Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara hii. Kwanza kabisa nianze kutoa pongezi zangu kwa kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri Engineer Ngonyani, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa taasisi zote katika Wizara hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, na mimi kwa kweli kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu nianze kupongeza kazi nzuri ambazo zimefanywa na Serikali ya Awamu hii ya Tano kama vile ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ujenzi wa mabweni UDSM, uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kati, uzinduzi wa miradi ya flyovers, TAZARA na Ubungo, Serikali kumiliki asilimia 100 TTCL, mradi wa ujenzi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na ununuzi wa ndege ya ATCL na kubwa kuliko zote, Serikali kuanza kulipa wakandarasi na washauri shilingi bilioni 788 kutoka katika deni la shilingi bilioni 930.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali hili zoezi liwe endelevu ili miradi yetu ikamilike kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia kuhusu ujenzi wa viwanja vya ndege. Naipongeza Serikali kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege kote nchini, ni pamoja na jengo lile la abiria Terminal III Kiwanja cha Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa tulipotembelea tulikuta kuna changamoto ya pesa kutopelekwa kwa wakati, sasa naiomba Serikali ipeleke pesa kwa wakati ili jengo liweze kukamilika na liendane na ununuzi wa ndege zetu. (Makofi)
Niendelee kupongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja chetu cha Nduli. Hiki kiwanja kwa kweli tumekuwa tukikidai kwa muda mrefu, sasa tunaishukuru Serikali angalau imeweza kutenga pesa na sisi kiwanja chetu cha Nduli sasa kitajengwa na najua hata Bombardier sasa itatua pale. Nitoe tu ushauri, kwamba pamoja na kuwa huu mradi tayari wananchi wa pale wameshaukubali sasa waweke alama katika yale maeneo ambayo upanuzi utafanyika ili yale maeneo yasiweze kuendelezwa, kwa sababu yakiendelezwa wakati wa kulipa fidia itakuwa tatizo kubwa sana.
Vilevile niiombe Serikali sasa, kuna viwanja vingi sana havina hati miliki kikiwemo hiki cha Iringa. Kwa hiyo, sasa itengeneze hati ili wananchi wasiendelee kuvamia katika hivi viwanja vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na ujenzi wa barabara nchini. Niipongeze sana Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa miradi ya barabara kwa kiwango cha lami.
Naomba niunge mkono ushauri, Mheshimiwa Serukamba alipokuwa akichangia amesema kwamba angalau zile barabara za Wilaya TANROADS iendelee kuzihudumia, kwa sababu tunaona hata sisi wenyewe tulipokuwa tunachangia watu wengi sana wanalalamikia barabara zilizopo katika vijiji kwamba miradi haiendi kwa wakati na vilevile tumeona kwamba hakuna wataalam wengi kwenye Halmashauri zetu. Kwa hiyo, kama barabara hizi zitamilikiwa na TANROADS tuna imani kabisa zitakwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia labda uwepo upembuzi yakinifu katika miradi ya barabara zetu, kwamba zile za kiuchumi ziweze kupewa kipaumbele, kwa sababu tumekuwa na barabara nyingi za kiuchumi katika halmashauri zetu ambazo zinakuwa hazijengwi kwa kiwango cha lami kiasi kwamba sasa wakati wa mvua malori yanakwama. Kwa mfano pale Iringa tuna miti, kama Mgololo kule unaona wakati wa mvua malori yanakwama na kuna ajali nyingi sana zinatokea.heshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile ubovu huu wa barabara hasa vijijini unasababisha hata vifo vya akina mama na watoto. Kwa sababu