Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuweza kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchukua fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa namna ambavyo amekuwa akiniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya kusimamia Menejimenti ya Utumishi wa Umma pamoja na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee pia nimshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwani wao pia wamekuwa wakituongoza vyema na wamekuwa wakitoa msaada mno na ushauri ambao umenisaidia sana katika kutekeleza majukumu ya ofisi yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Bunge, Katibu wa Bunge pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati yangu kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanikisha majukumu ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Utekelezaji wa Sera, Mikakati mbalimbali Pamoja na Mipango. Wote tunafahamu namna ambavyo inahitaji kuwa na watumishi wa umma wenye weledi, uadilifu na walio makini kwa kuwa wote tunajua utumishi wa umma ndiyo nguzo ambayo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Nia ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni kuendelea kuiboresha Sekta yetu ya Utumishi wa Umma, kuhimiza katika misingi ya weledi, kuendelea kuweka mifumo ya menejimenti inayowezesha watumishi kuwajibika vyema, kuwa na maadili ili waweze kutoa huduma iliyo bora na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa umma endapo watazingatia sifa hizo nilizozitaja basi kwa hakika tutaweza kujionea utendaji mzuri zaidi wenye matokeo na hii itatuwezesha kuwa na tija zaidi, kuwa na mapato makubwa zaidi na hatimaye kuweza kuboresha zaidi maslahi ya watumishi wetu wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunaendelea kuhakikisha kwamba utumishi wa umma unaongozwa na kusimamiwa ili kuhakikisha kwamba hauendi kinyume na misingi hiyo niliyoitaja awali. Ili kuhakikisha kwamba tunalinda misingi hiyo, kama Serikali tumekuwa tukifanya mabadiliko na maboresho mbalimbali katika Sekta yetu ya Utumishi wa Umma, lakini vile vile katika sekta mbalimbali tumeshuhudia maboresho katika utendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia programu yetu ya Maboresho katika Utumishi wa Umma hadi mwaka 2014, lakini vile vile tumeanza kuchukua hatua kwa kushirikiana na DFID pamoja na World Bank kuona ni kwa namna gani tunaweza kuweka utaratibu mwingine na kubuni maboresho yatakayoendeleza mipango ya matokeo makubwa katika utoaji wa huduma kwa kuondoa vikwazo katika utumishi wetu wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano, tumekuwa tukichukua hatua mahsusi za kusimamia Sera na mifumo ya kimenejimenti, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, masuala mazima ya nidhamu, mapambano dhidi ya rushwa, uadilifu na uwajibikaji navyo pia tumekuwa tukiendelea kuweka mkazo. Sisi tunaamini kwamba tutakapozingatia haya, basi watumishi wa umma watafanya kazi kwa weledi na kwa bidii kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, niwaahidi tu kwamba kama Serikali tutaendelea kuimarisha vita dhidi ya rushwa ambapo kama hatua ya uadilifu, tutaendelea pia kuhakikisha kwamba viongozi na watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viapo vya taaluma zao, viapo vya uadilifu na pia kuhakikisha kwamba wanawajibika kwa matokeo ya kazi na maamuzi yao ili kuhakikisha kwamba tunaondokana na maamuzi na matumizi mabaya ya madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba yangu. Niwashukuru sana Wabunge 47 walioweza kuzungumza, niwashukuru pia Wabunge 27 ambao waliweza kuchangia kwa maandishi. Nawashukuru Wabunge hawa kwa kuongozwa na Mheshimiwa Rweikiza Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Makamu wake mwanamama machachari Mheshimiwa Mwanne Nchemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimtambue na kumshukuru