Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi ambaye kwa matakwa yake mwenyewe ametuchagua sisi kuwa miongoni mwa waja wake ambao amewatunuku uhai na uzima na akili timamu na akawajalia pia kufanya kile ambacho wamejipangia wenyewe kukifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa imani ya dini yangu, katika mambo ambayo tunaambiwa tuyafanye kwa wingi sana ni kukumbushana kwa sababu katika kukumbusha hutoa msaada kwa wale wenye kuamini. Nami nalifanya hilo nikiamini kabisa kwa dhati ya moyo wangu kwamba nyumba hii imejaa wenye kuamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu ambacho kwa dini yangu nakiamini, Kitabu cha Quran, kuna aya ya 54 iko katika Sura ya 36 na sura hii kwa jina lake mahsusi inaitwa “Surat Yaseen” na kwa hadhi yake hii sura ndiyo inaitwa ndiyo moyo wa Quran. Katika hiyo aya ya 54 inasema:-
“Iangalieni ile siku ya hukumu ambapo haitadhulumiwa nafsi chochote na wala haitolipwa isipokuwa yale ambayo imeyatenda”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliseme hili kama tahadhari kwetu sisi sote, iko siku ambayo hakuna chochote ambacho tutaulizwa isipokuwa kile ambacho tumekitenda hapa. Kwa imani ya dini yangu, maisha ya kila siku, mahusiano yetu, kusoma kwetu, kuwa Wabunge kwetu yote haya yataulizwa siku hiyo na hayo ndiyo katika hayo ambayo tunayatenda. Kwa hiyo, naomba nitoe hiyo tahadhari na nimwombe Mwenyezi Mungu ashuhudie kwamba nimewakumbusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuchangia kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hotuba hii ya Waziri Kivuli wa Kambi ya Upinzani lakini pia mengi yaliyomo kwenye taarifa ya Kamati ya Katiba na Sheria hususani yale ambayo yameelezwa ukurasa wa 18 na 19 kuhusu msisitizo wa kuangalia masuala mazima ya haki za binadamu hasa yakiendana na namna ambavyo vyombo vya kutoa sheria ikiwemo Mahakama vinavyotakiwa vitende haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki kuhoji Mahakama zinafanyaje kazi lakini nataka kuhoji sera za nchi hii, sheria na taratibu kuhusu masuala ya haki za binadamu. Mheshimiwa Waziri amesema hili na Kamati imesema na Waziri Kivuli amesema namna gani kesi zinacheleweshwa, namna gani mahabusu na wafungwa wanateseka katika nchi hii lakini tumenyamaza kimya au hatuchukui hatua inavyostahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mashekhe ambao wanaoza mahabusu kwa miaka minne sasa ambapo suala lao linapigwa danadana hilo sijui kama siyo suala la haki za binadamu au siyo katika zile kesi ambazo taarifa zote hizi zimesema lazima masuala ya upelelezi yakamilishwe katika wakati ambao ni reasonable. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri huyu ambaye yuko leo na hoja yake Mezani lakini jana alikuwa anatupa utaalam kama Profesa wa Sheria, alipokuwa anazungumzia Sheria ya Ndoa alisema kwamba, kuna kitu kinaitwa legal anthropology. Ombi langu ni kwamba hii legal anthropology sipati maneno sahihi lakini ninachotaka kusema ni kwamba isiangalie tu masuala ya abstract, zile values ambazo huzioni, lakini pia iangalie masuala ambayo ni real and tangible, yale unayoyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, inapokuja suala la dini, viongozi ni katika values hizo. Sasa tunapoona viongozi wetu wa dini wanadhalilika, wananyanyasika kwa miaka nenda, rudi, mjue mnatukwaza kiimani na mnateteresha hivyo vitu ambavyo mnasema legal anthropology inaviangalia kwa umakini sana. Kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kabudi utanisamehe huko mwishoni kama nitashika shilingi ya mshahara wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa Kabudi kama ambavyo Waziri Kivuli amesema hapa kwenye ukurasa wa nne kwamba hakuna shaka