Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia hoja hii ambayo ni ya muhimu sana kwa mwananchi wa kawaida na hata mwananchi yoyote wa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, napenda kumshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli na hususan Waziri Mheshimiwa Profesa Mbarawa. Kazi ambayo Wizara hii imeifanya katika kipindi kifupi ni kazi ambayo inatakiwa isifiwe na ni kazi ambayo kila mtu ameiona. Katika kipindi kifupi Serikali hii ya Awamu ya Tano imeweza kutufanyia mambo mengi, imeweza kuleta ndege hapa. Kuna ndege sita; mbili zimeshafika. Zaidi ya kuleta ndege hizi kuna nchi nyingine ndogo tu kama Mkoa hapa nchini, zina ndege kubwa na sisi nchi hii tumeshindwa kuleta ndege na Mheshimiwa Rais ameweza kuifufua ATCL. Kwa hiyo, tumpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ameweza kuleta flyover. Flyover zimeanza kujengwa, zitapunguza msongamano mkubwa sana hapa nchini hasa ukichukulia maanani pia kwamba watu wote wanahamia hapa Dodoma sasa hivi, kwa hiyo, msongamano kule Mjini Dar es Salaam utapungua kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha msingi zaidi ni kuweza kuleta treni ya standard gauge ambayo kwa kweli ni treni ya kisasa. Kule nchi za nje wenyewe wanaiita bullet train. Sasa umuhimu wa treni hii kwa kweli utakuja kuonekana hasa wale ambao wataingia Bungeni mwaka 2020; wataacha magari yao yote Dar es Salaam na kuingia kwenye hizi treni. Kwa hiyo, mambo haya pamoja na mambo mengine ya vivuko ambavyo vimewahi kufanyika na mambo mbalimbali ambayo yamewahi kufanyika kwa kweli napenda kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Mbarawa ametembea nchi nzima hii kwa ajili ya kukagua miradi, ametembea kote, amekuja Tanga karibu zaidi ya mara tatu, ingawaje bado Muheza hajafika, namsubiri. Lakini nangependa kumshukuru sana, yeye na wataalam wake kazi ambayo wameifanya kwa kweli ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi zote hizo, lakini pia safari hii Wizara hii imeweza kuangalia Mkoa wa Tanga; tunajua tumepata zabuni ya kutengeneza bomba la mafuta kutoka Hoima kule Uganda mpaka kwenye Bandari ya Tanga, lakini kwenye kitabu hiki nashukuru sana Wizara imeanza kuboresha Bandari ya Tanga na tumefanikiwa kupata karibu shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kutengeneza bandari hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha msingi ni kwamba Mheshimiwa Waziri amesahau kuangalia reli ya Tanga. Reli ya Tanga ndiyo chimbuko, tena reli ya Tanga imeanza kabla hata ya hii reli ya kati, lakini sijui kwa nini hakuigusia, hata kuiangalia. Namuomba aangalie kwa kadri atakavyoweza tukitilia maanani kwamba tuna bomba la mafuta, tuna kazi kubwa, Tanga inataka kufufuka, kwa hiyo, tunaomba aangalie atafanya namna gani ili na reli ya Tanga iweze kuwa kwenye kupata standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, pia kuna na barabara ambazo zimesaidia sana, zinataka kutoa vitu kutoka Mkoa wa Tanga ili viende kwenye Mikoa mingine. Mheshimiwa Waziri ametusaidia sana kwenye barabara ya Bagamoyo – Saadani - Pangani ambapo barabara hii kwa kweli ndiyo tumepata hela ambazo ni kianzio tu, lakini tunashukuru sana. Tunaamini kwamba baada ya barabara hii kutengenezwa basi Tanga inaweza kufunguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo, ukitilia maanani pia tuna barabara ya Handeni - Kibarashi pamoja na Kibaya ambayo inakuja kutokea Singida. Barabara hii imewekewa hela ndogo, lakini tunaamini kwamba huu ni mwanzo tu, ataweza kuifikiria kuweza kuongezea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la msingi zaidi ambalo limenifurahisha kwenye bajeti hii ni kuweza kuweka hela za kutengeneza barabara ya kutoka Amani mpaka Muheza kilometa 36. Barabara hii safari hii imewekewa hela karibu shilingi bilioni tatu. Najua ni mwanzo tu, najua kutokana na jinsi nilivyokuwa namghasi Mheshimiwa Waziri atatuongezea hela, lakini hii ni chachu! Barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi katika Wilaya ya Muheza na ninaamini kabisa kwamba wana Muheza hasa watu wa Amani kama wananisikia watafarijika sana kuona kwamba barabara hii safari hii imewekewa hela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami namwambia Meneja wa TANROADS, Engineer Ndumbaro ambaye yupo kule, anafanya kazi nzuri sana na mara baada ya hizi fedha kufika, basi barabara hii, kama watu wa Amani wananisikia, itaanzia Amani kuteremka mpaka Muheza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, tuliahidiwa kilometa tatu na Mheshimiwa Rais alipokuja, alipata vumbi sana pale Muheza na akaahidi na tunazitegemea hizo kilomita tatu basi zitapunguza vumbi ambalo lipo pale Mjini Muheza.