Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kupata fursa ya kuweza kuchangi kwenye Wizara hii ya Miundombinu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kununua ndege sita. Ni jambo lisilo la kawaida kwa nchi kama ya kwetu ambayo tumekuwa hatuna ndege na akaamua kununua ndege sita, kwa hiyo na mpongeza sana kwa uamuzi wake huo, ambo ni mzuri sana ambao utatusababishia Watanzania tuweze kuwa na ndege za kutosha na hatimaye kuweza kuboresha uchumi wetu wa Tanzania kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa hotoba yake nzuri ambayo inaleta matumaini katika kuboresha miundombinu. Nimpongezi Naibu wake Waziri, niwapongeze pia watendaji wa Wizara hii ya Miundombinu kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa kuhakikisha kwamba miundombinu kwa maana ya barabara, reli na bandari na pia mawasiliano yana boreshwa kwa ajili ya kuimarisha na kuchochea uchumi wetu wa Tanzania; niwapongeze sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwa pongeze wajumbe wa kamati ya miundombinu kwa kutuletea taarifa nzuri na kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kushirikiana na Wizara katika kuandaa mipango na kuishauri vizuri Wizara ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hii, niwapongeze sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwa sababu katika taarifa yao wameeleza vizuri sana kwamba kuna baadhi ya mikoa ambayo bado haijaunganishwa na mikoa ile ya Njombe na Morogoro, mikoa ya Mbeya na Njombe, mikoa ya Katavi na Kigoma, mikoa ya Kigoma na Kagera, lindi na Ruvuma na mikoa mingine. Ukiangalia hii mikoa ambayo wameitaja ambayo haijaunganishwa ni mikoa ya uzalishaji. Ni mikoa ambayo tunaitegemea sana hasa katika kuzalisha mazao ya chakula lakini pia kuzalisha mazao ya biashara. Pia ni mikoa ambayo ina mvua nyingi sana, maana kwa kuwa ni mikoa yenye mvua nyingi lakini pia ndiyo mikoa inayozalisha chakula kwa hiyo barabara zake sio nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe katika mipango na nimeona mmeeleza na mmeiandaa vizuri sana; katika mikoa hii mmeanza kutekeleza kuhakisha kwamba inapata barabara nzuri, moja wapo ikiwa ni barabara ile ya Lupembe, barabara ambayo inasaidia sana katika kuhakikisha kwamba mazao ya biashara na mazao ya chakula kama nilivyosema yanasafirishwa. Kwa hiyo, niwashukuru kwa hilo, kwa kuhakikisha kuwa barabara yetu pia ya Lupembe inaendelea kuwekwa katika Bajeti na kuongezewa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mwaka wa jana tuliingiza kwenye bajeti tulitengea fedha na mwaka huu pia imetengewa fedha. Sasa naomba kujua, pengine Mheshimiwa Waziri utakaposimama utatueleza vizuri, je, zile fedha ambazo zilitengwa kwenye Bunge la Bajeti mwaka jana ambapo unaishia mwaka huu, na hizi fedha ambazo zimetengwa mwaka huu je, zitajumlishwa pamoja au zile za mwaka huu ambao unaisha zimeshapitwa na wakati au hazitatumika au hazitajumuishwa na tutegemee kupata tu fedha hizi za mwaka huu?