ya miundombinu ambayo ipo katika barabara zetu zilizopo vijijini wakati wa mvua akina mama wengi hawafikiwi. Kwa hiyo, mimi niombe hizi barabara zipewe kipaumbele ili kupunguza pia vifo vya akina mama na watoto katika vijiji vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie pia barabara zilizopo katika Mkoa wetu wa Iringa. Tunashukuru sana Serikali katika bajeti hii imeweza kutenga pesa kuanza ujenzi wa barabara inayokwenda katika mbuga ya Ruaha. Muda mrefu sana tumekuwa tukiizungumzia barabara hii kwa sababu utalii utaongezeka katika mkoa wetu na mikoa iliyopo katika Nyanda za Juu Kusini. Kwa hiyo, mimi nishukuru kwamba japo kuwa wametenga pesa, lakini sasa ujenzi ufanyike kwa sababu kutenga pesa ni kitu kingine na kuanza ujenzi ni kitu kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara za kiuchumi kama barabara ya Mafinga – Mgololo, Kinyanambo
– Isalavanu – Saadani – Rujewa, kuna Kiponzelo – Wasa, kuna barabara ile ya Kilolo mpaka Iringa Mjini. Tunaomba Serikali yetu izipe kupaumbele kwa sababu uchumi wa mkoa wetu unazitegemea sana hizi barabara ambazo ziko katika wilaya hizo nilizozitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie watu wenye ulemavu. Sisi wote hapa ndani ni walemavu watarajiwa. Nilipoongea na watu wenye ulemavu katika Mkoa wangu wa Iringa yapo mambo ambayo wanalalamikia hasa miundombinu katika magari. Inaonekana kwamba watu wengi wenye ulemavu bado Serikali haijawaangalia. Watu wanakuwa na baiskeli lakini hawawezi kupandisha kwenye gari kwa sababu hakuna miundombinu inayoruhusu mtu mwenye ulemavu kuweka baiskeli yake kwenye gari lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile majengo yetu bado si rafiki sana na watu wenye ulemavu kiasi kwamba yanasababisha hawa watu wenye ulemavu kukosa hata huduma nyingine. Utakuta mama mwenye ulemavu ni mjamzito anashindwa kupandisha ngazi kwenda kumuona daktari. Kwa hiyo, mimi ningeomba sheria iwepo ili watu wenye ulemavu pia wazingatiwe wakati wanajenga haya majengo yote yakiwepo hata majengo ya shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile TCRA labda iangalie, pia hata katika televisheni zetu bado hawajaweka watu kutafsiriwa zile lugha za watu wenye ulemavu. Kwa hiyo mambo yote hayo yazingatiwe. Hakuna pia michoro kwenye barabara kuonesha watu wenye ulemavu wanapopita, kwa hiyo mimi naomba haya mambo yazingatiwe kwa sababu sisi wote ni walemavu watarajiwa, huwezi kujua wewe lini utakuwa mlemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia kuhusu Shirika la Posta Tanzania. Kwa sababu Serikali imeanza kuyafufua mashirika nchini, ni kwa nini sasa Serikali isitoe mtaji wa kutosha ili hili shirika liweze kujiendesha. Shirika hili lilikuwa na deni kama la shilingi bilioni 5.1 ambapo Serikali imelipa shilingi bilioni 2.5 tu kwa shirika.
Sasa mimi ningeomba sasa hivi hili shirika lizingatiwe kwa sababu lilikuwa lina mali nyingi sana hapo zamani. Kwa hiyo mimi naomba wapatiwe pesa zao zilizobaki ili na lenyewe liweze kujiendesha ili wafanyakazi wale pia waweze kufanya kazi kwa kujiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nizungumzie mradi wa postal code na symbol za posta. Huu mradi kwa kweli umekuwa mara nyingi sana; kwanza ni muhimu sana kwa sasa hivi kwa sababu kwanza makazi yatatambulika, na isitoshe hatakukusanya kodi tutakusanya kwa urahisi kama nyumba zitakuwa zinatambulika kutokana na hizi symbol za posta, lakini mara nyingi sana imekuwa ikitengewa pesa kidogo sana kila mwaka, mimi naomba safari hii…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kuunga mkono hoja.