Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara ambayo iko mbele yetu sasa hivi. Kabla sijaenda mbali sana nilitaka niongee mambo mawili kimsingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kabisa ni kuishauri Wizara ya Miundombinu kwamba waangalie ni namna gani wanaweza wakawashauri wahusika wa bandari, kwa sababu ninafahamu Kisheria, watu wa bandarini wanaruhusiwa kuuza mali mbalimbali zilizoko bandarini ambazo wahusika wameshindwa kulipia ushuru ikiwemo pamoja na magari na vitu vingine. Bahati mbaya kabisa kuna wananchi Watanznaia zaidi ya 2,000 ambao wamenunua magari kwa njia za mnada bandarini lakini bado wanalazimishwa kulipa port charges pamoja na other charges za bandari. Sasa Watanzania wanatamani kutaka kufahamu kwamba kimsingi unaponunua chombo chochote kama gari bandarini kupitia kwenye mnada unalazimika kulipia tena na other charges? Kwa nini wanaruhusu kufanya mnada kama bado mtu haambiwi hali halisi au gharama halisi za ununuzi wa vyombo vile ambavyo wananchi wameshindwa kuvilipia bandarini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nililotaka nichangie ni kuhusiana na suala la barabara. Sisi wakazi wa Mtwara kwa kipindi kirefu kama wengi mnavyofahamu katika hata Mabunge yaliyopita walitokea wazee wetu ambao walikuwa Wabunge wa Mtwara, walikuwa wanatamani upande wa Mtwara uunganishwe na upande wa Mozambique kwa sababu ya shida kubwa ya barabara ambazo tulikuwa tunazipata. Miaka ya karibuni Serikali imeamua kujenga barabara na ndiyo sasa hivi tunaweza kufika Mtwara kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado tuna tatizo moja kubwa sana. Tunapoongelea suala la uchumi wa Mtwara tunaongelea kuhusu ring roads za barabara zetu ambazo zinaunganisha mkoa wa Mtwara pamoja na Lindi. Ukienda kwenye Kitabu cha Mheshimiwa Waziri, taarifa aliyotoa hapa ukurasa wa 165, utakuta hapa anaongea kuhusu barabara ya Masasi – Songea – Mbamba Bay. Sina uhakika kama yamefanyika makosa kwenye ku-record lakini pesa inayoonekana imetengwa hapa wanaongea habari za shilingi 64,514,000.144. Sasa labda kama ni bilioni basi mje kutuambia; lakini hata kama mtasema ni bilioni, hizo barabara tunazoziongelea kwa kutumia hiyo bilioni 64, tunaanza kuongea kuanzia barabara ya Masasi - Songea kuelekea Mbamba Bay. Lakini pia barabara hii inajumuisha pamoja na kulipa gharama mbalimbali za wakandarasi waliofanya kazi kwenye barabara ya Masasi kuelekea Songea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kilometa 70 za Mangaka – Nakapanya ziko ndani ya hii shilingi bilioni 64 kama si milioni. Kuna kilometa nyingine 66 ziko ndani ya hii shilingi bilioni 64, kuna kilometa nyingine 65 Mangaka – Mtambaswala ziko ndani ya hizo hizo pesa; kuna kilometa zingine 59 Tunduru na Matemanga zinaongea kuhusu hizo shilingi bilioni 64. Kuna kilometa 60 za Kilimasera – Matemanga. Mwisho kabisa wanasema, barabara za Masasi
– Newala (Mtwara), sehemu ya Mtwara – Navira kilometa 50 na kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbamba Bay kilometa 66, Masasi – Nachingwea – Nanganga kilometa 91.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko kabisa ninataka kusema bado tunarudi na lile lile wazo letu la zamani kwamba kama Serikali haina mapenzi mema na watu wa Kusini mtupe hii taarifa tuamue kujitenga wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ngombale ametoka kuchangia hapa karibuni, mmesikia kuhusu matatizo makubwa ya barabara inayoanzia Nangurukuru kuelekea Liwale. Watu hawa hawa wa Liwale wanatumia masaa sita kutokea Nachingwea mjini kuelekea Liwale kipindi hiki ambacho hakuna mvua, lakini wakati wa mvua wanakwenda kwa masaa tisa mpaka 12 umbali wa kilometa 95 Nachingwea – Liwale. Sijui katika hii mika zaidi ya 50 ya uhuru mnataka kutuambia nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule ndani unakuja kukuta bado kuna shida. Sasa hivi Serikali imeamua kuhamisha makao makuu ya nchi kuja kuyaweka Dodoma. Sisi wakazi wa Mikoa ya Kusini; Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma ili tuweze kufika Dodoma tunalazimika kupita tena Dar es Salaam. Tulikuwa tunakwenda Dar es Salaam kwa sababu ndiko ambako yalikuwa yanajulikana kama makao ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake alichokitoa hapa leo, sijaona kama Serikali ina mpango wowote wa kutaka kuunganisha mikoa ya Kusini kupitia Masasi, Nachingwea, Liwale hadi Morogoro kwa sababu ndiyo njia fupi sana ya kutuwezesha sisi kuweza kufika Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Waziri ni mtu anayetokea Jimbo la Namtumbo ambalo ni karibu tu na haya maeneo niliyoyataja, lakini yeye akiwa bado Wizarani hajaona kama kuna namna au kuna haja kweli ya ndugu zake wa Namtumbo kuhakikisha anawapitisha njia fupi ya kufika Dodoma pamoja na Wabunge wote na watu wote wanaotakiwa kufika Dodoma kwa wakati. (Makofi)
