Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa katika hali ya afya njema. Na mimi naomba nitumie fursa hii kuchangia katika Wizara hii ya Mawasiliano na Uchukuzi. Kwanza ningependa ninukuu Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano katika nyongeza ya kwanza katika masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Katiba yetu kwenye mambo ya Muungano mojawapo ni bandari. Sasa, bandari ni uchumi wa nchi, na mpaka leo hii toka Muungano huu tulipoungana miaka 53 bado suala hili liko katika masuala ya Muungano ambayo Zanzibar wameonesha wazi kuwa wanao uwezo wa kuisimamia bandari na kuweza kujitegemea kupitia bandari yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hadi leo hii bado suala hili limewekwa katika masuala ya Muungano na inapelekea kuizua Zanzibar kuwa na ile free port kujenga port kubwa pale ambayo iweze kusaidia kupokea mizigo inayotoka Kusini kufika Zanzibar na ile ya Kaskazini kufika Zanzibar wakagawana mizigo ile badala ya kusafiri umbali mrefu katika kusambaza mizigo katika hili eneo la Afrika Mashariki. Sasa nimuombe Waziri, iko haja sasa wakatafakari kutumia ile Ibara ya 98(b) kuletwa mswada hapa ili suala la bandari hili lisiwe tena la Muungano na liachiwe Zanzibar iweze kujitegemea ili kuendesha bandari yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la Posta na Simu, hili pia ni jambo la Muungano. Tangu ilipovunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1979 lilianzishwa hili shirika, lakini mpaka sasa hivi Zanzibar hatujaona faida yake ni ipi. Kwa hiyo, namuomba Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha hoja hii basi atuambie, at least hii miaka kumi ya Rais aliyestaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuambiwa TTCL imetengeneza kiasi gani na mgao wa Zanzibar ni kiasi gani, wametupa kiasi gani na bado kiasi gani tunawadai ili tujue, kwa sababu hii ni kama mali ambayo tumempa mtu anatukamatia, lakini hatujui hesabu, hatujui kitu chochote. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atupe ufafanuzi wa jambo hili la Posta na Simu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni suala la anga. Taasisi hii inakusanya makusanyo mbalimbali kwa ajili ya nchi yetu. Lakini bado mpaka sasa hivi masuala hayo hayapo wazi, namuomba Waziri atakapokuja hapa atuambie miaka hii kumi ya Rais Mstaafu, Idara hii imekusanya kiasi gani na imetoa mgao wake kwa Zanzibar kiasi gani, na kiasi gani tunawadai kwa sasa ambacho hawajalipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne ni suala la ndege. Mwaka wa jana hapa nilitoa ushauri katika Wizara hii, kwamba ni kweli tunahitaji Shirika la Ndege na hili wala hakuna mtu analipinga, lakini nikatoa ushauri kwamba tutafute mtaalamu wa masuala ya ndege, biashara za ndege ili huyu atuongoze kuonesha tuanzishe shirika kwa namna gani. Mfano, leo Shirika la ATCL tulipotoa ushauri Serikali imekimbilia kwenda kununua ndege haraka haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake tumenunua ndege ya Bombardier ambayo hii ni Kampuni ya Canada, lazima wa Canada walete base yao hapa kwa ajili ya kuzifanyia mantainance hizi ndege. Lakini miezi saba baadaye tumeingia mkataba na Boeing ambao nao inabidi walete base yao kwa ajili ya kuifanyia mantainance ndege hizi za Boeing ambazo zitakuwepo hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, shirika kubwa kama hili Ethiopian Airline kwa miaka sabini zimekuwa zikifanya kazi ya biashara ya ndege kwa kutumia kampuni moja tu ya Boeing, kuanzia sasa hivi sasa baada ya kuona kwamba wameshakuwa sustain ndipo wameanza kuingia mkataba na kampuni ya Air Bus kwa ajili ya kuongeza huduma zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa lengo la kuanzisha Air Tanzania ni biashara, lakini mpaka leo biashara hii ipo Serikalini haiwezi kuendelea. Biashara ukiichanganya kwenye Serikali haiwezi kuendelea. Lazima Shirika la Ndege la Air Tanzania liwe independent ndipo liweze kuendeshwa kwa faida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; leo kuna Shirika hapa la TPDC. TPDC inafanya kazi sasa hivi lakini hili Shirika linaendeshwa kwa hasara, kwa sababu ina fedha na kodi ambazo Serikali imeziweka inalipwa na TPDC ambazo ukiuliza hizi pesa zinalipwa kwa sababu zipi haijulikani. Mwisho wa siku ikija kuombwa bajeti zao hapa ile bajeti ambayo wameomba wao kufanya kazi zao za kawaida tu hawapati, lakini wao wameshazalisha fedha na fedha zimepelekwa Serikalini, halafu Serikali inawarudia TPDC wanaambiwa kwamba waweze kujiendesha wao wenyewe. Hatuwezi kuendesha biashara namna hii.