Mheshimiwa Ruth Mollel Waziri kivuli wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa maoni na michango yao ambayo naamini kabisa itaweza kutusaidia kuboresha utumishi wa umma na utawala bora nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda hautoshi kuweza kujibu hoja zote, nitajitahidi kadri nitakavyoweza, lakini niwahakikishie tu kwamba katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la 11 Wabunge wote mtaweza kupata majibu yetu kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na hoja chache zilizojitokeza katika Utumishi wa Umma. Kulikuwa kuna hoja ya Kamati yetu ya Bunge, kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma ni vyema kikawezeshwa ili kiweze kumiliki majengo yake katika campus zake na hususan walitolea mfano wa campus ya Mbeya ambayo wamekuwa wakitumia gharama kubwa sana kwa aili ya kulipia pango. Niseme tu kwamba nawashukuru Kamati kwa namna ambavyo wamekuwa wakifuatilia utendaji wa Chuo hiki. Waliweza kufika katika campus ya Chuo chetu cha Mbeya, waliweza kujionea na kuweza kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, tayari tumeshawasilisha maombi kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wanaliangalia jambo hili kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ili kuona ni namna gani sasa Chuo cha Utumishi wa Umma tunaweza tukamilikishwa majengo haya kwa taratibu ambazo tutaweza kupangiwa na kuelewana kwa pamoja. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunasubiri maamuzi ya TAMISEMI na tunaenda vizuri, tunaamini tunaweza tukafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja pia ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo pia Mheshimiwa Sannda aliitolea maelezo pamoja na Mheshimiwa Bobali. Hii ni kuhusiana na umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wetu wa umma, lakini wao walienda mbali kwamba tupanue wigo sasa, katika mafunzo haya basi tuangalie pia ndani ya nchi lakini twende pia na nje ya nchi ili kuhakikisha kwamba watumishi wanakuwa exposed zaidi katika kupata mafunzo. Niwashukuru wote kwa hoja hii. Hakuna anayebisha hata kidogo umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu kwamba tunayo Sera yetu ya mafunzo kama Serikali lakini vile vile tunayo Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 1999 ambayo ilirekebishwa mwaka 2004. Kimsingi Sera hii pia inasisitiza katika umuhimu wa waajiri kuweka kipaumbele katika kuandaa mipango ya mafunzo ambayo itazingatia mahitaji yao halisi lakini pia kuhakikisha kwamba wanaongeza ufanisi katika sehemu zao za kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema tu kwamba kupitia ofisi yangu pia katika Idara ya Uendelezaji wa Rasilimali watu tumekuwa tukitafuta fursa mbalimbali za mafunzo ili kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wengi zaidi wanaweza kujiendeleza na kuweza kupata ujuzi. Nikichukua tu katika mwaka 2015/2016 zaidi ya watumishi wa umma 395 waliweza kupatiwa mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu nje ya nchi. Pia katika Mwaka huu wa Fedha zaidi ya watumishi wa umma 654 nao pia waliweza kupata mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba ni eneo ambalo tunalipa kipaumbele. Nipende kutoa rai kwa waajiri wetu mbalimbali, kama ambavyo wanatenga fedha kwa kuzingatia masuala mbalimbali ya kuzuia virusi vya UKIMWI pamoja na masuala mengine yanayowekewa mipango katika MTF, ni vyema sasa first priority katika bajeti zao wahakikishe kwamba kipaumbele kinawekwa katika mafunzo. Tusitafute visingizio na sababu kwamba hakuna fedha. Humo humo katika kidogo, tuone namna gani tunawajengea uwezo watumishi wetu.