Kwa hiyo, nitaomba utakapo kuja kufanya majumuisho basi nipewe ufafanuzi wa juu ya zile fedha ambazo tulikuwa tumetenga mwaka jana na hizi fedha shilingi bilioni mbili ambazo zimetengwa mwaka huu kama zitakuwa zitajumuishwa kwa pamoja na barabara ile ianze kufanyiwa utengenezaji au ujenzi wa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kupongeza, kama tulivyosema nimeangalia kwenye taarifa pia mmeweza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara nyingine, ile barabara ya kutoka Ilunda mpaka kuelekea Igongolo, ni barabara ambayo ni ya muhimu sana katika uzalishaji wa mazao, kwa maana ya uzalishaji wa wananchi wa maeneo yale. Kwa hiyo nipongeze sana kwa fedha zile ambazo zimetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe badala ya kuendelea kutenga fedha kwa kiwango cha kokoto ni vizuri tuanze kujielekeza kutenga fedha kidogo kidogo kuanza kutengeneza kidogo kidogo lami na hatimaye barabara nzima zitakuwa zimekamilika au tuanze kutengeneza zile sehemu ambazo tunafikiri kwamba ni korofi, sehemu ambazo wakati wa kifuku wananchi/wakulima wetu wadogo wadogo hawawezi kupitisha mazao yao yakafikia kwenye masoko basi angalau zianze kujengwa maeneo hayo kwa kiwango cha lami na hatimaye tutaweza kumaliza barabara nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisubiri tu fedha itakuwa ni ngumu lakini tukianza na hizo fedha ndogo ambazo tunatengenezea vifusi vya kokoto, tukaanza kutengeneza kiwango cha lami kwenye maeneo yale ambayo ni korofi na hatimaye barabara zote zitatengenezwa kirahisi zaidi na zitaweza kupitika wakati wote hata wakati ule wa mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia kwenye upande wa mawasiliano. Imeelezwa hapa kwamba maeneo mengi ya vijijini bado mawasiliano ni shida, bado hayafikiki mawasiliano na maeneo haya ya vijijini ndiyo maeneo ambayo tunayategemea, kama tulivyosema, kwenye uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula; kwa kuwa maeneo haya hayana mitandao ya simu au hayajajengwa minara ya simu. Kwa mfano katika Jimbo langu la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, kuna kata tano hazina mawasiliano. Kuna kata za Ikondo, Ninga, Mfiliga, Idamba na Ukalawa hazina mawasiliano, kwa hiyo vijiji vyote vya maeneo hayo simu hazipatikani kwa urahisi zaidi. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri maeneo hayo tuweze kujengewa minara ili wananchi wale waweze kupata mawasiliano kirahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nichangie juu ya suala mtambuka. Niwapongeze Wizara kwa uamuzi wa kuanzisha mafunzo maalum kwa wakandarasi wa kike, mafunzo hasa yanayohusika na ukarabati na matengenezo
ya barabara na uandaaji wa zabuni. Hii itasaidia akina Mama wengi kujiunga na ukandarasi au kusoma masomo ya ukandarasi, masomo ya sayansi, lakini pia itawasaidia wanafunzi wetu wa shule za sekondari kuanza kupenda masomo ya sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa hivi wanafikiri kwamba ukandarasi au uhandisi au u-engineer ni kwa ajili ya wanaume tu. Kwa hiyo tukiwawesha hawa na wanapoenda huko kwenye maeneo haya ya ujenzi wa barabara wakiwaona basi watahamasika kusoma masomo ya sayansi na kuhakikisha kwamba wanafaulu vizuri, na tutakuwa na wanawake wengi ambao wanakuwa ni Ma- engineer na hatimaye kuwa na ma-engineer wa kutosha kuliko ilivyo sasa hivi, ma-engineer wengi ni wa kiume kuliko ma-engineer wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nichangie juu ya ajira hasa ajira za vibarua, wale ambao they are not trained kwenye maeneo huko ambako shughuli za ujenzi wa barabara zinaendelea. Niombe tuweke utaratibu wa kuwaangalia wale watu wanaowekwa kwenye maeneo ambako miradi hii inatengenezwa. Tukifanya hivi itasaidia kuwapa ajira vijana wa maeneo husika ambako barabara zinajengwa, lakini pia itawafanya hawa vijana wasiharibu miundombinu ya barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine vijana au watu wa maeneo yale wanaharibu kwa sababu wanaona kama ile barabara kwao hawajanufaika, wanapoona wajenzi wa barabara au wanaoshiriki kutoa labour force ya zile ambazo hazihitaji wasomi wanatumika watu wa kutoka maeneo ya mbali. Na kuna maeneo mengine wamekuwa wakiiba vifaa vya ujenzi au waki- vandalize vifaa vya ujenzi kwa sababu tu wao hawajashirikishwa katika ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukiwatumia vijana wa maeneo husika, maeneo ambako mradi unafanyika itawasaidia vijana wenyewe kuanza kupenda shughuli zile na kuhakikisha kwamba wanakuwa walinzi wa vifaa na mali zilizoko katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.