Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo na mimi pia niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, kwa kuwa nina mambo mengi ya kusema, naomba nitamke kabisa kwamba naunga mkono kwa asilimia mia kwa mia bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza sana sana Mheshimiwa Rais wetu. Mheshimiwa Rais amethubutu na ameweza kufanya mambo makubwa na mazito katika sekta ya barabara, anga, reli na bandari. Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi sana kwenye sekta hiyo na ameendelea kufanya mambo mengi katika maeneo mbalimbali na katika Jimbo langu la Mvomero kulikuwa na barabara ya lami ambayo ilikuwa imesimama kwa miaka mitano.
Mheshimia Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipokuja mwaka 2015 kuomba kura kama mgombea, alitamka iwapo atachaguliwa kuwa Rais, barabara ile itawekwa lami. Na kweli ujenzi umeanza mwaka 2016 lami ile imeshakamilika kwa kilometa 40 bado kilometa nane zimebaki, tuna mategemeo mwezi wa nane wa tisa itakuwa imekamilika. Kwa mazuri yote haya anayofanya Mheshimiwa Rais ndani ya nchi yetu na ndani ya Wilaya ya Mvomero, Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako naomba nimpigie salute Mheshimiwa Rais. Nampigia salute ya heshima, nampigia salute ya upendo, Mwenyezi Mungu ampe imani zaidi, ampe afya njema aendelee kuliongoza Taifa letu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Engineer Mfugale, Engineer wa TANROADS Mkoa Morogoro Mama yetu Engineer Mtenga, kwa kazi kubwa wanayofanya katika kusimamia masuala yote ya barabara katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na reli. Serikali yetu sasa hivi ina mpango wa kujenga reli na mpango ule umeanza na reli ile itakuwa reli ya kisasa, reli ya kasi ambayo tayari imezinduliwa kwa awamu ya Morogoro - Dar es Salaam - Morogoro. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, niwaombe na wataalam, reli ile inapoanza kazi kuja Morogoro na kwenda mikoa mingine, kwa kuwa itakuwa ni reli ya kasi, abiria wengi watapanda, ile miundombinu iliopo leo katika miji ya Morogoro na miji mingine haitoshelezi mahitaji ya kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wewe na wataalamu wako, jaribuni kubuni mkakati wa kuweka miundombinu mingine, tuseme mfano reli imepakia abiria 1000, abiria 1000 wanaoshuka katika reli ile katika kituo cha leo cha Morogoro kutakuwa na msongamano mkubwa, magari yatakuwa mengi kuwapeleka wale vituo vya mabasi na maeneo mengine. Jaribuni kujenga vituo vipya vitakavyokidhi mahitaji ya reli ya kisasa. Huo ni ushauri wangu kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwenye barabara ya lami inayojengwa kutoka Magole - Turiani - Mziha
- Handeni. Barabara hii lengo lake kubwa ni kufungua milango ya uchumi kutoka Tanga - Mombasa - Arusha - Kilimanjaro na maeneo mengine. Na kwa lugha njema barabara hii ndiyo barabara mbadala kwa barabara ya Chalinze - Segera. Lolote litakalokea kwenye Daraja la Wami, ujue barabara mbadala ni barabara hii ya Turiani - Mziha - Handeni. Kipande cha Magole - Turiani kinakaribia kukamilika, kipande cha kutoka Turiani - Mziha – Handeni, Mheshimiwa Waziri nikuombe mkandarasi yuko site, ana mitambo ya kisasa, ana uwezo mkubwa, na wewe kutambua uwezo wake na wataalam wako mkandarasi yule umempa kujenga interchange ile ya Ubungo. Mkandarasi huyu ndio anajenga pale Ubungo ambae leo anajenga lami Turiani, kwa sababu ana uwezo ana vifaa ana mtaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri, Engineer Mfugale na wengine wote wa TANROADS, kazi yake mmeiona, hebu muachieni amalize kile kipande kilichobaki, Serikali itaokoa mamilioni ya fedha. Hakuna mobilization, hakuna chochote zaidi ya yule kupewa kazi na kuendelea na barabara. Na barabara ile ndiyo itakuwa barabara mbadala kwa baadaye. Lakini leo Tanga tunajenga bomba la mafuta toka Uganda kuja Tanga, wenzetu wa Uganda watasafirisha mafuta yao kupitia kwenye meli. Tanzania tukinunua mafuta yale tutayasafirisha aidha kwa reli au kwa barabara. Barabara ya Segera - Chalinze ina msongamano. Mheshimiwa Waziri elekeza nguvu Handeni - Mziha - Turiani kupitia Dumila. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo naomba niseme suala la barabara za Halmashauri za Wilaya ya Mvomero ambazo tumeziomba zipandishwe daraja na ninaomba niseme kwamba taarifa nilizonazo kila Mkoa kuna barabara zimepandishwa daraja. Barabara iliyopandishwa daraja ya Mvomero kutoka Langali - Nyandila kwenda Kikeo, naomba sasa barabara ile itengewe fedha mwaka huu. Tusisubiri kwa sababu imepanda daraja mwaka huu isubiri bajeti ya mwakani. Na kila mkoa wamepata barabara, kila mkoa kuna barabara zimepanda daraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mikoa yote na Wilaya zote fedha zianze mwaka huu. Kwa sababu tunakiu ya barabara hizi zipande daraja naomba fedha hizi sasa zitolewe mwaka huu na barabara zile zianze kazi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, Meneja wa TANROADS Morogoro aliandika barua kwa Wizara yako kukumbushia ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipofanya ziara Mvomero katika tTarafa ya Mgeta, kwamba barabara ya kutoka Chuo Kikuu Mzumbe kwenda Mgeta itawekwa lami. Mheshimiwa Waziri, nakuomba wewe na timu yako tukumbukane katika ahadi ile ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende kwenye mawasiliano. Mheshimiwa Waziri wewe ni shahidi, nimekuja kwako mara nyingi, Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi tumezungumzia minara kwa ajili ya Mvomero. Halotel wamefanya kazi nzuri, wamejenga minara katika baadhi ya maeneo, lakini maeneo yafuatayo bado tuna upungufu wa minara. Maeneo ya kata za Pemba, Kinda, Mascut, Homboza pamoja na kata ya Kikeo pale Mgeta.
Mheshimiwa Waziri nakuomba sana waelekeze wenzetu wa Halotel na mitandao mingine waweze kutukamilishia ahadi ya mitandao hii ili wananchi waweze kufanya biashara zao, waweze kupata huduma mbalimbali kupitia simu za mkononi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Nimeona kuna bajeti imetengwa kwa ajili ya barabara ya Msamvu – Bigwa. Unapozungumza Msamvu – Bigwa unazungumzia Manispaa ya Morogoro, unazungumzia barabara ya Morogoro Mjini. barabara ya Morogoro Mjini sasa hivi ina msongamano mkubwa wa magari.
Nawaomba sana wenzetu wataalamu, barabara ile wachore ramani ya two way, kwa sababu ya reli inayokuja na kituo kile kilichopo barabara ile ina msongamano mkubwa. Fedha zilizotengwa wataalamu waelekeze kutoka Msamvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.