Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba Mheshimiwa Waziri mwaka jana nilieleza hapa kwenye bajeti zipo zahanati tano jimboni kwangu zimejengwa, zimekamilika ila hazijafunguliwa kwa sababu hakuna wahudumu, lile tatizo limeendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira mengine nimshukuru sana Waziri wa Ardhi, jana amefanya kazi kubwa, tena inahusu na Wizara yako Mheshimiwa Ummy.

Mheshimiwa Lukuvi namshukuru jana ameweza kumnyang’anya eneo mtu mmoja ambaye anapenda sana kuibaiba sana maeneo ya watu. Aliwahi kuiba eneo akamkabidhi Mkuu wa Mkoa Makonda pale Dar es Salaam, Mheshimiwa Lukuvi akamnyang’anya, jana tena kaenda kumnyang’anya hekari 4000, ambazo alitaka kuwaibia wananchi wa Jimbo la Mchinga katika kijiji cha Ruvu na kijiji cha Mchinga, kwa hiyo namshukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia aliyoitumia alijenga zahanati mbili, moja Mchinga na moja Ruvu. Kila alipokuwa anaambiwa azikabidhi akawa hataki kuzikabidhi, akamtumia Afisa Mipango Miji wakaenda wakaghushi hati ya kumiliki ardhi, alipoona Mheshimiwa Lukuvi anakomaa naye wakaamua kusita, kwa hiyo zile zahanati mbili ambazo jana lile eneo amenyang’ anywa, Mheshimiwa Ummy nafikiri sasa hivi muagize Mkuu wa Mkoa tuzichukue sisi. Tumemnyang’anya eneo lakini zile zahanati ziwe kwetu, kama hataki kabisa basi akavunje haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la upatikanaji wa dawa. Mheshimiwa Waziri siyo kila taarifa wanayokuletea watendaji wako uiandike na ui-copy kama ilivyo. Nimekisoma hiki kitabu, nimejiridhisha kwamba hii taarifa uliyoisoma jana haukuipitia labda kabla haujaja Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hali ya upatikanaji wa dawa Mkoa wa Lindi ukurasa 126, wameeleza kwamba Mkoa wa Lindi umepata dawa kwa asilimia 70. Lindi ina Halmashauri sita, ukienda kwenye upatikanaji wa dawa kwa Halmashauri, Halmashauri ya Kilwa asilimia 77, Lindi DC asilimia 80, Lindi MC asilimia 84, Liwale asilimia 88, Nachingwea asilimia 81, Ruangwa asilimia 86, ukitafuta wastani ni wastani wa asilimia karibu 83. Lakini huku kwenye Mkoa umetuandikia kwamba tumepata dawa kwa asilimia 70, ukitazama kwenye mgao wa Halmashauri asilimia wastani wake ni asilimia 83. Mlifanya mahesabu? Ndiyo maana nikasema wakati umeletewa hii taarifa haukuipitia, kwa hiyo, najua kwamba asilimia ya dawa tuliyopata Mkoa wa Lindi ni asilimia ndogo kuliko Mikoa yote. Hii inasikitisha, mmetusahau kwenye walimu, mmetusahau kwenye madaktari, mnaendelea tena kutusahau kwenye dawa. Ninaomba sana hali ya upatikanaji wa dawa katika Mkoa wetu wa Lindi siyo mzuri, naomba muongeze hiyo kasi ya kutuletea dawa katika Mkoa wetu wa Lindi. (Makofi)

Suala lingine ni suala la vifo vya akina mama hususan wanaokwenda kujifungua. Mheshimiwa Waziri wewe ni mwanamke, nilifikiri kwamba katika jambo ambalo utalipigania kwa dhati kabisa ya moyo wako, uache legacy, kila siku kina mama 30 nchi hii wanafariki wakiwa wanajifungua. Umeikuta hali hiyo hivi sasa mwaka wa pili hali ipo hivyo hivyo, utaondoka miaka mitano, hali ikiwa hivyo utaacha historia gani! Akina mama watakukumbuka kwa lipi? Tunaomba sana na nimewasikia Wabunge hapa wanakusifia sana na mimi pia mwaka jana nilikusifia, lakini nimegundua haya maneno mazuri ni kwa ajili ya asili yako tu ya kutoka Tanga, watu wa Tanga mnajua vizuri Kiswahili, mnaongea vizuri, tunahitaji ufanisi na utendaji, tunataka tuone uache legacy kwenye hii Wizara. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa nimesema Tanga tu, maneno yale mazuri kwa sababu ya Tanga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana tunahitaji matendo, ninataka mtu ambaye ana-perform na ndiyo maana nilisema mara ya kwanza, nimempongeza sana Mheshimiwa Lukuvi tumempelekea tatizo la ardhi, mtu anataka kunyang’anya watu ekari 4000 katika mazingira ya wizi tu, watu wa Serikali mpo, huyu Azimio Housing Estate kwa nini hii kampuni na yenyewe msiifungie kabisa? Kila siku anafikiria kuiba maeneo tu ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tena kumshauri Mheshimiwa Waziri, hatuhitaji maneno mengi kwenye vitabu hivi, tunahitaji action, tunahitaji utekelezaji. Bajeti yako inapungua umechukua mechanism gani kuishauri Serikali ikuongezee bajeti, usiwe unakubali tu unaletewa bajeti ndogo na wewe unakubali. Hii shilingi trilioni 1.1 haikutoshi, matatizo ya afya ya nchi hii ni makubwa kuliko kiwango cha pesa. Inawezekana hata hii shilingi trilioni moja usiipate yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu suala la magari ya wagonjwa niliona wakati fulani Mikoa ile ya Mwanza wapi kule, watu wanapewa magari ya kubeba wagonjwa, kwetu huku mbona hatuletewi? Mimi katika vituo vyangu vitatu, Kitomanga, Lutamba na pale Milola magari yake yote yamechakaa na sasa hivi hayafanyi kazi, yamekufanya kabisa yote, lakini wenzetu tumeona mnawapatia magari, je mna mpango gani na sisi kutupatia magari ya wagonjwa? Hii distribution of resources uwe sawa, hii keki ya Taifa tuigawane sawa, tunaposhindwa kutenda haki katika mgawanyo wa hii keki ya Taifa tunasababisha matatizo na wengine tutakuwa tunajihisi wanyonge. Sasa binadamu anapojihisi mnyonge ni tatizo kubwa sana, nisingependa katika Taifa hili wengine tujione wanyonge na wengine wawe siyo wanyonge.

Kwa hiyo, naomba sana hakikisha katika bajeti hii unatupatia gari la wagonjwa japo moja katika Halmashauri yetu na specifically liende kwenye Jimbo la Mchinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la vyeti fake limeathiri sana Halmashauri yetu. Ziko zahanati mbili zimefungwa hivi sasa ninavyokuambia kwa sababu watumishi wake wote wameonekana wana vyeti fake. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri uchukue initiative za haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani.