Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sote kukutana hapa kutimiza wajibu wetu wa Kikatiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara, vile vile nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo moja kubwa sana. Kwa muda mrefu tulikuwa tuna kilio cha reli ya kati. Tulipokuja kwenye Bajeti ya mwaka 2016/2017, Waheshimiwa Wabunge wengi sana tuliijadili reli ya kati ya kutoka Dar es Salaam - Kigoma - Mwanza kwenda Mpanda kwa maana ya reli ya kati yenye tafsiri ya Kitanzania. Kwa hiyo, tumeona jiwe la msingi limeshawekwa na vile vile mkandarasi anaanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa naibu Spika, nianze kuishauri Serikali kwenye hii project. Tunatumia zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa ajili ya Mradi wa Reli (Phase I). Ukitazama, kuna lot ya Morogoro mpaka Makutupora, halafu lot ya Makutupora mpaka Tabora. Ninachotaka kuishauri Serikali, kuwa na lot zenye masafa mafupi, cost per unit inakuwa kubwa. Ni vizuri kwa sababu kuna fixed cost whether ni kilometa 100, kilometa 200, kilometa 300, kilometa 600 mobilization cost unaweza ukakuta ni almost the same. Ni vizuri tukaangalia namna gani tunatoa huko mbele lot zinakuwa ni za kilometa ndefu ili angalau gharama iweze kupungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tunatumia fedha za ndani; tunachukua shilingi zetu converting into dollar kumlipa Mkandarasi. Nawaomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Wizara ya Ujenzi na watu wa TANROADs wapo hapa, waambieni hao Wakandarasi strictly sub-contracting jobs zote zifanywe na local kwa sababu zitasaidia fedha yetu tunayoitoa kubaki ndani. Tusipokuwa makini, tunaweza tukajikuta fedha nyingi zinakwenda nje badala ya kubaki ndani ya uchumi wetu. Hili ni muhimu sana kuliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza watu wa Wizara ya Nishati (REA). REA mkiangalia ilivyoanza, ilianza na foreigners lakini baadaye wali-up grade kuhakikisha sub- contracting jobs zote zinafanywa na local. Lots zilizotoka sasa hivi asilimia kubwa inafanywa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, huu ni mradi mkubwa sana, mkitusaidia kuweka hii condition kwenye kazi na hata tulivyokuwa tunazindua mradi wa maji ya Ziwa Victoria, tumemwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji kwamba 600 billions ya mradi wa maji ya Ziwa Victoria, hawa Wakandarasi waliopewa wa kutoka India wahakikishe kazi zote za sub-contracting zinafanywa na Watanzania ili tubaki na fedha ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika hili, nataka niishauri Wizara kwamba, mpango wetu ni reli ambayo itatumia umeme na hii ni miezi kama 36. Nawaombeni Serikali, hakikisheni suala la TANESCO na TRL kufikia muafaka namna gani umeme utapatikana. Itakuwa ni hatari sana kwamba tumefika mwisho, mradi umekamilika wa phase ya Morogoro suala la umeme likaanza ku-drag. Kwa hiyo, ni vizuri hivi vitu vyote vikienda vinafuatana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne katika hili la mradi wa reli; leteni Sheria ya RAHCO Mheshimiwa Waziri tuifute hapa ndani, haraka sana, ili tuweze kumpa mamlaka TRL. Halafu chagueni financial institutions moja, TIB atafute financial advisor wazunguke duniani kutafuta fedha. Hatuwezi kumaliza huu mradi kwa fedha zetu za ndani tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nina hofu, hata hii phase II anaweza akaomba Mturuki tu peke yake. Kwa hiyo, mtafunga milango ya competition. Watabaki wao kwa sababu wanatu-finance wao, wanaleta mkopo wao kwa kilometa hizo 400 zilizobaki, zitatu-restrict competition.


Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua Benki kama TIB ikatafuta financial advisor mwingine ambaye ni recognised internationally, wakazunguka kutafuta fedha, mtampunguzia kazi Mheshimiwa Dkt. Mpango kutafuta fedha kwenye Mfuko wa Hazina ku-finance hii miradi mikubwa, kwa sababu tuna miradi mikubwa sana ambayo iko katika Wizara yenu, miradi ya ndege na miradi hii ya reli. Tukiamua kuwa strategic miradi hii itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwenu ni transfer of knowledge. Nawaomba, hawa Wakandarasi wanaotujengea reli, component ya transfer of knowledge ni muhimu mno. Tutakapokwenda kwenye phase inayofuata kwa sababu tutahitaji kuwa na mabehewa na vichwa vya treni, lazima kuwe na makubaliano kwamba atakayeenda kutengeneza vichwa vya treni na mabehewa, ahakikishe anachukua watu wetu wakati wa kutengeneza ili watakaporudi hapa ndani, hizi kazi za kutengeneza vipuri, assembling zote zifanyikie nyumbani kuliko kufanyika nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza, mnafanya kazi kubwa sana ya kuifungua nchi na Mheshimiwa Rais ameamua, vision yake it is very costfull. Matokeo ya vision ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli inaweza ikatuchukua muda mrefu sana kuona matunda yake, lakini I believe baada ya miaka mitano, miaka kumi kazi hizi zinazofanyika sasa hivi matunda yake yataonekana wazi kwenye uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, mwezi Septemba tarehe 14 Mheshimiwa Rais alituahidi Nzega ujenzi wa kilometa 10. Ahadi hii ilitokea wakati yeye akiwa Waziri wa Ujenzi na Rais Kikwete juu ya ujenzi wa kilometa 10 ndani ya Mji wa Nzega.
