Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naitwa Njalu Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, maarufu Mtemi unakotoka. Kwanza nianze kuwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Itilima kwa kuweza kuniamini kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga hoja ya Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri aliyoizungumzia hasa inalenga vijana kupata ajira, amezungumzia suala la viwanda, nchi yetu imekuwa na viwanda vingi, viwanda vingine bado vinafanya kazi na vingine vilisha-expire.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Rais wasaidizi wake wakiifuatilia vizuri, na wakitekeleza kwa kasi wanayoifanya ni imani yangu tunaweza tukatoka hapa tulipo tukapiga hatua nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda ni lazima miundombinu yote iwe kamili, ninamshukuru Mheshimiwa Muhongo leo amejaribu kutoa ufafanuzi kuhusu mambo ya umeme. Viwanda vikubwa nchini lazima umeme uwepo saa zote, kwa sababu kiwanda kinapoendeshwa umeme ukikatika mwekezaji atakuwa na gharama kubwa sana.
Mheshimwa Mwenyekiti, jambo jingine ni lazima sasa Serikali ifike muda itenge maeneo maalum kwa ajili ya viwanda, na tunapozungumza viwanda maji yawepo na barabara ziwepo za kutosha hasa kule mali ghafi inakopatikana, utakuta maeneo mengi mali ghafi zipo lakini haziwezi kufika katika sehemu husika kwa sababu ya barabara hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kwenye Jimbo langu ninakotoka nashukuru sana Mheshimiwa Rais amempandisha Mheshimiwa Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi, alipokuja kilometa kumi tulitumia saa mbili kufika tunakokwenda, kwa kweli ni hali tete na mbaya sana. Haya maeneo yote yakishawekewa utaratibu mzuri, miundombinu ikakaa vizuri, basi katika haya yote tunayoyazungumzia, yanaweza yakatekelezwa vizuri na yakaleta matunda kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuimarisha kilimo ili viwanda tunavyovizungumza hivi viweze kuzalishwa katika maeneo husika ili mali ipatikane ya kutosha. Ukiangalia nchi yetu inatumia gharama kubwa sana hususani kwenye kipindi hiki cha njaa, lakini ukifuatilia kwa undani zaidi, utakuta ni Serikali haitekelezi wajibu wa kupeleka fedha au kuimarisha watendaji kwa maana ya Maafisa Kilimo katika maeneo husika zikaweza kuzalishwa malighafi za kutosha katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia Nyanda za Kusini, utakuta mbolea inaenda muda muafaka, pembejeo zinaenda muda mufaka, lakini leo tunakotoka katika Majimbo yetu, unaweza ukakuta tunavyoongea mpaka leo hata pembejeo hazijafika katika maeneo husika, tayari mkulima yule ataathirika tu kwa namna nyingine na ataanza kulia Serikali. Basi ifike muda muafaka mambo haya yaweze kutiliwa nguvu na kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, ili wananchi waweze kufaidika na kasi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu Mheshimiwa Rais alipokuwa akifanya kampeni, alitoa ahadi mbili, barabara ya kutoka Budalagujiga kwenda Mwabasabi, kwenda Nanga na akatoa ahadi ya tatizo la machungio katika vijiji vinavyoishi kando kando mwa mpakani, vijiji hivyo ni Nyantugutu, Pijulu, Mwaswale, Mwamtani na Kuyu, vyote hivyo kuna changamoto kubwa katika maeneo husika. Ningeiomba Serikali kwa ahadi ya Mheshimiwa Rais, nayo iweze kufanyiwa kazi ili wanachi hao waweze kuendelea kuamini na kasi ya utekelezaji ya awamu ya tano.
Mheshimwa Mwenyekiti, tunayo changamoto nyingine, kuna bwawa katika Kijiji cha Habia, limejengwa mwaka 2006. Takribani ya milioni 700 hadi 800 zimeshapotea pale, hakuna chochote kinachoendelea, ukiuliza wakandarasi walitoka Dar es Salaam, hela ile imepotea ukifika pale kwenye site unaletewa kitabu na mtu amebaki pale, kuendelea kusubiri Serikali inasema nini. Nimuombe Waziri wa Maji, jambo hili alitolee majibu, kwa sababu wananchi wa eneo hilo, walitoa eneo lao, lakini hakuna faida yoyote wanayoipata na matokeo yake watu wanapoteza maisha katika eneo lile husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali ya Chama cha Mapinduzi iendelee na kasi iliyonayo, kwa kutekeleza ahadi wanazozisema na kuzifanyia kazi papo kwa hapo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista Mhagama, alikuja katika Wilaya yetu, siku hiyo hiyo akaelezwa kilio cha wananchi na akatoa majibu na hivi sasa wananchi wale walipata alichokiahidi mahindi tani 400, hongera sana Mama, chapa kazi. (Makofi)
Ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, alitembelea katika kituo chetu cha Nkoma, nadhani hatua zimeshachukuliwa na inaendelea kufanyiwa kazi, hongera sana endelea na moto huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya na Mkoa wetu wa Simiyu ni mpya, bado hatujaungana na Mikoa mingine kwa maana ya lami, ninaomba sasa kilometa 52 zinazotoka Bariadi kwenda Maswa - Migumbi nazo basi Mkandarasi apatikane ili wananchi waweze kuuza mazao yao kwa bei nzuri zaidi. Ukizingatia Wilaya yetu na Mkoa wetu, ni miongoni mwa Wilaya zinazolima kwa wingi sana. Mfano hivi sasa tunavyozungumza choroko zimeshaanza kuuzwa lakini barabara ni mbovu, kwa hiyo mwananchi ataendelea kupata bei za chini. Lakini yote haya yakiwekwa vizuri tunaweza tukafanya kazi kubwa na nzuri zaidi ikawa na matunda na majawabu ya haraka zaidi iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa uvumilivu uliouonesha leo, kweli umedhihirisha kwamba wewe ni Mtemi, umevumilia vya kutosha na hatimaye umetoa majibu, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja ya Hotuba ya Mheshimiwa Rais