Mhsimiwa Naibu Spika, sasa inaonekana kwamba wataalam wetu ambao wanatushauri, wanatushauri ambavyo visivyo. Sasa Mheshimiwa, Shirika hili la Air Tanzania toka lilivyoanzishwa, amesema hapa Mheshimiwa Silinde kwamba Mwalimu Nyerere alituachia ndege 11 lakini leo inaonekana ndege hizi sita imekuwa jambo la ajabu. Ndege 11 zilikuwa zinafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa shirika hili toka lilipoanzishwa linatua katika viwanja vyetu kule Zanzibar, lakini halilipi kodi hili shirika, sasa kwa nini lisilipe kodi mpaka leo hii, hapa mwaka wa jana nilimuuliza Mheshimiwa Waziri hapa akajibu swali langu akasema kwamba kuna deni la milioni 230 linahakikiwa na CAG halafu tutalipa. Juzi ninamuuliza hapa anasema hata hajui kama zimelipwa. Sasa sijui huyo CAG mpaka leo hajamaliza wakati CAG ameshawasilisha ripoti zake mara mbili hapa Bungeni hakuna hili jambo. Sasa tuambiwe kwamba ni lini Air Tanzania (ATCL) italipa deni lake la landing fees kwa Mamlaka ya Viwanda vya Ndege ya Zanzibar na tupewe deni lile halisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana alisema Bhagwanji hapa sisi sote ni ndugu moja, sasa kwa nini mnatuzamisha sisi tusipate kuendelea na hili jambo mmelifanya kama liwe la Muungano? Sisi hatujakataa kwamba liwe la Muungano lakini sasa hivi imeonyesha kamba mashirika haya kwamba sisi tunachangia lakini hatufaidiki nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba Wizara ya Muungano ilivyokuja hapa imetoa ratio ya asilimia 21 kwa
79. Nimuombe Mheshimiwa Waziri sasa, shirika limeanza kufanya kazi naomba sasa kila baada ya muda patolewe takwimu kuhusu Shirika hili kama tumepata faida au tumekula hasara ili tujue Zanzibar mgao wao ukoje. Kama mgao wetu ni hasara tushaijua hasara, lakini kama kuna faida basi tushee faida kupitia Shirika la Ndege la ATCL.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo biashara ya Ndege imekuwa ni ya ushindani mkubwa. Shirika letu hili tulilibinafsisha kwa Shirika la Ndege la South African Airways. Na tulipowapa South Africa tumewapa na zile route zetu ambazo sisi tulikuwa tunakwenda. Leo tumeshanunua ndege ya 787 Dreamliner kwa ajili ya kwenda nchi za mbali. Lakini namuomba Waziri atuambie hizi route ambao itakwenda hii ndege atakapokuja hapa atuambie kwamba ndege yetu tuliyonunua mpya kubwa itakwenda kwenye route hizi huko Ulaya na Marekani anaposema. Kwa sababu ninavyofahamu kupata route kwenda Ulaya na Marekani si jambo rahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tu Kenya Airways leo wana route mbili kutoka Nairobi kwenda London, lakini kwa sasa hivi kwa Shirika lao limetetereka kidogo katika maswala ya kiuendeshaji na Oman Air wao wana route moja kutoka Muscat kwenda London, matokeo yake sasa Oman Air wametafuta hii route kwa muda mrefu ili wawe na route mbili kutoka Muscat kwenda Heathrow lakini wamekosa, wamerudi kwa Kenya Airways wamekwenda kununua ile route.

Mheshimiwa Naibu Spika, route hii wamenunua kwa 20 million USD, tena kwa masharti ambayo Kenya Airways imewambia kwamba tunakupeni hii route tunakuuzieni lakini pia ndege yetu moja kubwa lazima muitumie kwa ajili ya kufanya kazi, yaani waikodi Oman Air; na wamekubali kulipa 20 million USD kwa sababu ya route moja tu kutua Heathrow. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri atuambie kwamba ni route zipi ambazo ndege hii itakwenda ambazo zipo available, kwa sababu tayari route tulishamuuzia South African Airline akaua Shirika letu yeye wakaendelea na shirika lao na sasa hivi wanapata maendeleo makubwa kupitia ATCL ambayo ilikuwepo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli wa mambo ni kwamba kama Serikali haitotafakari basi tunaweza tukajikuta kwamba lengo la kuanzisha hii ndege kwamba itupe faida matokeo yake ikawa ni mzigo kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani British Airways ilikuwa inakuja hapa Tanzania, Dar es Salaam lakini imesitisha safari za kuja Dar es Salaam, kwa nini, kwa sababu ya ushindani wa kibiashara na kwamba leo Emirates ana ndege nne ambazo zinakwenda Uingereza kila siku, kwa hiyo route ile ndiyo ambayo abiria wanaitumia na British Airways imejikuta kwamba imekosa abiria wa kutosha kuweza kuitoa ndege Londan kuleta hapa. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili sana kwa sababu hapa lengo na madhumuni ni kwa ajili ya kujiendesha kiuchumi ili Taifa letu liweze kufunguka na kutoka kwenye umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru Mheshimiwa Naibu Spika.