Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hii Wizara. Kwanza kabisa napenda niungane na wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu ambao wamepata athari kubwa sana kutokana na mvua ambazo zinakaribia kuisha, athari ambazo zimesababisha watu karibu saba hivi kupoteza maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda niishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambao baada ya kusikia tatizo hilo, wameweza kufika mahali pale na kuweza kufanya tathmini na kutoa huduma ya kwanza kwa wale walioathirika, takribani nyumba 200 hawana makazi mpaka sasa. Nawaomba wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu, Mwenyezi Mungu atupe wepesi wa kuvumilia na tatizo hili ninalishughulikia na niko pamoja na ninyi katika matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niishukuru sasa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ambayo imeanza kutekeleza ilani yake. Unajua waswahili wanasema, mti wenye matunda hauishi kupigwa mawe. Ukiona mti haupigwi mawe, ujue una kasoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa wetu ni mti wenye matunda na sasa tunatekeleza na haya ndiyo
tunayotekeleza. Amesaini mikataba mingi ambayo Mheshimiwa amekwishaongea, sitaki kurudia, lakini ni ukweli na uwazi ambao unaonekana kwa juhudi ya Serikali ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, namna ambavyo inafanya kazi kwa bidii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja sasa katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Napenda niishukuru Serikali kupitia Wizara hii, nimekuwa na kilio cha muda mrefu sana kuhusu daraja langu la Kavuu ambalo ni kiungo cha barabara ya kutoka Majimoto mpaka Inyonga. Daraja hili ninavyosema, katika ufunguzi wa Mbio za Mwenge zilizofanyika Mkoa wa Katavi lilipitika. Aaah, nilitaka kusema CCM oyee! Mheshimiwa Naibu Spika, samahani!
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema napongeza sana. Kelele zangu na juhudi zangu zimezaa matunda daraja lile linapitika. Namuomba Mheshimiwa Waziri, sasa zile kilometa kumi zinazounganisha Majimoto kupitia daraja hilo kwenda Inyonga, sasa ziishe na daraja lile wananchi waweze kulitumia kwa ukamilifu kwa sababu, limetumia pesa nyingi ambazo ni kodi za wananchi. Kuliacha hivi hivi kwa kutokuwa na barabara tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Jimbo la Kavuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa maana kwamba Hospitali ya Wilaya iko Inyonga, wananchi wanalazimika kwenda Hospitali ya Mpanda ambako ni mbali. Sasa ni vema tukamaliza ile barabara tuwasaidie akina mama, watoto na wananchi kwa ujumla ambao wanaenda kupata matibabu mbali.
Pili, litatusaidia pia kuwasaidia wananchi wale kuweza kufanya biashara zao kati ya Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa barabara yangu ya Starike - Mpanda imekamilika; lakini naomba barabara ya kutoka Kizi – Kibaoni yenye kilometa 76.6 imalizike. Barabara ile kupitia upande wa pili wa Mlima wa Lyamba Lya Mfipa, imekuwa ni tatizo na kisababishi kikubwa cha ajali kwa sababu, hakijamalizika pale. Kwa hiyo, magari mengi yanakuwa yanatumbukia kule chini kiasi ambacho siyo rahisi kuokoa na imekuwa ikisababisha vifo vya watu wengi. Naomba barabara ile ikamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba barabara inaishia pale Kibaoni, barabara hii ya kutoka kibaoni ambayo imekuwa ikiulizwa humu na maswali mengi ambayo yamekuwa na majibu yasiyotosheleza, barabara ya kutoka Kibaoni kupita Muze mpaka Kilyamatundu ambayo inaenda kupita Daraja la Momba, naomba Mheshimiwa Waziri katika hotuba yako utakapohitimisha, tunahitaji majibu ya uhakika. Hatuhitaji kurudia maswali, tunataka leo tupate majibu ya uhakika, ni lini barabara hii itafanyiwa usanifu na ni lini itaanza kuwekewa lami? Kwa sababu, ni miaka kumi imepita tukiiongelea hii barabara ya kutoka Kibaoni mpaka Kilyamatundu kupitia Muze.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije kwenye aya ya 50 inayoongelea barabara ya Mpanda – Tabora – Ipole mpaka Sikonge. Barabara hii nashukuru imetengewa pesa na angalau tuna kilometa 30 kutoka Tabora Mjini mpaka Sikonge, sawa. Mahali pabaya ni kutoka Sikonge kupita Koga mpaka Mpanda. Sielewi kigugumizi kiko wapi hapa?
Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara Mheshimiwa Rais alipokuwa Waziri wa Ujenzi alinihakikishia na alinishirikisha maongezi na Mwakilishi Mkazi wa ADB pamoja na World Bank na wakakubali na pesa zilikuwa zimeshatoka. Ukisoma kwenye hii aya, wanakwambia pesa zilikuwa zimetoka, sasa ina maana zimeenda kufanya kazi zipi? Ama zinaendelea kufanya kazi ipi? Ni vema tukajua status ya hii barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara tumekuwa tukiipigia kelele kila siku. Kwa kweli, Serikali yangu naipenda,
inafanya kazi vizuri na ni sikivu. Naomba barabara hii sasa tuipe kipaumbele ili wananchi wa kule nao waweze kuondoa mazao kule. Mazao yako kule na mvua zimenyesha, mazao yameharibika, hawana pa kuyapeleka kwa sababu ya barabara mbovu. Tunaondokaje na umaskini na sisi tunataka twende kwenye kima cha kati? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, Profesa, nafikiri unanielewa ninapoongelea hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi za dhati kwa Serikali kuonesha nia ya kujenga reli ya kati. Napenda niseme, reli ya kati haiishii Mwanza, ina matawi yake aliyojenga Mjerumani ambayo inakwenda mpaka Mpanda mpaka Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Mheshimiwa Nsanzugwanko, aliongea vizuri sana kuielewesha jamii ya Tanzania pamoja na Serikali kwa ujumla reli ya kati maana yake ni nini?
Kwa hiyo, pamoja na kwamba tunaenda kwa vipande, naomba basi vile vipande vinavyobakia vingine visiishie Mwanza. Raha ya reli ya kati ifike Mpanda. Nashukuru kwamba mnatoka Mpanda mnaenda mpaka Karema, Karema mnajenga bandari pale mpaka Kalemii, tunashukuru sana. Sasa itoke pia Tabora – Urambo mpaka Kigoma. Hapo tutakuwa tumeweza kuwaunganisha wananchi wa huku kwetu pamoja na Ukanda wa Kongo, Burundi, Rwanda na Zambia kwa ajili ya biashara. Tunaweza tukainua uchumi kwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la viwanja vya ndege. Nimeona katika kiwanja cha ndege cha Mpanda ambapo pesa imetengwa kwa ajili ya kumlipa mkandarasi. Sasa tukishamlipa yule mkandarasi sijaona mwendelezo kwamba nini kitafanyika pale. Ule uwanja umejengwa, hautumiki. Ni kiungo kikubwa kwa kukuza uchumi kupitia maliasili zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Katavi National Park pale, kila siku nasema jamani, ile mbuga ina wanyama wakubwa hakuna mfano. Kuna twiga mrefu hakuna mfano, kuna twiga chotara ambaye hutampata Tanzania kokote. Naomba kile kiwanja; kitatuunganisha sisi na mbuga za Kigoma, tunaunganishwa na mbuga zinazotoka huko Kaskazini, watu watapenda kutembea sehemu mbalimbali za Tanzania. Tusisubiri mpaka sijui Clouds nini wale, wafanye utalii ndiyo na sisi tuamke, hapana. Naomba kabisa kwa dhati kile kiwanja mkiendeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa kule kutokana na ubovu wa barabara, msifikiri hawana uwezo wa kupanda ndege, uwezo huo tunao. Sisi tunalisha karibu nusu ya Tanzania, tushindwe kupanda ndege!
Kwa hiyo, tunaomba kabisa kile kiwanja sasa kifikie mahali tuone ndege zinatua, zinaondoka na watalii wanashuka pale, ili tuone ni kwa namna gani ambavyo tunaweza kukuza uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kwa mara nyingine, pamoja na kwamba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nitaleta maombi binafsi kwa Mheshimiwa Waziri, kuhusu barabara zangu za Katavi. Ahsante sana.