Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwa maandishi katika hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakapoongelea maendeleo ya nchi hii huna budi kutilia mkazo masuala ya miundombinu, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, hii inaonesha jinsi gani Mheshimiwa Rais wetu alivyo mzalendo katika ufanyaji kazi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, sina budi kuwapongeza Mawaziri wenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, Mbunge na Naibu wake Mheshimiwa Injinia Edwin Amandus Ngonyani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kibiti zipo changamoto nyingi hasa barabara ya Bungu – Nyamisati. Barabara hii ina jumla ya kilometa 42. Naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kuiangalia kwa jicho la huruma barabara hii. Tunaiomba Serikali yangu barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami kwani kufanya hivyo inaturahisishia kwa wananchi wa maeneo ya Delta kama Nyamisati, Salale, Kiomboni, Mchinga, Mfisini na ndugu zetu majirani zetu wa Wilaya ya Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Gati la Nyamisati; naiomba Serikali yangu sikivu suala hili lipewe kipaumbele kwani gati hili lina umuhimu sana kwa wananchi wa maeneo ya Delta na Mafia kwa ujumla. Katika Jimbo langu la Kibiti lina jumla ya Kata 16, kati ya hizo zipo tano ambazo zipo katika maeneo ya Delta, kati ya hizo ni Maparoni, Mbuchi, Salale, Msala, Kiongoroni. Katika Kata za Maparoni, Mbuchi, Salale, Msala, Kiongoroni katika Kata ya Maparoni, Mbuchi, Kiongoroni kuna barabara ya kutoka Ikwiriri – Kibiti, naomba njia hii ipewe kipaumbele kwani inatuunganisha Wilaya mbili, Kibiti na Rufiji na barabara hii ambayo inapita vijiji vingi sana ambavyo ni Mchukwi, Rungungu, Nyamatanga, Ruaruke, Kikale, Mtunda, Muyuyu, Umwe, ambapo barabara hii ina jumla ya kilometa 48. Ili kurekebisha barabara hii tuna kila wajibu wa kujenga Daraja la Ruhoi kwa box karavati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ya baadhi ya vijiji vyangu hakuna mawasiliano kama Makima, Mchukwi, Nyambunda, Ngulakula, Mngaru, Nyakinyo na maeneo mengine, tunaomba tupatiwe mawasiliano ili tuboreshe kupeana taarifa kwa njia nyepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usiposhukuru kwa kidogo hata ukipata kikubwa huwezi kushukuru. Tunashukuru Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia Wilaya mpya ya Kibiti, lakini tuna ombi la barabara ya lami kutoka barabara kuu hadi tunapojenga Makao Makuu ya Wilaya na kwenda kwenye kituo chetu cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ruaruke kwenda Nyamisati. Barabara hii ina madaraja mawili ambayo ni Mkelele, Mkumbwa na Mkelele Mdogo ambayo yamesombwa na maji kwa hiyo hadi sasa barabara haipitiki kwenda Nyamisati – Ruaruke ambayo ni muhimu sana inatoka Muhoro hadi Mbwera. Barabara hii ina jumla ya kilometa 41. Awali ya yote sina budi kuishukuru Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutupatia wafadhili wa kujenga Daraja la Mto Mbuchi na Daraja dogo la Kipoka lakini yapo maeneo ya Mkelele mchakato wa kupata mzabuni, naomba ufanyike haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishakamilisha madaraja haya mawili tunawaomba tena wafadhili hawa wa DFIB, tunaomba barabara yetu ya kutoka Muhoro hadi Mbwera watujengee kwa kiwango cha tuta kubwa ili kulingana na hali halisi ya mazingira ya maeneo hayo, yanahitaji makalavati kila baada ya mita 200 kwani maeneo haya ni ya sehemu ya maji njia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka njia panda ya Kingwera kuja Mchukwi hospitali ambayo ina urefu wa kilometa tano, naiomba Serikali yangu sikivu watuwekee lami kwa barabara hii, ni muhimu sana kwani inapitiwa na wagonjwa wengi ambao wanakwenda kupata matibabu katika hospitali hii ya Mchukwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano, maeneo ya Delta; katika Jimbo langu la Kibiti naomba maeneo ya Delta watuangalie kwa jicho la huruma kwani katika mazingira haya hatuna mawasiliano ya simu. Tunaomba tupatiwe mawasiliano ya simu kwani mtu akipata matatizo hakuna njia mbadala ya kupata msaada mwingine bila ya njia ya mawasiliano. Barabara ya maeneo ya Delta naomba Serikali yangu itujengee magati ya gharama nafuu na kujaza matuta katika barabara zetu za maeneo hayo.