Mheshimiwa Mweyekiti, kulikuwa na hoja ya utumbuaji wa watumishi na kwamba utumbuaji huo uchukuaji wa maamuzi ya kinidhamu ulikuwa hauzingatii sheria na umekuwa ukifanywa kwa ukiukwaji na hata umepingwa na Tume ya Haki za Binadamu. Nipende tu kusema kwamba waliotoa hoja hii hususan Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wanajua kabisa taratibu nzima za maamuzi ya kinidhamu, Sheria Namba 8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 imeeleza kabisa bayana taratibu. Zaidi ya hapo tunazo Kanuni za Utumishi wa Umma. Ukiangalia katika Kanuni ya 46 na 47 imeeleza bayana ni masuala gani na hatua zipi za kuzingatiwa pindi mamlaka ya ajira na nidhamu inapotaka kuchukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba, hatua hizi za kutengua teuzi, kusimamisha mtu kazi na kuwafukuza kazi zimeelezwa bayana. Ni yule tu mwenye mamlaka ya nidhamu ndiyo anatakiwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, niombe sana watu waendelee kufuata taratibu hizo na zaidi ya yote nisingependa kusikia sehemu zingine inaelezwa mchakato mzima usizidi siku 120 katika hatua za kinidhamu, lakini unashangaa kuna mwingine zaidi ya miezi minne tangu amepewa hati ya mashtaka shauri hilo halijahitimishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana na tunaendelea kuwafuatilia na kwa mwajiri yeyote tutakayembaini amekiuka taratibu, amekiuka masharti ya Kanuni ya Utumishi wa Umma katika kuchukua nidhamu tutahakikisha tunamchukulia hatua na ajira yake pia itakuwa mashakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kuendelea kusisitiza, hakuna mamlaka yoyote ya nidhamu inayoruhusiwa au inayopata ruksa ya kukiuka haki za watumishi kwa namna yoyote ile. Kwa hiyo, ni vyema tu waajiri wahakikishe kwamba wanazingatia Sheria, wanazingatia Kanuni, Miongozo pamoja na Taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine kuhusiana na upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta ya utumishi wa umma, mifano iliyotolewa ni kada ya afya pamoja na elimu. Waheshimiwa Wabunge walitaka kufahamu Serikali itaajiri lini watumishi wa kada hizo. Hoja hii ilitolewa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani lakini vile vile Mheshimiwa Rashid Chuachua, Mheshimiwa Bura, Mheshimiwa Atashasta na wengine wengi walilisemea hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kaka yangu Simbachawene ameanza kuliwekea utangulizi kidogo na niseme tu kwamba kama Serikali tunatambua umuhimu wa kuwa na rasilimali watu inayotosheleza kuweza kuhudumia wananchi wetu kwa utoshelevu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema, kama nilivyoeleza katika maelezo ya hotuba yabgu, tayari tulishatoa vibali zaidi ya 9,700 na wameshaingia kazini. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais pia, kwa kuona umuhimu wa Madaktari zaidi ya 258 na tayari Jumatatu wanaingia kazini. Nipende tu kusema huo si mwisho, tunaendelea pia na watumishi wengine katika kada zingine ili kuhakikisha kwamba kweli tunakuwa na utumishi wa umma wenye watumishi wa kutosha. Niwahakikishie tu kwamba kabla ya mwaka wa fedha haujakwisha mtakuwa mkisikia na kushuhudia watumishi katika sekta mbalimbali wakiendelea kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili kuweza kutoa neno lingine la kutia moyo, katika mwaka ujao tena wa fedha wa 2017/2018 tutaajiri tena kwa nyongeza watumishi wengine 52,436. Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba kama Serikali tunaliona na tunaendelea kuajiri kwa awamu kwa kuhakikisha kwamba haturudii makosa yale ya wakati ule ya kuwekwa wale watumishi hewa, kurudia makosa ya kuwa na watumishi ambao hawana sifa na weledi unaohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja kwamba Serikali hii imekuwa ni ya kuhakiki tu. Kwa kweli ni hoja ambayo imenishangaza sana mimi. Duniani kote, kama kweli unataka kuwa na utumishi wa umma uliotukuka hutaacha kufanya uhakiki wa rasilimali watu wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukakaa tukawa na watumishi wa umma zaidi ya laki tano na arobaini na mbili elfu na mia moja na sabini na sita bila