Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, mimi na sisi sote tuliopo hapa ili tuweze kuwawakilisha wananchi wetu kama ambavyo Katiba inataka tufanye.
Pili, naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuitikia maombi ya Watanzania. Mwaka 2014/2015 Watanzania tulikuwa tunaomba katika imani zetu mbalimbali. Tuliomba kwamba tupate Rais mwenye maamuzi, tuliomba kwamba tupate Rais mwenye vitendo, tuliomba kwamba tupate Rais mwadilifu na tuliomba kwamba tupate Rais ambaye kweli atakuwa ni mtetezi wa wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nimeshiriki katika maombi kwa nyakati tofauti na ushahidi kina mama Jenista Mhagama, tumeshiriki nao tukimuomba Mwenyezi Mungu kwamba atupatie Rais ambaye atakuwa ni mtetezi wa wanyonge. Kinachotokea nchini kwetu dhahiri inaonyesha kwamba Rais John Pombe Magufuli wa Awamu ya Tano ni mwitikio wa maombi ya Watanzania. Ni Rais aliyetoka kwa Mungu na mimi ninaamini mtu yeyote akijaribu kumbeza atakuwa anabeza maamuzi ya Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa kujiamini na kwa uwazi kabisa na kwa dhati ya moyo wangu, kwa sababu yapo mambo mengi ambayo yamekuwa ni hadithi ya miaka mingi leo tunayaona yakitokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka miaka yote tulikuwa tukizungumzia kwa mfano sekta ya utalii ambayo mimi nimewahi kuhudumu, kwamba ili uweze kukuza uchumi wa nchi ni lazima uangalie miundombinu na hasa usafiri wa anga. Na ili kukuza utalii tukasema tunahitaji sana Shirika la Ndege la Tanzania liweze kufufuliwa. Kufufua kwa Shirika la Ndege la Tanzania kunamaanisha kwanza, tunatangaza nchi yetu, lakini pili, tunaongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi yetu, na jambo la tatu na muhimu zaidi, ili kunufaika na idadi ya wageni unaowapata ni lazima uangalie wageni hao wanatumia fedha zao kwenye maeneo yapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tafiti zilizofanyika, asilimia zaidi ya 65 ya fedha anazotumia mtalii anayetoka nje anatumia kwenye usafiri hasa usafiri wa anga, usafiri wa nje na usafiri wa ndani na asilimia karibia 25 anaitumia kwa ajili ya accommodation. Kwa hiyo, ili Taifa liweze kunufaika na idadi kubwa ya watalii inaopata ni lazima tuboreshe na tufufue Shirika letu la Ndege. Kimekuwa kilio cha Watanzania, leo ATCL imefufuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashangaa kumsikia Mtanzania ambaye anajua maana ya kukuza uchumi, akibeza maamuzi hayo. Tumezungumzia sana kuhusu mawasiliano hasa ya reli, mimi wananchi wangu pale Isaka ilifika mahali wakawa wamekata tamaa, hotuba zote nilizokuwa ninawaeleza walikuwa wanaona kama ninawadanganya. Leo wameshuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge. Ni mambo ya kihistoria ambayo yalikuwa hayajawahi kutokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuitikia maombi yetu Watanzania kutuletea Rais ambaye alihitajika sana kwa wakati huu tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme jambo lingine moja, hata nidhamu Serikalini sasa ipo na hata hapa Bungeni niliwahi kufika wakati fulani kule nyuma kipindi cha Bunge kama hiki, watu ambao walikuwa hawana nia njema na nchi hii walikuwa wanajaa kwenye mahoteli, wanakutana na Wabunge kuweka mashinikizo ili Serikali iweze kufanya mambo ambayo wanayataka. Ilifika mahali Serikali ikawa inaundwa kutoka nje ya matakwa ya Serikali yenyewe. Linawekwa shinikizo mtu fulani afanyiwe hivi kwa sababu tu wameathirika na maamuzi yaliyofanywa na viongozi wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo uhuni huo haupo, Serikali ipo stable na Mawaziri wanafanya kazi kwa kujiamini. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa na msimamo na kutumia vyombo vilivyowekwa Kikatiba katika kumpa ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa. Kwenye hotuba yake ya mwaka uliopita nilisema kwamba kwa kiasi kikubwa hakunifurahisha, lakini alinieleza kwamba Mheshimiwa Mbunge barabara yako ya kwenda Kahama kwenda Geita hatujaiwekea fedha wakati huu kwa sababu tuna madeni ya wakandarasi wa miradi inayoendelea. Ninakuhakikishia awamu ijayo ambayo ni bajeti hii barabara hiyo itakuwemo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia Hotuba ya Mheshimwia Waziri na nimemsikiliza. Ukiangalia aya ya 257 ya hotuba yake bila kupepesa macho amesema barabara ya Kahama kwenda Geita itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Naompongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa maamuzi hayo, ni Waziri muungwana alichokisema ametenda, ninajua wapo wengine kwa namna moja ama nyingine wanaweza matarajio hayajafikiwa kwa wakati huu. Lakini niwaombe mbona mimi mwaka uliopita niliambiwa nitulie nikatulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe sote kwa pamoja bajeti hii ni nzuri sana na niwaome katika upigaji kura wote tuunge mkono bajeti hii kwa sababu matarajio ya wananchi na maombi ya kwetu yamekuwemo. Naomba kwa kumalizia, kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameonyesha usikivu, nimpongeze sana pia Katibu Mkuu Engeneer Nyamuhanga kwa sababu haya yamefanyika kwa ushauri ambao akimpa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuweka maombi ya nyongeza ambayo ninaamini kwa ushahidi huu tulionao sasa yatatekelezwa. Kuna barabara ambayo ilikwisha kuwekwa kwenye Ilani kwa ajili ya kuanza kujenga ujenzi wa kiwango cha lami, barabara ya kutoka Kahama - Bulige - Mwakitolyo - Salawe hadi Mwanza. Kwenye kitabu hiki inaonyesha kuwa itafanyiwa up grading pamoja na rehabilitation ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sasa angalau kwenye bajeti ijayo, kama tulivyofanya mwaka huu, najua kwamba angalau feasibility study haitaweza kufanyika mwaka huu basi mwaka ujao iweze kufanyika feasibility study. Lakini pia kuna barabara nyingine inayotoka Kahama inaunganisha na Karume makao makuu ya Nyang’hwale kwenda hadi Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa upande wa Sengerema na Geita, wamekwisha kuanza kuifanyia maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Kipande cha kutoka Kharumwa makao makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale kuja hadi Kahama hakiko kwenye mpango wowote wa Serikali kwa ajili ya kuweka kiwango cha lami. Nimuombe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla angalau hii barabara na yenyewe ili ikamilike kama ambavyo ipo designed iwe kwa kiwango cha lami kutoka junction ya Nyambula kupita Busangi kupita Nyang’holongo kwenda mpaka Kharumwa hadi Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema; Mheshimiwa Waziri alipomaliza hotuba yake mimi nilisimama. Pamoja kwamba mimi ni Mbunge wa kawaida lakini niliunga mkono hotuba tu kabla ya kufika kwenye hoja yenyewe. Naomba nikuhakikishie nakuunga mkono Mheshimiwa Waziri, naunga mkono bajeti hii kwa asilimia 100 na ninaomba nikuhakikishie nitafanya kampeni ili bajeti hii ipite kwa sababu maombi yangu na maombi ya Waheshimiwa Wabunge tulio wengi umeyazingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi naomba niseme naunga mkono hoja, ahsante sana.