Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na nianze kwa kuwapa hongera sana Waziri, Naibu Waziri na timu yako ya wahandisi mlioko Wizarani na wahandisi walioko TANROADS, mnafanya kazi nzuri hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitakuwa na machache sana. Mheshimiwa Waziri mimi nataka kukukumbusha tu suala la kisera kwanza. Alikuwa anatukumbusha Ndugu Chenge mchana hapa, ujenzi wa barabara za nchi hii zinahitajika kila mahali sana kabisa na nchi yetu bahati nzuri ni kubwa. Naomba tujirejeshe kwenye sera ya ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulishakubaliana kwa mujibu wa Sera ya CCM ya miaka 20 kwamba tutajenga barabara za kuunganisha mkoa na mkoa, tungejielekeza katika maeneo hayo. Kuna mikoa ambayo imeunganishwa tayari na kuna mikoa mingine haijaunganishwa. Na fedha ambazo mnatenga kwenye bajeti ni kidogo mno, sasa sungura mdogo lakini fedha mnatapanya na baadhi ya maeneo kusema kweli hayana umuhimu wa kiuchumi leo. Kuna Mkoa kama Katavi kwa mfano, Mkoa wa Katavi haujaunganishwa na Kigoma, Mkoa wa Kigoma haujaunganishwa na Geita, Mkoa wa Kigoma haujaunganishwa na Shinyanga, Mkoa wa Kigoma haujaunganishwa na Tabora ingawa kuna juhudi hizo kidogo za kilomita chache, Mkoa wa Kigoma haujaunganishwa na Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri wewe umetembea mpaka pale Kasangezi nilikuona siku ile, yale ndiyo maeneo ambayo yanazalisha chakula kingi. Sisi ndiyo tunalisha migodi mingi iliyoko ukanda wa ziwa. Naomba mjirejeshe kwenye sera tuweze kufanya haya mambo kwa utaratibu, otherwise kila mahali barabara, uwezo huo kwa mara moja hatuna. Mheshimiwa Waziri wewe unajua barabara ya Kigoma - Nyakanazi huu ni mwaka wa 20 barabara haikamiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha kutoka Kidahwe mpaka Kasulu kilometa 50 huu mwaka wa tisa haikamiliki. Sasa nimeona kwenye bajeti yako umetenga bilioni 19, lakini umesema hizo ni za Kidahwe – Kasulu hizo ni za Kabingo – Nyakanazi na unazungumza kwenye hotuba yako unasema katika fedha hizo hizo ni za upembuzi yakinifu na kuandaa ujenzi wa barabara ya Manyovu – Kasulu – Kibondo – Kakonko, na unasema ni za maandilizi ya ujenzi. Sasa nilikuwa nakuomba hizi shilingi bilioni 19 ni ngapi zinajenga barabara ya Kidahwe tujue Kasulu na ngapi zinatoka Kabingo ziende Nyakanazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sielewi kabisa jambo hili. Hili jambo mkilifanya kisera tutafanikiwa, tutaanza na barabara ambazo zina umuhimu kiuchumi si kujenga kila mahali kwa mara moja. Nilikuwa naomba hilo liwe la kwanza Mheshimiwa Waziri, nikurejeshe kwenye sera na wewe bahati nzuri umekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya muda mrefu, hili jambo unapaswa kulisimamia wewe, hili ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapo hapo nilishazungumza na Mheshimiwa Waziri nilikwenda ofisini kwake zaidi ya mara moja, kwamba hii barabara ya Kidahwe - Kasulu haifiki Kasulu Mjini inaishia Nyumbigwa au Kanyani karibu na njia panda ya kwenda Uvinza kwenda barabara ya Katavi. Naomba kwa sababu mkandarasi yuko site inakuwa ni vigumu sana kuja kum-mobilize baadaye apatikane kwa kilometa nane zile za kuja Kasulu Mjini, itachukua muda mwingine mrefu. Maadamu mkandarasi yuko site ingekuwa ni vizuri basi kuwe na addendum au nyongeza ya mazungumzo ili aongeze kile kipande cha kilometa nane ile barabara itoke Kidahwe ifike Kasulu Mjini. Hilo naomba sana ulizingatie na liko ndani ya uwezo wako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nalizungumza, na nisipolizungumza kila mmoja atanishangaa, ni hii reli ya kati. Waziri Mbarawa, reli ya kati msiipotoshe, reli ya kati inatoka Kigoma kwenda Dar es Salaam si vinginevyo. Lakini zaidi ya hayo faida ya reli ya kati hasa standard gauge ni kwenda kubeba mzigo mkubwa na mzito.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri leo hata Mheshimiwa Rais wakati anazungumza na vijana wa UDOM hilo kalizungumza kwamba tunajenga standard gauge kwa ajili ya kubeba mizigo mizito ili barabara zetu ziwe salama. Sasa economics zake ziko hivi, ukitoka Dar es Salaam ukaenda mpaka Tabora, Isaka, Keza, Msongati na Kigali ni mbali zaidi kuliko kutoka Dar es Salaam ukaja Uvinza, ukaenda Msongati, ukaenda Bandari ya Kigoma tofauti yake ni kilometa 700, hizo ni economics tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uking’ang’ania hii route mnayotaka kuichukua mnakwenda kuinufaisha nchi ya Rwanda, maana Kigali wanataka ile hub itoke Isaka pale iende Keza, iende Kigali - Msongati na Msongati ni South East ya Burundi. Msongati ambako kuna deposit ya nickel, coal, cobalt na copper iko karibu na Mkoa wa Kigoma, ni South East.