kujua kila mmoja ana sifa na weledi, bila kujua kama kweli work load analysis kwa kila sehemu kila mtu ana kazi inayomtosheleza, bila kujua kama kila mmoja anatekeleza majukumu yake inavyotakiwa, bila kujua kama kweli ana sifa na weledi unaotakiwa katika utumishi wa umma, lakini pia bila kujua kama kweli yuko kazini au hayuko kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba kwa sasa zoezi la jumla la uhakiki ni kama limeisha lakini uhakiki ni endelevu. Mkija mkisikia uhakiki mwingine unaendelea wala msishangae, tutaendelea kufanya hivyo na wala hatutafanya hivyo kwa kuwa tunaogopa mtu yoyote au kusikiliza maneno kwamba tunatishwa tusifanye uhakiki kwa kuwa Serikali hii itaonekana ni Serikali ya kufanya uhakiki kila kukicha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako ambao walitaka kufahamu uhakiki huu matokeo yake yamekuwaje. Nipende tu kusema kwamba kama mlivyofahamu, zaidi ya watumishi hewa 19,708 waliweza kubainika katika orodha yetu ya malipo ya mishahara na waliondolewa. Endapo tungewaacha hawa katika ajira ingeigharimu Serikali kila mwezi Shilingi bilioni 19.8, hivi ni fedha ndogo hizo? Si fedha ndogo hata kidogo! Ziko baadhi ya Wizara zingine ndiyo bajeti yake ya mwaka mzima huo. Kwa hiyo nipende tu kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge watuelewe, tunapofanya haya tunafanya kwa nia njema kuhakikisha kwamba hakuna mianya hata kidogo na kuhakikisha kwamba fedha za Serikali zinatumika kwa matumizi sahihi ili walipa kodi waweze kujionea manufaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hiyo tu, tumewaeleza hapa ajira mpya tutakazozitoa zaidi 52,000 katika mwaka ujao wa fedha. Tunapoendelea pia kutoa watumishi hawa hewa, pia inatengeneza fursa zingine kwa ajili ya watu wengine wahitimu ambao wako nje wanasubiri ajira. Hivi tusingewatoa hawa 19,000 si tungeendelea kuziba ajira? Tunaendelea kila mwezi kulipa zaidi ya bilioni 19.8. Kwa hiyo, nipende tu kuwahakikishia Wabunge pia hiyo ni fursa nyingine kwamba wahitimu wetu wataendelea pia kupata fursa hizo za ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu walitaka kufahamu pia kwamba mpaka sasa katika watumishi hawa hewa 19,700 waliondolewa, wale maafisa walioshiriki katika kuhakikisha kwamba watumishi hao hewa wamekuwepo wamechukuliwa hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba katika zoezi zima la kuondoa, tumehakikisha pia kwamba kwa yeyote aliyeshiriki na mpaka sasa tumeshawabaini zaidi wa watumishi 1,595 wa madaraka mbalimbali au ngazi mbalimbali ambao wamehusika katika uwepo wa watumishi hewa katika orodha ya malipo na mishahara na tayari tumeshawachukulia hatua mbalimbali. Wako ambao tayari wana kesi mahakamani, wengine wamechukua hatua nyingine za kisheria na wako ambao wamefukuzwa kazi, lakini zaidi ya yote, zaidi ya bilioni 9.3 zimesharejeshwa Hazina na tunaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kila fedha iliyochukuliwa basi fedha hiyo itarudi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine ya Walimu ambao walipandishwa vyeo na hii inaendana pia na watumishi wengine wa umma, lakini baadaye mshahara wao ukarudi kwenye mshahara wa zamani na watu walitaka kufahamu mishahara hiyo itarekebishwa lini na hiyo ni pamoja na watumishi wa umma waliopandishwa madaraja wakarekebishiwa mishahara yao kwa wakati ni nini kitafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema, kwanza kabisa wapo ambao walisema miaka mitatu mtu automatic ana sifa ya kupanda cheo. Nipende kutofautiana nao, mtumishi anapanda cheo kwa kuzingatia muundo wake wa maendeleo ya utumishi, mtumishi atapanda cheo kwa kuwa ameshatimiza sifa si chini ya miaka mitatu, siyo fixed kwamba ni lazima miaka mitatu unapanda.

