Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii, ya kuongea katika Bunge lako Tukufu. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuongea sasa hivi katika Bunge lako.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya mambo mengi, mengi kweli. Katika kazi zake muda wake wote huu, ameweza kujenga barabara za lami mahali pote na kwenye majimbo yetu yote na hakuna mtu yeyote anayeuliza mwongozo, hayupo kwenye majimbo yote. Mheshimiwa Rais ameweza kuweka jiwe la msingi la reli na hiyo reli watu wote wataipanda, hakuna mtu atakayeuliza taarifa. Mheshimiwa Rais ameweza kununua ndege ambazo kila mmoja anazipanda, hakuna mtu anayesema mwongozo au taarifa. Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imefanya mambo mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo mambo mazuri yanafanyika ni afadhali upongeze kuliko kubeza kila kitu. Huko Dar es Salam kuna mabasi ya mwendo kasi, kila mmoja anaingia hakuna mtu anayeuliza mwongozo au taarifa au swali la nyongeza, hakuna, kila mmoja anaingia. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu ni kweli anafanya kazi nzuri, ameibadilisha Tanzania kwa muda mfupi, barabara hizi tulikuwa tunaziona Ulaya, flyover zinajengwa aaah, tTunamuombea maisha marefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuongelea daraja la mto Kilombero. Wananchi wa Morogoro tunapongeza sana, tuliteseka sana kwa kusafiri kwa kivuko kwenye mto wa Kilombero, kiasi kwamba wengine walipata matatizo. Imekuwa ukombozi kwetu sisi kuona daraja limekamilika. Daraja hili ni kiungo cha Wilaya za Kilombero, Ulanga na Wilaya ya Malinyi. Enzi za kivuko kilikuwa kinafanya kazi kwa saa 12 tu. Kwa hiyo, ukiwa na mgonjwa baada ya saa 12 na ikishindikana kutibiwa kwenye hospitali za Malinyi na Ulanga huyo mgonjwa wako anaweza akafa. Sasa hivi kwa kupata daraja hili mgonjwa anasafirishwa na anakwenda Kilombero kwenye Hospitali ya St. Francis ambayo ndio hospitali kubwa na hasa akina mama wajawazito, na kwa kuwa akina mama wengi wanajifungua usiku, kwa hiyo kuwepo daraja letu la Mto Kilombero kwa kweli ni fahari na imerahisisha usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naongeza tena hapo hapo, wakulima wengi kwa pande zote mbili, upande wa Kilombero/Ifakara na upande wa Ulanga/Minepa na Lupilo; wa Ifakara wanalima mpunga Lupilo na Minepa. Sasa wanawake ndio wanaolima, unaju asilimia 70 ya wanawake ndio wanalima chakula hasa. Kwa hiyo ni ukombozi wa usafirishaji wa vyakula na kwa mwanamke hasa wa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine. Kwa sababu Ulanga kuna madini hata watu wengine watatumia daraja hilo la Mto wa Kilombero.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba niongelee reli ya kati, ambapo kilometa 200 tayari Mheshimiwa Rais ameshaweka jiwe la msingi na mkataba umeshasainiwa. Na hiyo reli inaanzia Dar es Saalam kuja Morogoro, wana Morogoro tusime nini? Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu huu ni usafiri mbadala wa barabara, saa moja tu kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro. Naona hata magari yetu tutayaacha tutaanza kusafiri kwa reli. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mkoa wetu wa Morogoro ni wakulima, wakulima wa mboga, wakulima wa matunda, wa nafaka na kweli watafaidika kwa kusafirisha mazao yao kwa kutumia hii reli. Wananchi wa Morogoro tunampenda sana na tunaishukuru Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais kwa kujenga reli ambayo itatumiwa na watu wote bila kuuliza swali la nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongelea kuhusu barabara za mkoa wa Morogoro, napenda sana kuongelea barabara ya Dumila mpaka Kilosa. Barabara ya Dumila mpaka Kilosa kilometa 63, kuna sehemu imejengwa kwa kiwango cha lami kutoka Dumila mpaka Ludewa. Kwa kweli barabara hii ilikuwa mbaya sana, sasa hivi unaweza ukatembea usiku na gari lako dogo (saloon) ukafika mpaka Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipande cha barabara cha kuanzia Ludewa mpaka Kilosa Mheshimiwa Waziri ambaye na mpongeza na Makatibu wake na Mheshimiwa Naibu Waziri mnafanya kazi nzuri; mmesema kuwa mkandarasi tayali anatafutwa kwa hiyo naomba hiki kipande cha barabara cha kuanzia Ludewa mpaka Kilosa kiweze kujengwa kwa muda muafaka. Kitu ambacho sikuona kwa muendelezo wa barabara hii ya Dumila mpaka Mikumi ni kuanzia Kilosa mpaka Mikumi wananchi wa jimbo la Mikumi wanauliza tutafanyaje mpaka na sisi tuweze kuendana na barabara hii kwa sababu ni wakulima wazuri.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nakishukuru sana Chama cha Mapinduzi na nasema naunga hoja asilimia mia moja, ahsante.