Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Afya na nguvu ni bora kuliko dhahabu; mwili wenye nguvu ni bora kuliko utajiri mwingi. Joshua Bin Sira 30:13. Hakuna utajiri ulio bora kuliko afya ya mwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hayo kwa sababu hatuwezi tukazungumzia maendeleo ya aina yoyote kama hatuwekezi ipasavyo kwenye afya ya binadamu. Lengo la Tatu la Maendeleo Endelevu ya Dunia yanazungumzia afya bora kwa rika zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya afya ya Tanzania ikoje? Hali ya afya ya hapa kwetu Tanzania kwa kiasi kikubwa ambapo tuko zaidi ya watu milioni 50 inatisha. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha ifikapo mwaka 2030 zaidi ya Watanzania 85,000 watafariki kwa magonjwa ya moyo; Watanzania 42,000 watafariki kwa magonjwa ya saratani; na Watanzania 68,000 watafariki kwa magonjwa haya ya ajali. Sasa tujiulize tunashindaje changamoto zote hizi? Tufikiri globaly na tu-act locally tutaweza namna gani kupambana na changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, magonjwa ya moyo, magonjwa ya kansa, magonjwa ya figo, mashine kwa mfano ya kusafisha damu kwa kiasi kikubwa mashine hizi ziko Dar es Salaam zaidi na ni ghali sana. Kwa mfano sindano moja wakichomwa ni shilingi 67,000 unaandikiwa sindano 12, huyu Mtanzania hata wa kipato cha kati ataweza kumudu kiasi gani? Tujiulize ile linear accelerator kwa ajili ya magonjwa ya kansa ambayo tumeimba kwa zaidi ya miaka kumi ifungwe pale Ocean Road ni lini itafungwa? Tumekuwa tukizungumzia uwekezaji kwenye sekta ya afya kwamba Hospitali za Apollo kutoka India watakuja kuwekeza hapa Tanzania ili kusaidia foreign kuwekeza kwenye sekta ya afya ili kuwe na ushindani hali ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiri hivi karibuni nilikuwa natibiwa Hospitali ya Zydus kule India. Ni hospitali ya watu binafsi ina vitanda zaidi ya 550, ina vitanda vya ICU 162 na ina mashine za kisasa ukilinganisha na sisi kama Taifa la Tanzania. Hospitali za namna hii namna gani tunafanya mazungumzo nao kwa sababu penda tusipende dunia leo imekuwa ni kijiji, kama hapa kwetu Tanzania hatujitoshelezi tunaweza tuka-source hata wenzetu wa nje wakawekeza kwetu hapa Tanzania. Kwa sababu leo hii sekta ya afya ina upungufu wa wataalam zaidi ya 58% na Afrika Mashariki hapa Kenya, Uganda na Tanzania, Tanzania tunashika nafasi ya chini sana katika kuwa na watalaam wa kutosha katika sekta ya afya. Sasa changamoto zote hizi tunashiriki namna gani kuziondoa? Ndiyo maana nimesema afya ya mwili ni bora kuliko utajiri mwingine wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa kawaida kabisa wakati ilivyotokea kikombe cha babu, ni Watanzania wangapi waliokimbilia kwa babu, ni Watanzania wangapi waliopoteza maisha kwenda kwa babu na namna gani Serikali ilijitoa kwenye sera yake ikaenda ikawekeza miundombinu kwa babu na Serikali karibu yote ikahamia kwa babu kwa ajili ya matibabu kwa babu? Sasa unaweza kuona tu kwamba Watanzania wengi ni kwamba afya, afya, afya ziko katika hali ambayo siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano watalaam mabingwa kutoka nje wanaokuja hapa nchini, kupata vibali tu vya kufanya kazi (working permit), inachukua miezi sita mpaka minane lakini unawapa kwa muda wa miaka mwili tu! Sasa wale mabingwa hawawezi wakasubiri muda wote huo. Badala ya kuwapa miaka miwili wape basi hata miaka mitano au zaidi ili kuwapa confidence ya kuwekeza katika sekta ya afya. Hata tukijiuliza miaka 10 iliyopita ni mabingwa au ni taasisi ngapi za kidunia zimewekeza vizuri katika sekta ya afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nikienda Vunjo, Hospitali ya Kilema nimeizungumzia na hata leo asubuhi nimeizungumzia. Tukiangalia Hospitali ya Kilema ina zahanati zaidi ya 13 za Maua, Makomu, Womboni, Mboni, Mbahe, Rauya, Arumeli, Uparo, Mawanjeni, Uchira, Miwaleni, Iwa na Yamu lakini Zahanati ya Miwaleni imefungwa moja kwa moja haina hata wataalam.