Pili, ni lazima bajeti hiyo ya wewe kupandishwa cheo iwe imekasimiwa na mwajiri, lakini tatu uwe na utendaji uliotukuka katika kipindi chote hicho na uwe umejaziwa tathmini ya form ya OPRAS kwa zaidi ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba tutaendelea kufuatilia na kuhakikisha kwamba watumishi wanapanda kwa kuzingatia sifa na kwa kuzingatia utendaji uliotukuka. Kwa hiyo, kupanda cheo si automatic, tutaangalia vigezo hivyo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wako kweli ambao walipandishwa hadi kufikia mwezi Juni, 2016. Wako ambao walishapata mshahara uliorekebishwa mwezi mmoja, wako waliopata mishahara iliyorekebishwa miezi miwili, wakarudishwa katika mishahara ya zamani. Nipende tu kusema kwamba, Serikali ilifanya hili kwa nia njema na lengo lilikuwa ni kuwapa fursa Serikali kuweza kuupitia muundo wake upya ili pia kuhakikisha kwamba tunaondoa watumishi wale hewa, lakini pia kutoa nafasi ya kuendelea kuhakiki vyeti vya kidato cha nne, kidato cha sita na vya vyuo vya ualimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba, tayari zoezi hili limekamilika. Kwa upande wa uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne tunategemea mwezi huu litakamilika na matokeo yake naamini mmeshaanza kumsikia Mheshimiwa Rais na tusubiri baada ya hapo ni nini kitakachofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema, kwa wale waliopandishwa wote ndani ya mwaka huu wa fedha, wataweza kupandishwa na kurudi katika madaraja yao sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia kuna hoja kuhusiana na TASAF. Wako ambao, especially Kamati, ilisema kuwa kwamba kuna kasoro katika usimamizi, katika utambuzi na katika uandikishaji wa kaya za walengwa wetu wa mpango wa kunusuru kaya maskini. Pia wako Waheshimiwa Wabunge wengi kina Mheshimiwa Nditiye, Mheshimiwa Sikudhani, Mheshimiwa Ikupa na wengine wengi, walieleza hisia zao kwa namna ambavyo waliona zoezi hili kwa namna moja au nyingine utambuzi haukwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao walitoa maoni zaidi, katika suala zima la kuondoa kaya ambazo zilikuwa hazistahili na hasa walikuwa wanaamini kwamba wako wengine waliondolewa bado ni maskini, lakini mbaya zaidi wametakiwa warejeshe fedha. Nipende tu kusema kwamba, uhakiki huu ulifanyika kwa nia njema na tayari tumeshatoa miongozo katika halmashauri zote nchini pamoja na halmashauri zote za Zanzibar kusitisha kuwaondoa walengwa ambao ni kaya maskini, ambazo ziliingizwa katika mpango kwa kufuata taratibu zote ambazo zilitakiwa na tayari kaya hizo zimeshaanza kurejeshwa kwenye mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote, tatizo kubwa lililojitokeza unakuta wengine walikofanyiwa uhakiki walipoonekana hali zao zimeboreka wakaondolewa. Kwa hiyo, tumetoa maelekezo kwamba mtu ataingia kwenye graduation strategy baada ya kuwa tathmini imeshafanyika ili kuhakikisha kwamba kweli hali yake imeboreka na hataweza kurudi katika umaskini. Kwa hiyo, niwape tu comfort kwamba wameshaanza kurudishwa na hakuna atakayedaiwa fedha hizo kama kweli mtu huyo ni maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaotaka kuhangaika nao ni wale ambao waliingizwa kama ni kaya zisizo na sifa, ni wale ambao waliingizwa ni watumishi wa umma, ni wafanyabiashara na wenye kipato na wameingizwa na kuonesha kwamba hawana uwezo wakati uwezo huo wanao. Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba hili litafanyika vizuri na hakuna atakayeonewa lakini zaidi niwashukuru kwa namna ambavyo mmelisemea kwa hisia kubwa na kwa namna ambavyo mmekuwa mkilifuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wabunge wengi pia wamekuwa wakilisemea hili, kuhusiana na asilimia 30 ya vijiji vya walengwa wa TASAF ambavyo bado havijafikiwa, sasa hivi tumefikia asilimia 70. Kamati ya Bunge imelieleza hili, Mheshimiwa Bobali amelieleza, vile vile Mheshimiwa Rhoda Kunchela naye pia ameweza kulisemea. Nipende tu kusema, mpaka sasa hatujafikia mitaa, vijiji na shehia 5,690.