Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kusimama hapa kuchangia kwenye Wizara hizi mbili; kwenye mwelekeo wa bajeti inayokuja mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Wizara ya TAMISEMI. Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye Wilaya 19 zilizoanzishwa hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Uvinza. Ninavyoongea, tangu Wilaya ya Uvinza ianzishwe, haina Hospitali ya Wilaya. Tunatambua kabisa kwamba Wizara ya TAMISEMI ni Wizara mtambuka, ndiyo inayosimamia masula yote ya Halmashauri zote nchini. Sasa namwomba sana Mheshimiwa
sana Waziri, akiungana na Naibu wake waone ni jinsi gani wanaweza kutupitishia maombi. Tumeleta barua ya maombi kwenye maombi maalum, shilingi bilioni mbili; tunaomba hizo shilingi bilioni mbili tupewe ili tuweze kujenga hospitali na tayari tumetenga eneo la ujenzi, ekari 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ukipitia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, ya mwelekeo ya mapato na matumizi ya bajeti ya 2017/2018, ukurasa wa 103 utaona kwamba kwenye Mfuko wa Pamoja wa Afya, Halmashauri ya Uvinza haijapangiwa hata shilingi moja. Tuna Halmashauri takriban tisa, lakini tuna Majimbo manane. Kati ya Majimbo hayo, ni Jimbo moja tu ndilo linaloongozwa na mwanamke.
Sasa ninaanza kupata shida na msemaji mmoja aliongea juzi ndugu yangu Mheshimiwa Chikambo kwamba Wizara inaongozwa na wanaume. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwanamke, yaani Halmashauri zote zitengewe pesa kwenye Mfuko wa Pamoja wa Afya, Halimashauri yangu ya Uvinza isitengewe hata thumni, kulikoni? Mheshimiwa Waziri nazungumzia kwenye pesa zile za nje za forex; sina hata thumni, nimejisikia vibaya sana. Nimeangalia kwenye ule ukurasa, nikanyong’onyea, nikasema kulikoni? Ila sina mashaka, Mheshimiwa Simbachawene ni jirani yangu, nadhani utaliangalia hili na utarekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye ukurasa huo huo kwenye pesa za lishe na ulinzi wa mtoto, sina hata thumni. Wakati Halmashauri yangu ya Mkoa wa Kigoma inapitisha bajeti, Hazina ilikubali kututengea pesa; nasi tuna watoto 86,388 ambao wapo chini ya umri wa miaka mitano. Sasa ninashangaa, Hazina wamekubali kutuwekea shilingi 86,388,000 lakini kwenye hiki kitabu hakuna hata shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana, kulikoni? Maana yake ukiona mwanamke amepita kwenye Jimbo, ujue alipambana kweli kweli, siyo mambo ya ki-sport sport! Hatukuwa na mambo ya ki-sport sport mpaka tukaingia hapa. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri unisaidie kama ambavyo Majimbo mengine yalivyopata pesa, basi nami naomba unifikirie. Utakapokuja kufanya majumuisho hapa, uniambie utanisaidiaje
kwenye huo Mfuko wa Pamoja wa Afya pamoja na lishe na ulinzi wa mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nizungumzie Kituo cha Afya cha Nguruka. Tarafa ya Nguruka ina Kata nne na hiki kituo kinahudumia wananchi zaidi ya 100,000 na kitu na wanahudumia vilevile Kata ya Usinge kutoka Wilaya ya Kaliua. Sasa tumekuwa tunaomba mara kwa mara kupewa pesa ya kuweza kukipanua hiki Kituo cha Afya ili kiweze kuwa na huduma zinazostahili sambamba na
