Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Serengeti, lakini pia nichukue nafasi hii kuwapa pole kwa tatizo kubwa la njaa walilonalo. Nafahamu wana hali mbaya kweli kweli, lakini niwaambie tu Serikali imekubali kufanya tathimini ya mahindi yaliyopo Shinyanga kwenye ghala la Serikali na watapata mgao wa mahindi kwa ajili ya kupunguza mfumuko wa bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo, sasa nijielekeze moja kwa moja kwenye Wizara husika. Naomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako mnisikilize kweli kweli hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 mmekuja ndani ya Wilaya ya Serengeti kuhusu barabara ya Makutano
- Mgumu - Mto wa Mbu. Ni barabara ambayo imeanza kujengwa tangu mwaka 2013 mwezi wa tatu. Kipande cha kilometa 50 kuanzia Makutano mpaka Sanzate, mwaka 2016 nimeongea hapa sana; sasa hivi ninavyoongea hapa wamepewa almost shilingi bilioni 26 kama sikosei, lakini mpaka leo miaka zaidi ya minne bado hata kilomita moja haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alipokuja Jimbo la Serengeti kutembelea ile barabara, bahati nzuri tulikuwa naye, tulikaa tukaongea na alitoa tamko kwenye vyombo vya habari kwamba ikifika mwezi wa nne, kama hata kilometa moja haijakamilika, hawa wakandarasi tunawatumbua. Mheshimiwa Waziri, huu ni mwezi wa ngapi? Hata kilometa moja bado.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind up aniambie lile tamko alilolitoa kwenye vyombo vya habari na huu ni mwezi wa nne umeisha, hata kilometa moja bado haijakamilika, umechukua hatua gani kulingana na maneno aliyoyasema ambayo kimsingi wananchi wa Mkoa wa Mara, Musoma, Bunda na Serengeti walimsikia akitoa tamko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri, barabara hii ilitakiwa itengenezwe kwa kiwango cha lami kuanzia Makutano mpaka mpaka wa Hifadhi ya Serengeti National Park pale Tabora B; naona mmekomea pale Mugumu Mjini. Kilometa 18 hazieleweki. Naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kusema, atuambie hizi kilometa 18 kutoka Mugumu mpaka mpakani mwa Hifadhi ya Serengeti kwa maana ya geti la Tabora B, wataitangaza lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye barabara hii mwaka 2016 imetengewa shilingi bilioni 20; upande wa Arusha shilingi bilioni nane na upande wa Mara shilingi bilioni 12. Sasa mwaka huu mpaka ninavyoongea kipande ambacho kimetangazwa cha kuanzia Mugumu kwenda Nata na Isenye bado mkandarasi hajapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda sasa kupitisha bajeti ya Mheshimiwa Waziri na Mkandarasi hajapatikana, nitaomba aseme chochote kuhusu upatikanaji wa mkandarasi wa kujenga hii barabara. Na mimi namwomba Mheshimiwa Waziri, bahati nzuri yeye sio mwanasiasa, amekuja pale nimemwona, hana mambo ya ubaguzi ubaguzi kama wengine, nampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie ili barabara hii ikamilike. Kimsingi, tunawapenda wakandarasi wa ndani, lakini kama hawawezi kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba, kwa nini tuendelee kuwa-entertain?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri ukumbuke Mheshimiwa Waziri, hii barabara ilianza kuwekwa kwenye Ilani ya CCM tangu enzi za Nyerere. Nyerere akaondoka akaja Mwinyi, akaja Mkapa; na wakati wa Mkapa kumbuka pia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli ndiye aliyekuwa Waziri wa Ujenzi. Akaondoka, amekuja Kikwete; Mheshimiwa Dkt. Magufuli huyo huyo ndiye alikuwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie tu kwamba wananchi wa Serengeti na wananchi wa Mkoa wa Mara, walimpa kura Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa sababu walijua akiwa Rais, hizi barabara zitakamilika upesi. Sasa tunaenda 2020 sijui mtasemaje kama zitakuwa hazijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, barabara ya Tarime - Mugumu inafanyiwa feasibility study. Wananchi wa Jimbo la Serengeti wanataka wajue ni lini barabara hii itaanza kulimwa? Kwa hiyo, utakapokuja naomba useme kuhusu barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka niseme, tuna barabara ya Musoma inaitwa Nyankanga - Rung’abure ambayo kimsingi mkoa kwa maana ya TANROADS wameanza kujenga kilometa mbili, wameanza kidogo kidogo. Kwa hiyo, naomba kwa niaba ya wananchi wa Serengeti na wananchi wa Mkoa wa Mara, barabara hii iingizwe kwenye barabara za kufanyiwa upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka niseme, ni vizuri mfahamu kwamba Hifadhi ya Serengeti ambayo ndiyo hifadhi inayoongoza Afrika kwa kuingiza watalii wengi na watalii wengi wanaoingia Hifadhi ya Serengeti wanatokea Kenya, ni vizuri mfahamu umuhimu wa barabara hii kwamba ni kiungo kikubwa cha kiuchumi katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri mfahamu kwamba Serengeti National Park ambayo ina tembo na simba wengi, wanaathiri watu wa Serengeti, ni vizuri mkafahamu ni mbuga ambayo duniani inatambulika, lakini unapoenda Serengeti unatwanga vumbi kuanzia Bunda mpaka Mugumu; kuanzia Tarime mpaka Mugumu na kuanzia Musoma mpaka Mugumu, sidhani kama mnamtendea haki hata Baba wa Taifa ambaye jana tulikuwa tunamuenzi kwa sababu ya makubaliano ya Muungano walioufanya na Rais wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie, katika Jimbo la Serengeti, bado hali ya mawasiliano kwa maana ya minara ni shida kweli kweli. Mwaka 2016 nilisema hapa kwamba ukienda kwenye maeneo ya mbuga yetu ya Serengeti ambako kimsingi tuna population kubwa mle ya watalii na nini, mawasiliano ni shida kwa maeneo ya Robo, Birira, Seronera na maeneo mengine ya mbuga yanahitaji mawasiliano ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Wilaya ya Serengeti, kuna maeneo ambayo tunahitaji minara. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye hili la minara, naomba uniambie, ni lini maeneo hayo yatapata minara ya simu, ama Vodacom ama Halotel? Kwa hiyo, ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo, nachukue nafasi hii kukuomba hayo mambo ya msingi ambayo wananchi wangu wa Serengeti wamenituma, wanataka kusikiliza kutoka kwako Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nashukuru sana.