Mheshimiwa Mwentekiti, sasa ni namna gani tunawekeza akili na fikra zetu ili bajeti ya Wizara hii iweze kutosheleza mahitaji. Nikiri bajeti ya Wizara hii ni kidogo mno katika kutekeleza majukumu yote katika sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya mwanadamu na utu wa mwanadamu ni afya kwanza. Mwanadamu aliyeshiba vizuri na mwenye afya nzuri, na nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na Naibu wako kwa kazi kubwa mnayofanya lakini bajeti yenu kidogo mno. Katibu Mkuu atadaiwa huku na kule, Dkt. Mpoki, anafanya kazi nzuri tu lakini sasa afanyeje wakati bajeti ni kidogo kiasi hiki? Kwa hiyo, tujifikirie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge, tumepewa mamlaka na Katiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Tukiacha tofauti ya itikadi zetu hapa tukaamua kuisimamia Serikali vizuri, tunaweza tukapangua hata bajeti hii tukaiongezea Wizara ya Afya bajeti zaidi ili binadamu aweze kushiba vizuri, binadamu aweze kuwa na uelewa vizuri na aweze kuondokana na haya matatizo ambayo ni makubwa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya miundombinu katika Hospitali ya Kilema pamoja na Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi. Tuna changamoto ya uzio kwa mfano pale Mawenzi na miundombinu yote ile ni chakavu. Pale Kilema hatuna Kitengo cha ICU, ujenzi wa jengo la utawala ni matatizo, uzio wa hospitali ni matatizo, nyumba za watumishi ni matatizo, marupurupu kwa watumishi kwa ujumla wake ni matatizo wanafanya kazi katika hali ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde tuangalie ni namna gani Wizara inashirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuwa na mawazo mapana zaidi na kuangalia wenzetu duniani wanafanya nini ili tuweze kuondokana na changamoto hizi tukawekeza vya kutosha katika sekta hii ya afya ambayo ni duni kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujifunze kwa wenzetu duniani na tuangalie wanafanya nini, kwa sababu kila mtu hapa atazungumzia Jimbo lake la uchaguzi, atazungumzia sehemu yake, bajeti ni kidogo, lakini Wabunge tunayo nafasi, tunayo nguvu, tunao uwezo wa Kikatiba wa kuweza hata kupangua bajeti hii, kwa sababu bajeti kubwa haijasomwa na wakati wa kukaa na Serikali ili Wizara hii ikaongezewe bajeti ili performance ya Watanzania katika Wizara ya Afya iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde niombe tena, Serikali inaweza ikafanya maamuzi kwenye miundombinu, barabara, reli na mengineyo wakawekeza zaidi kwenye private sector, lakini fedha tunazopata ndani tukawekeza zaidi kwenye ile miundombinu inayokuza utu wa mwanadamu zaidi. Kwa mfano, afya, elimu ambayo ndiyo kipaumbele namna gani wataalam wetu wa humu ndani tunawapa haki zao, stahili zao, watumishi wetu. Madaktari wetu wa humu ndani wako kwenye hali gani, Wakunga wako kwenye hali gani, wauguzi wako kwenye hali gani, vituo vyetu vya afya viko kwenye hali gani. Kwa mfano, pale Vunjo Kituo cha Afya cha Kirua, Kituo cha Afya cha Mwika na Hospitali ya Marangu vile vituo vyote vya afya na zahanati zote zinazotoa huduma wanatoa huduma nzuri sana lakini katika mazingira magumu sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali za Rufaa kwa mfano, KCMC, Bugando angalia Hospitali ya Muhimbili kweli tunazungumza kwamba hali ya Muhimbili bado ni tete sana angalia wagonjwa wanalala ndani wane, watano wajawazito hawa zaidi ya wawili watatu, wengine wako katika hali ambayo siyo nzuri sana tuwe wa kweli. Unaweza ukasema hapana, lakini ukienda Hospitali ya Mwananyamala, Temeke haziridhishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba chonde chonde Wizara hii naomba iongezewe bajeti ili iweze ikatoa huduma yake kwa kukuza utu wa mwanadamu. Ahsante sana.