Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiembesamaki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia Wizara ya Utawala Bora na TAMISEMI. Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa nikiwa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na utawala bora, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na sisi wote tukiwa ni mashahidi, kwa muda mfupi kwa kweli ameweza kutuletea maendeleo ambayo sisi wote tumestaajabu katika kipindi kifupi sana Mheshimiwa Rais Magufuli ameweza kufanya mambo ambayo yametupa imani na wananchi wamekuwa na imani kubwa sana juu ya Mheshimiwa Rais. Nikitolea mfano, kwa mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kuyafanya katika muda mfupi, kwanza ni katika kupiga vita rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nchi hii ya Tanzania ilikuwa inanuka kwa rushwa, hakuna mtu ambaye alikuwa haelewi, lakini leo ukienda Wizara yoyote au taasisi yoyote ya Serikali, unahudumiwa bila kuambiwa kutoa chochote, hii kwa kweli imetujengea heshima kubwa sana. Zamani ukienda kwenye nafasi yoyote nyeti, kama mfuko wako mdogo, huwezi kufanikiwa kupata haki yako. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha nidhamu katika taasisi za Serikali na katika Wizara za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwaondoa watumishi hewa. Kwa kweli pesa zetu mabilioni ya pesa yalikuwa yanaliwa na watu wajanja sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri kupitia Wizara yake ya Utawala Bora ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Kairuki, ni dada mmoja ambaye kwa kweli amepewa Wizara na ameweza kuimudu vizuri sana. Nampongeza sana dada yangu Mheshimiwa Kairuki. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuwaambia, anachofanya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, anafanya kwa ajili yetu sisi, kwa sababu mambo anayofanya sasa hivi katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, fikiria baada ya miaka mitano Tanzania itabadilika, na sisi tunataka kwenda mbele, hatutaki kurudi nyuma. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais amesisitiza kwamba maendeleo kwanza, Tanzania kwanza. Kwa hiyo, sisi Waheshimiwa Wabunge, bila kujali itikadi zetu za kisiasa, lazima tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekitil, mimi nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka mitano yatakuja mambo kubadilika Tanzania hii na tulishaanza kuona mabadiliko. Ameanza mambo ya reli kiwango cha standard gauge, ameshaanza kuleta ndege mbili, kuna ndege mbili nyingine zinakuja mwakani, mambo ya flyover bridge haya; Mheshimiwa Rais ameweza kufanya mambo chungu nzima! Sasa mnasema kwamba utawala, utawala gani mnaotaka nyie? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba tuwe wastahimilivu katika kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais anataka kuijenga Tanzania mpya. Mimi nazidi kumwombea Mungu ampe umri, ampe afya ili tupate maendeleo ambayo itakuwa siyo maendeleo yetu sisi bali ya vijukuu vyetu ambao ni Taifa letu la kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika Wizara ya TAMISEMI, kwanza nampongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kweli masuala ya elimu, leo Watanzania watoto wao wanakwenda kusoma shule bure. Mtoto wakati wa miaka ya nyuma alikuwa hawezi kwenda kusoma kwa sababu alikuwa hana ada. Leo Mheshimiwa Rais amesema kwamba watoto wote wasome bure na Mheshimiwa Rais kwa kupitia Wizara yake TAMISEMI, wamejitahidi sana kwamba leo asilimia 75 ya shule zetu zina madawati. Seventy five percent, hayo mengine twenty five percent, basi ma-desk yatakuja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda cha kuwaomba TAMISEMI, ni kwamba watupatie na walimu wazuri ili watoto wetu wawe na education bora. Hapa walipofika TAMISEMI kwanza niwapongeze sana na Inshallah Mwenyezi Mungu atawapa nguvu Mheshimiwa Simbachawene na Naibu wake ili kuona kwamba elimu na kwa sababu elimu ndio ufunguo wa maisha, sasa watoto wetu watakapopata elimu nzuri basi naamini na Taifa hili tutakuwa na watoto wenye vipaji.

Mheshimiwa Mwneyekiti, nikija kwenye masuala ya Jiji letu la Dar es Salaam, nataka kumwambia Mheshimiwa Simbachawene kwamba sasa Dar es Salaam unapokwenda mtaa wowote pale mjini kama mitaa ya Libya, Bibi Titi Mohamed, Samora ukienda wapi pamukuwa na ombaomba ambao sasa wameweka magodoro yao na usiku wanaweka vyandarua, wana lala kabisa, asubuhi wanaoga pale pale, kwa kweli mandhari ya Jiji la Dar es Salaam inapotea kabisa na kama huamini mimi nipo tayari kufuatana na wewe usiku nikakuonesha hali ilivyo Dar es Salaam. Wakati wa asubuhi inanuka kwa sababu pale pale wanamaliza haja zao. Mimi mwenyewe binafsi nimeshuhudia mtu asubuhi anafanya haja yake, anamwaga maji.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Simbachawene kupitia Jiji lako la Dar es Salaam naomba sana, itafika wakati Dar es Salaam patakuwa tena ni kama Bombay ya pili. Hali ni mbaya sana, mimi ninashangaa Jiji la Dar es Salaam, Manispaa ya Dar es Salaam wamekaa kimya, sijui hawaoni! Ni kitu cha ajabu sana. (Makofi)

Vilevile wenzetu ambao wanafanya biashara ya nyama choma, kuku choma na chips, usiku wanakuja wanavunjiwa meza, wanavunjiwa viti na wanachukuliwa na wanadaiwa rushwa. Hivi juzi wamechukuliwa wafanyabiashara wote, wamepelekwa pale Manispaa, wamedaiwa rushwa na wametoa na ushahidi upo.

Mheshimiwa Rais Magufuli anajitahidi kupiga vita rushwa lakini bado watu katika kudai rushwa. Kwa hiyo, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Simbachawebe hawa watu ambao wanawekeza usiku wapo tayari kulipa kama kuweka viti, meza wapo tayari kulipa na mimi nitakupa mfano mmoja wa Bangkok, na hivi karibuni nilikuwa huko. Kuna mitaa fulani ikifika saa 12.00 wanaruhusiwa kuchoma nyama, kuku, chipis na kuweka nguo mpaka usiku saa 6.00 usiku, lakini hawapigwi wala hawatozwi rushwa. Hawa wenzetu wa Dar es Salaam, baada ya saa 12.00 jioni wapo tayari kulipa hata shilingi 500,000 au 1,000,000 kwa mwezi, lakini kila unapoenda kudai kibali, hawapewi wanazungushwa na matokeo yake wanakuja kudaiwa rushwa. Mheshimiwa Simbachawene, hili vilevile wanaipaka Serikali yetu matope.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu inafanya kazi nzuri lakini kuna baadhi ya watu wanaiharibu sifa ya Serikali yetu kwa tamaa yao tu na ubinafsi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa Wizara ya TAMISEMI ni kuhusu hao wenzetu wanaopewa parking za magari, ni ruksa. Wanapewa kuanzia saa 2.00 asubuhi mpaka
12.00 jioni lakini utakuta mtu anamiliki parking saa 24, lakini ukimwambia muda hapa saa 12.00 jioni ondoa parking yako muda umekwisha, anakwambia hapana, mimi nimelipia. Hujalipia kwa saa 24. Mheshimiwa Simbachawene imekuwa ni matatizo ya parking Dar es Salaam ni sugu sana. Watu ikifika saa 12.00 jioni tunaomba uwaambie Manispaa waondoe kile kibao chake, kichukuliwe... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja Wizara zote mbili, Wizara ya Utawala Bora na TAMISEMI. Nakusuhuru sana kaka yangu Chenge.