Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia. Nakushukuru wewe, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Makamu wa Rais chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu na wanavyoshirikiana na Rais Dkt. Mohamed Shein wa Zanzibar kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri kwa hotuba yao nzuri, ambayo imetoa taarifa ya mambo ambayo yamefanyika mwaka huu na ambayo yanategemewa kufanyika mwaka ujao. Niseme tu kwamba kwa sababu muda ni mdogo, naunga mkono hoja kabla ya muda wangu haujakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifafanue tu kwamba Mheshimiwa Ngwali amezungumza hapa juu ya Sheria ya Mafuta na hili suala la Muungano. Naomba kuwaambieni hapa kwamba moja, Katiba haikuvunjwa wakati tunatunga sheria hii mwaka 2015 na bahati nzuri tulikuwa wote humu wengine wakaamua kuondoka tukabaki na Wabunge wawili wa Opposition. Sheria hii iliyotungwa inazingatia maslahi ya Muungano wa pande zote Zanzibar kama alivyosema Mheshimiwa Nahodha, kwavhiyo tuiunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 2 cha Sheria ya Mapato ya Gesi na Petroli hayatoi maelekezo kwamba Bunge la Zanzibar litunge sheria, inasema masuala ya mapato yanayotokana na gesi na petroli yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria zinazotungwa na Zanzibar, ndivyo hali halisi ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge naomba kuwatoa wasiwasi tuunge mkono suala hili. Tulichokifanya katika Sheria hii ya Petroli Kifungu cha 4, tulisema kwa sababu hili suala bado liko kwenye Katiba, tuliwekee utaratibu kwamba hili linabaki bado kuwa Jamhuri, lakini tukasema litasimamiwa na Serikali zote hizi mbili. Ukisoma hiki Kifungu ndivyo kilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikishasimamiwa na Serikali zote mbili, Katiba ya Zanzibar Ibara 88 inatoa mamlaka kwa Baraza la Wawakilishi kutunga sheria ku-regulate hiki kitu. Kwa hiyo, suala liko kwenye Katiba sawa la Muungano lakini utaratibu wa kushughulikia hayo mapato umewekwa kwenye sheria. Kwa hiyo hizi sheria hizi mbili ndicho nilichokuwa nazungumza hapa lisituchanganye sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hili ambalo Mheshimiwa Ngwali amependekeza kwamba, tulete mabadiliko ya Katiba hapa ili tuondoe suala hili kwenye Muungano. Hili anataka tu kuharakisha hoja, kwa sababu bado tuna kiporo cha Katiba Mpya na Katiba yenyewe kilichobaki ni kupigiwa kura. Muda muafaka tutapiga kura kwa Katiba Mpya, kama wananchi watairidhia ikapita ndiyo itakuwa Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi hapo Waheshimiwa Wabunge ni kwamba, unajua Zanzibar tayari imepata hii fursa, tusiwafanyie hiyana mbaya hapa, kwa sababu uliondoe kwenye Katiba sijui vitu gani, tayari wamepata hii fursa ya kusimamia hii rasilimali kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sitaki kwenda kwenye siasa ninachoweza kusema tu ni kwamba hakuna Katiba yoyote ambayo tumevunja kwenye hili. Hilo naomba kushauri hivyo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba kusema ni hili la Mheshimiwa Aeshi amelizungumzia na akaungwa mkono na Mheshimiwa Kangi Lugola. Unajua haya mambo mengine, haya masuala hoja zao hizi, haya masuala yako Mahakamani. Serikali ilipoanza zoezi hilo, watu walifungua kesi Mahakamani. Kama anachosema tumefanya maamuzi yanayovunja Katiba, Mahakama itaamua. Katiba hii msiisome upande mmoja tu isome holistically. Hatuwezi kuacha watu wanaumia, watu wanakuwa wahalifu, kwanza pia wanavunja sheria zile halafu tukasema eti sijui tunafanya vitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa huko vijijini huko Kahama, nimeenda kule wanasema wanaishukuru Serikali kwa hatua iliyochukuliwa. Wanasema watoto wetu walikuwa wanaenda kufa, halafu walikuwa wanashiriki uhalifu. Leo Serikali inachukua hatua hizi mnasema tuache, that cannot be entertained. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.