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu ilikuwa ni mwaka huu tufanye utambuzi pamoja na uandikishaji lakini bahati mbaya kutokana na ufinyu wa bajeti, zoezi hilo la utambuzi halikuweza kufanyika. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge, katika awamu hii ya kwanza itakapomalizika Serikali imetuhakikishia kwamba itatenga fedha kupitia mchango wake wa ndani ili kukamilisha zoezi la utambuzi pamoja na uandikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya hatua gani zimechukuliwa dhidi ya waliovuruga utaratibu na kuingiza walengwa wa TASAF ambao hawastahili. Mheshimiwa Lubeleje, Mheshimiwa Malembeka, Mheshimiwa Maige na wengi tu pamoja na kamati wamelieleza vizuri sana. Kwanza niwashukuru kwa namna ambavyo mmekuwa mkifuatilia, lakini niwaombe pia, kwa kuwa na ninyi ni Madiwani na tumewagawia orodha pia muweze kufuatilia katika orodha ya ruzuku iliyofika katika maeneo yenu, kujiridhisha kama kweli pia ruzuku hiyo katika mizunguko yote hiyo imefika au haijafika ili muweze kuwa pia jicho na sikio letu kwa niaba ya Serikali huko katika maeneo yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshachukua hatua, zaidi ya waratibu wa mpango 84 walioko katika halmashauri wameshachukuliwa hatua na wamesimamishwa na sasa hawawezi kushughulikia au kuratibu shughuli za TASAF. Vilevile Watendaji wa Vijiji pamoja na Kata na Mitaa 156 nchi nzima wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi lakini si hiyo tu hata TASAF kwenyewe Makao Makuu kwa sababu nako pia wamehusika katika usimamizi. Zaidi ya watumishi 106 walisimamishwa kazi na hatimaye wameweza kuchukuliwa hatua na wengine wamepewa onyo ili kuhakikisha kwamba upungufu kama huu hauwezi kujirudia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, watumishi saba waliokuwa makao makuu ambao mikataba yao imekwisha na walionekana pia utendaji wao ulikuwa haujaridhisha nao pia mikataba yao haijaweza kuhuishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya Mfuko wa Rais kujitegemea kuweza kuwezeshwa kifedha. Nipende tu kusema kwamba, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mama Kilango, Mheshimiwa Ritta Kabati na wengine wote ambao wameweza kuusemea Mfuko huu wa Rais wa Kujitegemea. Ni kweli ni Mfuko ambao ni wa muhimu sana, ni Mfuko ambao una historia ya muda mrefu, tangu hayati Sokoine mwaka 1984 ambaye alidiriki hata kuchangia sehemu ya mshahara wake, kuweza kuanzisha Mfuko huu. Niwashukuru sana lakini nipende tu kusema kwamba katika mwaka huu tumeutengea Shilingi milioni 500 na tunaamini itaweza kusaidia katika kutimiza malengo yake na Serikali itakuwa ikiongezea fedha kila mara itakapokuwa na uwezo ulioboreka katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Mama Kilango, kwamba ni lini Mfuko huu wa PTF utaanza kutoa huduma zake Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mama Kilango kwamba katika mwaka 2018/2019, PTF imejiwekea mipango ya kwenda Kilimanjaro pamoja na Tabora pamoja na mikoa mingine tutakuja kuitangaza huko baadaye. Kwa mwaka huu tutaenda Dodoma, Iringa pamoja na Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kulikuwa kuna hoja Mfuko huu unaonekana ni wa Muungano, kwa nini haufanyi shughuli zake Zanzibar? Ni hoja nzuri sana. Nipende tu kusema kwamba, Zanzibar upo Mfuko wa Rais wa Kujitegemea pia kupitia SMZ ambao unafanya kazi nzuri, ambacho tunakifanya sasa ni Mifuko hii miwili kuwa na ushirikiano na kuweza kufanya kazi pamoja lakini hoja hii tumeisikia tutaona ni namna gani pia inaweza ikafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya Mheshimiwa Kishoa kwamba Serikali hii imekosa utawala bora, kiasi kwamba haipati mikopo, kiasi kwamba haipati misaada. Kwa kweli nipende tu kusema ni hoja ambayo kidogo imenishangaza na inasikitisha. Kwa takwimu zilizopo Waziri wetu wa Fedha amekuwa akifanya majadiliano mengi tu na