kamati ya Bajeti mkasema last time mnaenda kuleta bei halisia ili tukamalizie maboma na tuanze kujenga vituo vya afya. Sasa mwenzenu katika Wilaya ya Kalambo yenye kata 23 na vijiji 112 kuna vituo vya afya vitatu tu; mnaweza mkaona jinsi gani uhitaji ulivyokuwa mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamejitolea wamejenga kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali hii kwamba wajenge kufika usawa wa lenta na baadaye Serikali i-take over na hakuna hata siku moja ambayo Serikali imekuja ikasema utaratibu ule umefutwa. Kwa hiyo, bado ni jukumu letu ni jukumu la Serikali kuhakikisha Wananchi ambao wamejitoa kwa moyo wao kazi nzuri hii iweze kumaliziwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mapendekezo, kwa namna iliyo nzuri tulipendekeza shilingi hamsini iwe kwenye tozo ili iende ku-address tatizo hili la ujenzi wa vituo vya afya pamoja na kumalizia zahanati ambazo wananchi wamejitoa kwa moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wasikie na watie uzito katika haya ambayo nnayasema naomba niishie hapo nashukuru sana.