Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Itabidi twende mwendo kasi maana dakika tano hizi hazitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo ada na inavyostahili nawapongeza sana Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, Katibu Mkuu naye anafanya kazi nzuri sana, inaoneka watu tunamsahau na timu yake pia, kwa kweli kazi inaoneka. Mimi ni mmoja wa watu ambao binafsi nikijaribu kufuatilia unaona kabisa kwamba sasa kuna mahali tunakwenda kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna mwanafalsafa mmoja anasema dunia yetu siyo mbinguni na kufanya vizuri haitoshi ni lazima tufanye vizuri zaidi. Kwa hiyo, mnafanya vizuri lakini lazima tufanye vizuri zaidi. Sasa nasema yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba ya Waziri, ukurasa 127, kiambatanisho namba tatu, anapoongelea upatikanaji wa dawa, kuna majedwali pale yanazungumzia kila Wilaya asilimia 80, 90 na mambo kama hayo lakini kwa wastani kitaifa anasema upatikanaji ni asilimia 87, ni jambo zuri. Hata hivyo, hii maana yake ni kwamba katika kila watu 10 unaokutana nao wametoka hospitalini pale, tisa watakuambia tumepata dawa tuliyoandikiwa, kitu ambacho uhalisia kule chini sio kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wasiwasi wangu ni kwamba inawezekana Bohari ya Dawa kusukuma madawa kule wilayani ndio asilimia 87 lakini upatikanaji wa dawa kwa maana ya kutoka pale ilipo kumfikia mgonjwa sio tunachokiona kinachofanana na hii 87. Biharamulo pale ukizungumza na watu kumi wanaotoka Hospitali ya Wilaya pale, ukasimama tu nje, watu watano mpaka sita wana malalamiko ya dawa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ujumbe wangu ni kwamba umefanikiwa sasa kusukuma dawa kwenda kwenye hospitali zetu lakini ukashughulike na kituo cha tiba na mgonjwa ili upatikanaji wa dawa uwe kwa mgonjwa. Kuna habari ya committed supply na actual supply. Kwa hiyo, tuone namna gani mgonjwa anapata dawa hiyo hatua inayofuata. Naomba hata CAG aende mbele zaidi afike hapo na kwenda hatua ya pili kwa sababu lazima twende kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anasema kuna shilingi kama bilioni mbili za Mfuko wa CHF hazieleweki zimefanya nini huko kwenye maeneo yetu, sio maneno yangu ni CAG. Kwa hiyo, naomba tutazame kwenye ukurasa fulani hapa kwenye hotuba unazungumzia CHF iliyoboreshwa inakwenda kutatua habari ya mipaka ya tiba kwa kutumia CHF kuondoka nje ya Halmashauri lakini hiyo haijibu matumizi ambayo hayaeleweki ya pesa ambayo tayari watu wamechanga. Wananchi wakisikia habari sisi inatuwia ngumu kuwahamasisha waendelee kujiunga na CHF. Tunaomba muende hatua ya ziada zaidi ya kuongelea CHF iliyoboreshwa kuwaondolea mipaka ya matumizi ya ile bima yao lakini ukatazame ni kwa nini pesa hizo hazitumiki kama zilivyopangiwa, anasema CAG sio maneno yangu hayo twende kinachofuata kwa sababu tunakwenda kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Biharamulo tuna vituo vya afya vitano lakini katika vituo hivyo ni kimoja tu ambacho kina mtaalamu wa maabara tena ambaye sio wa kiwango cha Laboratory Technician ni Laboratory Assistant. Maana yake kwenye vituo vya afya vyetu vyote pale hawa madaktari wetu waganga wasaidizi wanapiga ramli yaani hata mtu akisema nina dalili za malaria hawezi kwenda kupima, inabidi mganga apige ramli ndio ajue hii ni malaria ama ni nini. Tunaomba tuangalie ni namna gani tutakwenda chini hasa kwenye zile huduma ambazo ni lazima na zinamsaidia yule mganga kufanya tabibu zake kama anavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 57 mpaka 58 kwenye hotuba ya Waziri anaongelea makundi ambayo yanahitaji msamaha na anataja walemavu, familia zenye migogoro, wakimbizi, waathirika wa pombe kwamba hao ndio wanafikiriwa pale.

Mimi nikafikiria tuna 10% ile ya akina mama na vijana kwenye halmashauri na tumewapa wale kwa sababu ni makundi maalum lakini yako makundi maalum zaidi, walemavu na watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI hawa wana mahitaji zaidi, ni makundi maalum, maalum ndani ya maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute namna ambavyo na wenyewe tuwajumuishe kwenye ile 10% waangaliwe kwa upekee waweze kufanya shughuli za uzalishaji, waweze kununua bima na waweze kupata tiba lakini ukimfikiria kwenye msamaha mpaka mtu aliyeathirika na pombe, mpaka mkimbizi, wakati mlemavu hujamfikiria, nadhani vipaumbele vyetu vinakuwa sio sawa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.