Kwa hiyo, niiombe Serikali ifikirie sasa ione namna ya kuunganisha Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Ruvuma kutokea Masasi, Nachingwea kupitia Liwale mpaka kufika Mahenge – Morogoro na kutoka Mahenge kuja Ifakara na maeneo mengine ni njia fupi sana ya kuweza kutufikisha Dodoma badala ya kung’ang’ana na ile njia ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nakuja suala la reli. Mheshimiwa Naibu Spika kwa taarifa yako labda kama umesoma vizuri historia ya Tanzania, na nataka niwakumbushe pia na Waheshimiwa Mawaziri, mwaka 1949 ilizinduliwa reli ya kwanza ya Kusini, ilikuwa inatokea Mtwara inapita Mkwaya, Mnazi mmoja na vijiji vingi, Lukuledi kuelekea Nachingwea. Siku moja Mheshimiwa Nape hapa aliuliza na Serikali miaka miwili, mitatu iliyopita ilisema wana mpango wa kufufua reli ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa kuna crisis, kuna watu wengi ambao walikuwa wanatamani kuwekeza kwenye reli ya kati ambayo sasa inakwenda kwenye standard gauge. Sasa niwaombe, watu wale ambao wameshindwa kuwekeza kwenye reli ya kati tuwaombe waje kuwekeza kwenye reli hii ya Kusini ambayo inakwenda Mchuchuma, Liganga itapita Tunduru, itakwenda Songea itaweza sasa kuboresha na kuongeza mapato ya Taifa kwa ajili ya bandari ya Mtwara ambayo ni bandari inayozalisha gesi. (Makofi)
Kwa hiyo tuwaombe Serikali jambo hili mlifikirie kwa ajili ya kuongeza uchumi lakini pia kurahisisha usafiri. Barabara zetu hizi ambazo tumezilalia kwa muda mrefu toka wakati wa uhuru mpaka miaka mitatu iliyopita zinakwenda kuharibika kwa kupitisha magari yenye uzito mkubwa tofauti na stahiki zake. Magari yanayobeba makaa kutoka Mchuchuma na maeneo mengine, magari yanayobeba makaa ya mawe ambayo yanatakiwa yalete Bandarini Mtwara. Kwa hiyo, tuiombe Serikali kwa namna ya kipekee watueleze; kama itashindikana basi tutaishia kutoa shilingi; wana mpango gani na reli ya Kusini, hilo tunataka tulifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni suala la ndege. Si maeneo mengi sana yanayotumia ndege katika maeneo yetu lakini wachache wanatamani kutumia ndege. Tumeona sasa Serikali hata kama walifanya nje ya bajeti ya kawaida kabisa lakini wameamua kuzileta ndege. Sasa hivi kwenda Mtwara, one way ticket ni shilingi 631,000 kutoka Precision Air. Ukiwahi kukata mapema utapata hiyo ticket kwa shilingi 410,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya yanatokea maeneo mengi, tumeona Serikali sasa inataka kuleta ndege maeneo yale na wanatangaza kwamba itakuwa ni yenye gharama nafuu; lakini tuwaombe ndege ile isiishie Mtwara Mjini. Watu wa Masasi wanatamani kutumia ndege, watu wa Ndanda wanatamani kutumia ndege ambazo ni kilometa 200, pamoja na watu wa Nachingwea. Maeneo yote haya yana viwanja vya ndege tena vikubwa vya siku nyingi.
Kiwanja cha Nachingwea kilikuwa kinatumika wakati wa vita za ukombozi Kusini mwa Afrika kila mtu anatambua, kiwanja cha Nachingwea pale kuna kambi kubwa ya jeshi ambao wanahitaji ndege kutua pale. Viwanja hivi sasa viboreshwe viweze ku-accommodate kwa ajili ya kutua ndege za Serikali ambazo tunaamini pamoja na kuwa commercial lakini nia yake hasa ni kutoa huduma kwa ajili ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuwaombe, kama hamna mpango, kwa sababu sijaona kwenye vitabu vyenu, wa kuboresha viwanja vya ndege vya Masasi na Nachingwea, watu wale wanaozunguka viwanja vile vya ndege ni bora tukawaeleza ili waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida za uchumi, kufuga pale Mbuzi na vitu vingine kwasababu nyumba zao zilichorwa “X” na lile eneo sasa hivi limekuwa vichaka, linafaa kabisa kuwa malisho ya mifugo. Kama mnapata nafasi Mheshimiwa Waziri nikuombe twende pamoja ukalione hili, kimsingi niunge mkono hoja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CECIL D. MWAMBE: …hoja ya upinzani.