Mheshimwia Naibu Spika, nimeangalia kitabu cha Mheshimiwa Waziri hapa hakuna any shillings ambayo imekuwa allocated kwa ajili ya hizi kilometa 10, na ukitazama kwenye bajeti ya 2016/2017, road fund fedha zilizokuwa allocated kwa ajili ya Halmashauri ya Nzega ilikuwa ni milioni 707 lakini tulichopokea ni milioni 190.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri, na wewe kwenye mwezi Desemba, wakati Rais anaenda Chato, niliongea na wewe kwa simu ukaniambia Hussein sema mbele ya wananchi na Mheshimiwa Rais kwamba daraja la Nhobola na daraja la Butandula tunajenga mwaka huu wa fedha. Shekhe mwaka unaisha, Mheshimiwa Waziri na mwaka huu tumepoteza watu watatu katika mto ule. Mheshimiwa Waziri naomba sana hili jambo lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, zimekuwepo hoja nyingi sana juu ya priority, na mimi nataka niiombe Serikali, tunapojenga hii reli tufanye cost benefit analysis kwa sababu tunawekeza fedha, ni wapi return on investimate itakuwa rahisi. Mzee Chenge ameongelea northen corridor kwamba wanakwenda speed sana, lakini wanakimbilia wapi? Wanakimbilia wafike Kigali ili waweze ku-benefit na Msongati. Tujiulize kipi kiwe mwanzo? Tufike Mwanza ama twende Kigoma ndio iwe priority? Wizara lazima ifanye hii analysis ili iweze kutuambia Watanzania kwamba tunakwenda Mwanza kwa sababu tuta-benefit mizigo ama tunakwenda Kigoma kwa sababu tuta-benefit mizigo na fedha tulizowekeza kama nchi zitarudi haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni jambo la upotezaji wa fedha za Watanzania kama tutakwenda Mwanza wakati kuna biashara kubwa Kigoma, Kalemii ama Msongati. Mzigo ulioko Msongati kama tutawahi kufika Msongati kabla ya northern corridor, sisi ndio tutakuwa na competitive advantage kuliko watu wengine. Ni vizuri sana mkafanya maamuzi haya kwa mtazamo wa kibiashara zaidi. Reli si kubeba abiria, abiria ni subsidiary, fundamental ni mzigo unaobebwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie, Mheshimiwa Waziri, kwa heshima kabisa nitakuomba unapokuja kufanya wind up hapa uniambie daraja la Nhobola ambalo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu ni namna gani linajengwa. Halmashauri ya Mji wa Nzega na TAMISEMI haziwezi kujenga daraja la Nhobola.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tunaweka fedha kwenye Rural Road Agency inayotaka kuanzishwa. Mimi ningeshauri tulitazame sana, TANROADS imekuwa good performer. Kurundika shughuli kwenye TAMISEMI wote tunalalamika, TAMISEMI Elimu malalamiko, TAMISEMI Afya tunalalamika, kila kitu TAMISEMI, ni afadhali tuangalie namna gani Rural Road Agency ni unit ndani ya TANROADS. Kwa sababu safari hii mmeiwekea bilioni 80 hamna kitu haiwezi, lakini TANROADS ina sheria ina vyanzo vyake vya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Rural Road Agency haina vyanzo vya mapato inapewa kwa hisani, haiwezi kuwa sustainable unless mtuletee sheria hapa. Lakini mimi nadhani kwa technical no how kwa infrastructure iliyopo ni vizuri tukaangalia hii wakala wa ujenzi wa barabara vijijini ikiwa ni sub unit ndani ya TANROADS ambayo inatengewa fedha kwenye bajeti ya TANROADS na TANROADS waisimamie. Kwa sababu TANROADS wana watu, tayari wana ofisi kwenye mikoa na wana kila kitu. Tukianzisha hii agency tutaanza kujenga miundombinu mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru, naunga mkono hoja.