yoyote kwamba Ripoti ya Tume ya Warioba na Rasimu ya Katiba Mpya ina alama za vidole vya kitaalam vya Profesa Kabudi, ni kweli. Ninachoongeza tu ni kwamba alikuwa ana wasaidizi wake kama proof-readers wake, wanawake wawili, mmoja napenda nimtaje Mheshimiwa Kibibi Mwinyi Hassan, mwingine kwa leo nahifadhi jina lake, walifanya kazi ile kwa kukesha, tukatoka na document zile na mimi nilibahatika kuwa katika Tume ya Warioba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ripoti ile haikuzumngumzia tu pendekezo la Katiba Mpya lakini kuna masuala kadhaa ya kijamii, kisheria, kitaratibu ambayo Tume ya Warioba iliandaa kwa volumes na zikakabidhiwa Serikalini. Laiti mchakato ule ungefikishwa mwisho haya mambo yote hapa tunayozongwazongwa nayo sasa hivi yasingekuwepo. Taratibu zingekaa sawa, Katiba Mpya ingepatikana masuala yote haya tunayosema huyu asitajwe, huyu asifanywe hivi yalishajadiliwa na wananchi kwa kina kabisa mpaka suala la viroba na zile suruali ambazo vijana wetu wanavaa, wananchi walilisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama tungeupeleka mchakato mpaka mwisho wake yale yote yasingekuwa issue sasa hivi, lakini imekuwa hivyo kwa sababu suala la Katiba Mpya limekuwa kizungumkuti, sasa sijui nikisema limepigwa kaputi nalo nitaambiwa msamiati siyo, lakini ni katika lahaja tu na nadhani Waziri anayehusika na utamaduni alisimamie hili. Lugha yetu ya Taifa ni Kiswahili, tutumie utajiri wa lugha hii, tutumie lahaja ambazo zinaleta ladha masikioni, lugha ina ladha yake masikioni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilo la Katiba Mpya masuala ya maadili ya kijamii, mila na desturi zetu, tunu hizi za Taifa ikiwemo lugha yetu, uongozi na mihimili hasa mihimili hii mitatu versus masuala ya vyama vya siasa yamefanyiwa kazi vizuri kabisa. Wananchi walisema hatutaki kumuona Spika ambaye ni m-NEC, hatutaki kumwona Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Siasa na walitaja kwa vitu specific lakini hatukulifanyia kazi sasa hivi tunahangaishana hapa kila kinachosemwa kinaambiwa sicho, kila kinachoandikwa kinaambiwa kifutwe, lakini kile kisu cha jana kile kwa bahati mbaya kimebaki humu na kinaendelea kutesa watu, mimi sijui kisu gani. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia humu asubuhi haki ya msingi kabisa ikitetereshwa ambayo ni haki ya kujieleza. Hivi Mbunge, Waziri Kivuli anapozongwazongwa, anapokatazwa kueleza kile ambacho yeye ana imani nacho inashangaza. Mimi nitashangaa sana ikiwa Mawaziri Vivuli wa Kambi hii watarudia yale hotuba za Mawaziri wa upande ule itakuwa kituko! Yule Waziri akisema tumefanya kila kitu na Waziri Kivuli naye aseme Serikali ile imefanya kila kitu, itakuwa kiini macho gani hicho? Hebu tupewe haki hii ambayo tunaizungumzia hapa, haki za binadamu, utawala wa sheria uachwe utekelezwe katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kabudi amevishwa viatu au sijui amevishwa kilemba hiki ambacho inabidi akifanyie kazi sawasawa. Namshauri asisite kushauri mamlaka husika kuhusu utawala wa sheria unavyotakiwa kufanya kazi kwa sababu sasa hivi tumefikishwa mahali ambapo hatujui twende kwa sheria au kwa matamko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inasema, vyama vya siasa vipewe ruzuku vifanye kazi, vifanye shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara. Matamko yanasema, hakuna kufanya kazi za siasa, hakuna mikutano ya hadhara mpaka tarehe fulani, kipi ni kipi? Hii haifai na haikubaliki katika nchi ambayo tunasema tunafuata utawala wa sheria, tuna demokrasia ya vyama vingi lakini zaidi tunasema kila siku tuombeane dua, tuombeane Mungu, hatuwezi … (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)