kuongeza wodi ya wanaume na wodi ya wanawake. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aweze pia kutuangalia katika suala la Kituo chetu cha Afya cha Nguruka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia hayo, naomba pia nizungumzie Mfuko wa Barabara. Mfuko wa Barabara kwa bajeti hii tunayokwenda kumaliza tarehe 30 Juni, tuliidhinishiwa shilingi milioni 695, lakini hadi sasa tumepokea asilimia 45 tu. Sasa kwenye hii coming budget tunayotarajia ambayo itaanza tarehe 01 Julai, tumepitishiwa shilingi milioni 495 tu na sisi kwenye Jimbo letu, kwenye Halmashauri hii, hakuna barabara yoyote yenye lami. Mtandao wa barabara ambazo zina changarawe ni kilometa 44 tu na siyo zaidi ya hapo. Kwa hiyo, naomba hebu tuwe tunaangalia hizi Halmashauri mpya, tuwe tunazipa kipaumbele zaidi kuliko zile Halmashauri ambazo zimeanzishwa
miaka mingi. Niliona hilo nalo nilizungumzie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala la uanziswaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nguruka. Tumekuwa tunaleta barua kwenye Wizara hii ya TAMISEMI na huko nyuma tuliambiwa kwamba hakuna shida, Mamlaka ya Mji Mdogo inaweza ikaanzishwa, lakini changamoto ambayo tunayo ni nini? Kata ya Nguruka ina vijiji viwili; Kata ya Itebula ina vijiji viwili; Kata ya Mganza ina vijiji sita; na Kata ya Mteguanoti ina vijiji vine. Sasa unaangalia kwamba kama hatuwezi kuongeza, maana yake hizi Kata ni kubwa mno. Tunachoomba Wizara ya TAMISEMI mmesema hamna mpango wowote wa kuongeza Kata, wala vijiji, lakini kuna Majimbo mengine ni makubwa mno, lazima mfikirie namna ya kutuongezea kugawanya Kata na vijiji ambavyo ni vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Jimbo langu mimi lina square meters 10,178. Dada yangu Mheshimiwa Anne alikuwa anaongelea hapa, kwamba Same ina square meters 5,000, nikashtuka; kwangu ni 10,000. Kijiji kimoja mpaka ukimalize, unatakiwa ufanye ziara kwa siku mbili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri uone namna ya kutukubalia maombi yetu pale tutakapoyaleta ili tuweze kuongeza vijiji kwenye
Kata ya Nguruka, Kata ya Itebula ili uanzishwaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Nguruka utakapokuwa unaanza, basi tuweze kuwa na vijiji vya kutosha mamlaka hiyo iweze kuendeshwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie migogoro baina ya vijiji na hifadhi. Kwenye Kijiji changu cha Sibwesa na Kalilani wamekuwa wana mgogoro zaidi ya miaka 30 na Hifadhi ya Mahale, lakini cha kushangaza, tunatambua kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni alitoa tamko kwamba kila taasisi za Serikali zihakiki mipaka yao. Ninavyofahamu, unapotaka kufanya uhakiki wa mipaka, wewe kama ni Wizara fulani kwa mfano ya Maliasili, maana yake nazungumzia Hifadhi ya Mahale, lazima ushirikishe na Wizara ya TAMISEMI. Kwa sababu hivi vijiji
vimewekwa kwa mujibu wa sheria na aliyetangaza tangazo kabla ya kutangaza hivi vijiji ni Waziri Mkuu; ni Ofisi hiyo hiyo ya Waziri Mkuu. Sasa iweje leo Mkurugenzi wa Mahale anakwenda kuweka alama (beacons) kwamba hapa ndiyo sisi Mahale tunatakiwa mipaka yetu iishie; anaingilia mpaka zile GN za Serikali ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri mambo haya yakafanyika kwa mashirikiano. Nimewahi kuwa DC pale Arumeru, migogoro yote ya Arumeru tulikuwa tunafanya kwa ushirikishwaji. Unahusisha Wizara ya Ardhi, unahusisha Wizara ya TAMISEMI na kama kuna hifadhi, unahusisha pia na Wizara ya Maliasili. Sasa tatizo ambalo tunalo, tuna Wakuu wa Wilaya wengine ambao hawaelewi watatue matatizo ya wananchi kwa namna gani. Napenda kumuelimisha ana… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono, hoja japo m da ni mdogo, nilitaka niseme
zaidi ya hapo. Ahsante sana.