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ile reli ikitoka Msongati – Uvinza ni karibu na Bandari ya Kigoma ni karibu na kwenda Bandari ya Dar es Salaam, hizo ni economics tu. Msihangaike na hiyo route ya mbali, tuanze na hii route ya karibu kwenye mzigo, kwenye mali na andiko la economics of geography inatueleza kwamba (na liko pale TRL, aliandika Bwana Karavina akiwa Mkurugenzi pale TRL) kwamba mzigo ulioko DRC ndiyo uatakofanya reli ya kati ya standard gauge iwe na maana kiuchumi, ni tani milioni 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nashangaa eti mnaanza upembuzi yakinifu kutoka Tabora mnakwenda Shinyanga, kubeba samaki? Hizi reli ni za kiuchumi hizi. Dhamira nzuri ya Mheshimiwa Rais ya kujenga reli ya standard gauge itusaidie kuokoa na barabara zingine hizi ambazo zinaharibiwa kwa kubeba mizigo mizito. Tafadhali sana mjielekeze kwenye historia ya mambo haya. Sasa sina haja ya kuzungumzia habari ya reli ya kati kwa sababu nadhani hiyo imeingia, ni economics tu. Bashe amezungumza asubuhi, tuma watu wako basi wafanye hizo cost benefit analysis tuone ni wapi kuna nafuu ya kiuchumi zaidi na tuna ushindani zaidi kuliko sehemu nyingine, simple.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilisemee kidogo, nimesoma kwenye taarifa ya Kamati kwamba Shirika la ATCL ambalo tumelifufua kwa juhudi kubwa na kila mmoja ananufaika nalo kwamba si mwachama wa IATA. Sasa swali dogo tu, kwa nini si mwanachama wa IATA na kama sio mwanachama wa IATA maana yake nini kiusalama? Kwa sababu tusifanye mambo tumefumba macho, exactly!

Mheshimiwa Naibu Spika, IATA ni Shirika la Usalama la Anga la Dunia, sasa Air Tanzania nimesoma kwenye paragraph moja kwamba ATCL sasa sio member wa IATA, kwanini sio member wa IATA? Sasa juhudi zote hizi, zinakuja ndege kubwa, tunataka kwenda China, twende Marekani, lazima tuwe member wa IATA kwa sababu masuala ya kiusalama na masuala mengine ya anga.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa nizungumzie; Mheshimiwa Waziri tunaomba utupe comfort hii barabara ya Manyovu ambayo unasema ni barabara ya East Africa chini ya NEPAD ufadhili wa African Development Bank inafanyiwa upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka kujua, bila shaka kuna time frame upembuzi yakinifu unaisha lini na ujenzi huu unaisha lini? Kwa sababu tayari kuna problem kwamba tayari kutoka Manyovu kuja Kasulu Mjini nyumba zimewekwa alama “X” kwamba watu watalipwa fidia. Sasa hebu mtueleze, na mimi ningeshauri strongly Mheshimiwa Waziri kwamba mna wataalam wengi pale, tuwe na vita ambavyo vinajulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ukifanya upembuzi yakinifu maana yake ni miaka kumi? Lazima kuna time frame yake; kama ni miaka miwili ama ni mwaka mmoja tuweze kujua. Ningependa Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha utueleze barabara ya Manyovu - Kasulu - Kibondo
- Kabingo huo upembuzi yakinifu utakuwa umekamilika lini na lini barabara hiyo itaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa kabla kengele haijalia, nizungumzie kipande kidogo hiki cha Kanyani kwenda Uvinza hadi Katavi. Hicho kipande Mheshimiwa Waziri au Naibu wako amepita pale, kile kipande kinatoka Nyumbigwa pale ambapo ndiyo Kanyani zamani, mnaita ni barabara eti ya Nyakanazi kwenda mpaka Tunduma, mimi sielewi hii! Ile barabara inatoka pale Kanyani inakwenda Rungwe mpya, inakwenda Basazi inakwenda Uvinza, inakwenda Mishamo inakwenda Mpanda Stalike. Barabara ile ni muhimu sana kwa sababu ukijenga hii barabara ya Kidahwe - Kasulu kwenda Nyakanazi ile ndiyo roop ya kwenda Mkoa wa Katavi, ni barabara muhimu sana inayotuunganisha sisi na Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tafadhali sana zingatia hayo zirejeshe kwenye sera.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa sababu mmeanza vizuri. Nashukuru sana.