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko barabara nyingine ambayo inatoka kwenye junction ya Pangani, Boza. Barabara hii ni muhimu sana kwa watu wa Muheza. Sasa hivi inashughulikiwa na TANROADS na tuliomba sana iingizwe kwenye mpango huu wa sasa hivi kwa sababu barabara hii inatoka Boza junction na inapita Muheza, inakwenda moja kwa moja mpaka inapita Misozwe, inakwenda mpaka Maramba. Sasa barabara hii tuliomba hata tupewe hela ziingie hata kidogo kwa ajili ya kufanyia upembuzi yakinifu tayari kwa kuwekewa lami. Tungeshukuru sana kama utasikia kilio hiki kwa sababu niliwahi kuiongelea barabara hii kwenye bajeti iliyopita na ninaamini kwamba hata safari hii utaweza kuangalia unaweza kuifanyia vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambazo tuliomba zipandishwe hadhi na ziweze kushughulikiwa na TANROADS na barabara hizo tumeshazipitisha kwenye RCC. Barabara hizo zipo tano; kuna barabara ya Kilulu ambayo inakwenda mpaka Mtindiro inapita kwa Fungo. Tunaomba sana ipandishwe hadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Kibaoni - Misarai - Zirai inatoboa mpaka inakwenda Korogwe. Barabara hii ningefurahi sana kwa sababu inatoboa kwenye Jimbo la Profesa wangu Maji Marefu. Tumekuwa tunaipigia makelele sana; tungefurahi sana kama ingeweza kupandishwa hadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara ya Potwe - Shambakapori na Amtiko inapitia Masuguru mpaka Kerenge. Sasa tutashukuru sana kama ungeweza kutuangalizia barua hizo ambazo tumeshapitisha kwenye RCC na tungeshukuru sana kama ungeweza kutusaidia hizi barabara zishugHulikiwe na TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mawasiliano. Tarafa ya Amani ina matatizo sana ya mawasiliano, nilizungumzia bajeti iliyopita na nilishakuja Wizarani na nikatoa kilio hichi kwamba uchumi wa Muheza unategemea sana Amani, lakini sasa watu wenyewe kule hawana mawasiliano ya simu. Tulikuwa tunaomba kampuni moja ya simu ituwekee minara kule. Maeneo ya Misarai, Mbombole, Zirai, Kwemdimu, Tongwe na Kiwanda kote kule kuna matatizo sana ya mawasiliano ya simu. Kwa hiyo, ningeshukuru sana kama ungewaamuru hata kampuni moja tu iweze kutuwekea, ingewasaidia sana watu wa Amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miradi, Wizara hii ina miradi mingi sana, lakini ningeshukuru sana kama miradi hii ingeanza kushirikiana na PPP. Watu binafsi ni watu muhimu sana. Nchi zote duniani sasa hivi zinashirikiana na watu binafsi na bila watu binafsi tutachukua miaka mingi sana kukamilisha hii miradi. Mmewahi kuona acha hii miradi mikubwa ya madaraja au barabara, lakini barabara zote sasa hivi, hata nchi zilizoendelea zinatumia road toll. Sasa huu mpango ambao unatumia sasa hivi wa kukata hela kidogo za mafuta hauna effect. Mimi ningeshukuru sana kama mngeanzisha road toll ili watu binafsi wajenge hizi barabara na mwingie makubaliano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kama Mheshimiwa Waziri ukisimamia vizuri huu urasimu ambao upo hapo treasury wa kuweza kutoa hizi zabuni kwa watu binafsi, ungeusimamia naamini kabisa kwamba sasa hivi tungekwenda kama rocket kwenye hii nchi. Kwa hiyo, uchukue hayo mawazo na uangalie kwamba utaweza kuyatekeleza kwa namna gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaamini kabisa kwamba mambo yote ambayo Mheshimiwa Waziri ameyafanya, safari hii ameiona Tanga vizuri, lakini tunaomba aangalie kabisa suala la reli yetu ya Tanga na pia tunaomba aangalie kwenye kiwanja chetu cha ndege kwa sababu kitakuwa busy sana sasa hivi, tunategemea kupata Waziri wa Viwanda hapa, ndugu yangu ametuletea kiwanda kikubwa sana kule, sasa kutakuwa na mambo mengi sana Tanga, bandari inafanya kazi vizuri na imeshaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, tunaomba uangalie kiwanja chetu na chenyewe kiweze kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na ninazidi kuipongeza Wizara hii kwa kazi ambayo imefanya. Wizara hii imekuwa ni kioo cha Wizara nyingine nyingi hapa. Kazi ambazo zimefanyika, zinaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kushukuru na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana.