Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kunifanya kuwa mchangiaji wa pili kwa hotuba hii iliyotukuka ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ambayo imebeba maudhui ya Wizara zote, imesheheni mipango na mikakati madhubuti ambayo kama itatekelezwa hivi ambavyo imewekwa, kwa hakika itatutoa Watanzania hapa tulipo leo na kutufikisha kwenye maisha ya uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Wazari Mkuu kwa hotuba hii nzuri, pia niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili, ambao pia wameleta hotuba yao mbele ya Bunge lako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika tu kwamba kwa bahati mbaya nilitarajia nipate mawazo mbadala, lakini yameshindikana, hata hivi nadhani tutakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubaliane na mipango pamoja na mikakati yote ambayo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imebeba. Maeneo ambayo nilipeda nitoe ushauri na niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu kuifanyia kazi, katika kipindi hiki cha mwaka 2016/2017, moja ni Kitengo cha Maafa.
Katika hiki Kitengo cha Maafa kwanza nimpongeze sana Mkurugenzi wa Kitengo hiki kwa kazi yake nzuri anayoifanya mpaka sasa, licha ya changamoto alizonazo zinazoendana na ukosefu wa nyenzo za kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupitia makabrasha ya kitengo hiki, nilibaini kwamba pamoja na nia nzuri ya kitengo hiki kukabiliana na maafa, pamoja na jitihada nyingi zilizofanyika kuwajengea uwezo wanaofanya kazi katika kitengo hiki, bado kitengo hiki hakijawa na nguvu ya kutosha kuweza kukabiliana na changamoto za maafa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe jitihada za makusudi zifanyike kuhakikisha kwamba kitengo hiki, pamoja na kujengewa uwezo wa kinadharia ambao kwa sasa wameendelea kujengewe kupitia miradi mbalimbali ingefaa pia kitengo hiki sasa kiwe na vituo maalumu vyenye nyenzo maalumu za kuweza kukabiliana na maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ni kwamba wakati Dodoma na Kondoa wanalia kwelea kwelea responsiveness ya kitengo kinachohusu maafa ilikuwa ndogo sana, huu ni ushahidi kwamba bado tuna changamoto kubwa kwenye eneo hili, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilipenda nichangie ni eneo la elimu. Wakati nachangia jana nilimueleza Mheshimiwa Spika kuhusu hali ya Jimbo langu la Madaba. Jimbo letu la Madaba ni Jimbo changa lina takribani miezi michache sana na Halmashauri ya Wilaya nayo ina miezi michache tu. Lakini upande wa elimu kama ilivyo katika maeneo mengine tuna changamoto nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao walimu zaidi ya 412 ndani ya Wilaya ya Songea, walimu hao Wilaya ya Songea inahusisha pia Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, walimu hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu pamoja na kwamba wana hizo sifa. Nimeomba Chama cha Walimu kiniwasilishie nyaraka mbalimbali ambazo nitaziwakilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili mtusaidie kutanzua tatizo hili kwa sababu ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya elimu katika Halmashauri yetu na Wilaya ya Songea kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo ningependa nitoe mchango wa kina ni eneo la soko la mazao ya mahindi. Kama unavyojua Mkoa wa Ruvuma ni ghala la Taifa la chakula. Mkoa huu kwa miaka mingi umeendelea kuzalisha chakula cha kuwalisha Watanzania, katika Mkoa huu Halmashauri Wilaya ya Madaba, Jimbo la Madaba lina wakulima ambao wanazalisha sana mahindi ambayo yanachangia sana kwenye chakula cha Taifa letu. Kwa bahati mbaya mfumo wa manunuzi wa haya mahindi bado siyo rafiki kwa wananchi wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa bado tunategemea kituo kimoja cha Madaba, yapo maghala katika kila Kata yanajengwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kupitia mradi wa BRN. Maghala haya mpaka sasa hayajakamilika, na ujenzi wake umesimama kwa muda mrefuwakandarasi bado wanalalamika hawajalipwa.
Naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati tunaendelea na mchakato huu tuhakikishe kwamba ule mchakato ambao umesimama katika vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya Madaba ya kujenga na kuimarisha maghala ukamilike kwa sababu wananchi wa Jimbo la Madaba wataanza kuvuna mwezi ujao na watahitaji kuhifadhi mazao yao. kama ambavyo ulisema mwenyewe Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipotembelea Mkoa wa Ruvuma, ulishauri kwamba NFRA wanunue mahindi katika vituo vilivyoko vijijini ili kuwaondolea Wananchi adha ya kusafirisha mazao haya kuyapeleka katika vituo maalum vya mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yetu ya Madaba pia inachangamoto kubwa sana ya maji. Mji wa Madaba pekee na Kijiji cha Mkongotema ndiyo wenye maji yanayotiririka, lakini wingi wa mabomba hauwiani na idadi ya wananchi waliopo. Ipo miradi iliyofadhiliwa na World Bank, miradi hii imetekelezwa katika vijiji vitatu vya Mkongotema, Lilondo na Maweso. Kwa bahati mbaya miradi ya Maweso na Lilondo imesimama kwa muda mrefu sana, kwa vyovyote vile jitihada zilizofanyika mpaka sasa kubwa na niishukuru sana Wizara husika kwa kutufikisha pale ambapo tumefika. Ninaomba sana tunapoendelea na mchakato huu zoezi hilo pia la kukamilisha hii miradi ya maji katika maeneo yaliyobaki liendelee, lakini pia niombe sana Mji wa Madaba una kilio sana cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo ambao wamekuja ndani ya Jimbo langu na kushirikiana na wananchi kutatua kero zinazowakabili kwenye eneo la afya na eneo la umeme. Hivi ninavyokuambia Mheshimiwa Sospeter Muhongo yupo kwenye mchakato wa kukamilisha umeme wa maeneo ya Mji wa Madaba na Mungu bariki Disemba tutakuwa na umeme, ninaniomba sana zoezi hili liendelee, wananchi wa Madaba wanatambua sana juhudi za Mheshimiwa Sospeter Muhongo, lakini pia wanatambua sana jitihada za Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu za kuhakikisha kwamba Madaba tunapata Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho na la muhimu sana ni kwamba tulipokuwa tunaelekea uchaguzi wa mwaka 2015 vipo vijiji vingi vilivyozaliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kama ambavyo vilizaliwa katika maeneo mengine ya Songea Vijijini. Vijiji hivi bado havijapata usajili wa kuduma na kama vimepata havija…
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.