amekuwa akisaini mikataba mingi tu na mikataba hii imekuwa ikiwa na mafanikio makubwa. Nitoe tu mfano, ukiangalia hadi sasa kupitia Kuwait Fund na Serikali wameingia mkataba na zaidi ya dola milioni 51 tayari kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahuwa umepitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa EU na Tanzania Rais amehakikishiwa fedha zitatoka; lakini nisiende mbali nikienda kwenye TASAF tu peke yake, DFID imetoa zaidi ya dola milioni 170, ndogo? Benki ya Dunia imetoa zaidi ya dola milioni 420, Irish Aid imeahidi kutoa zaidi ya dola milioni 11, USAID inatoa dola zaidi milioni 10 hapo sijaenda mbali kwenye Wizara zingine, niangalie tu zinazonihusu kwa harakaharaka. Sijaangalia TAKUKURU, sijaangalia Maadili na kwingineko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipende tu kusema kwa kweli, hebu tusiupotoshe umma kuonekana kwamba ni Serikali ambayo haina utawala bora. Utawala bora upo, fedha zimetoka, Abu Dhabi fund wametuahidi, barabara zinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huko Iramba kwa Mheshimiwa Kishoa naamini mafanikio yako mengi tu na wananchi wako wanakusikia unaposema uongo, watakapokuja kuona hizo fedha hazipo tutakuja na tutafanya ziara huko Iramba pia kuweza kusema kama ni uongo au ni kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kuhusiana na semina elekezi kwa viongozi walioteuliwa. Tumekuwa tukifanya hivyo, tukitoa mafunzo kwa kutambua umuhimu wa viongozi wenye uwezo wa kitaalam, lakini ambao wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utawala bora. Kila mara tulipoona inahitajika tumekuwa tukitoa semina hizo na mafunzo kuhakikisha kwamba wateule wetu na watumishi wetu wanapata mafunzo kuhusiana na namna Serikali inavyofanya kazi, wanapata mafunzo kuhusiana na namna Serikali ilivyo na utamaduni wake, kupata mafunzo ya namna ya kuwa mtumishi bora wa umma pamoja na wao kuelewa majukumu yao mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nipende tu kuhakikisha kwamba, tutaendelea kufanya hivyo na hata katika mwaka huu wa fedha tunaoumaliza mpaka Juni zaidi ya viongozi 80 watapata mafunzo na mpaka ikifika Desemba viongozi wote watakuwa wamepatiwa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya madai ya malimbikizo na namshukuru kaka yangu Simbachawene ameeleza. Katika madai yasiyo ya mishahara, zaidi ya bilioni 33 zimeshalipwa na imekuwa ikifanya hivyo kila mara. Niwahakikishie tu watumishi wa umma, Serikali yenu inawajali, Serikali yenu inawathamini, tunatambua mchango wenu na kila mara tutaendelea kuangalia maslahi ya umma na kuyaboresha kwa kadri uwezo na bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tu katika haya madai mbalimbali, wako baadhi ya watumishi wamekuwa wakiwasilisha madai ambayo si sahihi na ndiyo maana tunasema uhakiki unachukua muda mrefu. Unachukua muda mefu kwa sababu huwezi ukalipa, hii ni fedha ya walipa kodi, ni lazima ujiridhishe kila hela unayoilipa ni hela ile ambayo kweli ndilo deni ambalo ni sahihi na ambalo limepitia katika michakato mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kulikuwa kuna hoja kwamba tuna Makatibu Tawala zaidi ya mmoja katika mkoa, tuna Wakurugenzi Watendaji zaidi ya mmoja...... hilo na tayari kila mmoja kwa nafasi yake ........na wale wengine wamepangiwa majukumu katika ofisi zao zinazowahusu.
(Hapa maneno mengine hayakusikika kutokana na hitilafu ya mtambo)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na niombe kwa wale ambao sijawataja waweze kuridhika na tutahakikisha kwamba majibu hayo mnayapata kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuhitimisha kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge mWendelee kuunga mkono hoja hii, ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora na taasisi zake kwa ufanisi katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.