Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mendard Lutengano Kigola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze na kuipongeza Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano naamini kabisa iko makini sana; na tunaposema utawala bora maana yake ni kutimiza malengo ambayo uliwaahidi wananchi. Nakumbuka katika Mwaka wa Bajeti 2016/2017, naweza nikayakumbuka malengo ya Serikali 14 ambayo yamefanywa na Serikali na yametekelezeka tayari. Kwanza kabisa, lengo
la kwanza, katika ununuzi wa ndege, walisema watanunua ndege sita na sasa hivi kuna ndege mbili tayari ziko zinazunguka Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika viwanja vya ndege ambavyo vimefanyiwa upanuzi na Serikali; na usafiri wa anga sasa hivi kila kona wenzetu Watanzania wameanza kusafiri na naomba kutoa ombi kwamba ndege inayotoka Dar es Salaam kuja Dodoma ipite Iringa iende Mbeya ili na
sisi watu wa Iringa tukitoka Dodoma tuweze kupata usafiri wa ndege mpaka Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wengine wameanza kubeza hizi ndege; sisi wa Iringa tunahitaji ndege. Hata kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini tuna viwanja vidogo vitatu, wananchi wale wanataka ndege na wenyewe. Ukienda Ngwazi pale pana kiwanja cha ndege,
ukienda Luhunga pale kuna kiwanja kidogo cha ndege, ukienda Mgololo pale pana kiwanja kidogo cha ndege, tunahitaji ndege na sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, katika utekelezaji wa Serikali kuhusu elimu bure. Serikali ilisema itatoa elimu bure kwa watoto wa Watanzania wote na imefanya hivyo, hiyo ni hatua kubwa sana. Kama jambo zuri limefanyika lazima tulisifu. Hata kwa Mungu kama unaanza kupiga maombi kwa Mungu wako wewe humsifii Mungu huwezi kupata Baraka hata siku moja, hilo niwaambie kabisa. Kitu kizuri kimefanyika tuseme hiki kizuri kimefanyika, elimu bure tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili suala la elimu bure watu wana-mislead, elimu bure sio kwamba ni na kujenga madarasa na mambo mengine, elimu bure maana yake ni ile ada. Watoto kuanzia shule ya awali, shule ya msingi na sekondari wanasoma bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, tatizo kubwa la madawati limepungua kwa asilimia kubwa sana, hata kwenye jimbo langu nilikuwa na tatizo kubwa sana lakini sasa hivi madawati tunaweza tukasema kuna sehemu nyingine wana ziada ya madawati. Watoto walikuwa wanakaa chini sasa hivi wanakaa kwenye madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tukitaka uchumi wa Tanzania ukue ni kutengeneza miundombinu ikae vizuri. Nimeifurahia sana mipango ya Serikali. Kwa mfano kuimarisha usafiri wa reli ni suala la msingi sana. Barabara zilikuwa zinaharibika kwa sababu zinabeba mizigo mizito. Kwa mfano watu wanasafirisha mbao kutoka Iringa mpaka Dar es Salaam,
kutoka Iringa mpaka hapa Dodoma kwenye barabara hizi za kawaida, za lami, barabara zinaharibika; lakini mpango wa Serikali wa kusema utaimarisha usafiri wa reli ni mpango mzuri mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pale Mgololo kuna barabara ya reli imepita, namwomba Waziri wa Uchukuzi, akiangalie kile kituo cha Mgololo; mbao zitoke pale Mafinga ziende moja kwa moja kwenye kituo cha reli ili waweze kusafirisha kwa njia ya treni ili tusiharibu hizi barabara za lami, ziweze kukaa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ni la msingi sana; tumesema Serikali iimarishe vituo vya afya. Bahati nzuri sisi Wabunge tulipewa semina moja ambayo mimi pia nilihudhuria, ilinisikitisha sana. Inasemekana kwa siku moja akinamama 30 wanakufa kwa ajili ya tatizo la uzazi. Sasa ukichukua 30 ukizidisha mara siku 30 maana yake akinamama 900 wanakufa kwa mwezi mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika takwimu pia walisema watoto 180 wanakufa kwa siku moja, ambayo ni hatari. Sasa nataka niiombe Wizara ya TAMISEMI, suala ya kuimarisha vituo vya afya ni suala la msingi sana. Tukitaka kuepukana na hili tatizo la uzazi kwa akinamama lazima
tuhakikishe vituo vya afya kule vijijini vimekaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri, naishukuru Serikali, nilisikia wanagawa ambulance, ambulance kama mia ngapi zilikuja lakini bahati mbaya sana kwenye jimbo langu sikupata. Kwenye kile Kituo cha Mgololo kuna takriban kata tano zinazotegemea kituo cha afya kimoja lakini hakuna ambulance. Kwenye bajeti yetu ya Halmashauri tulitenga 500,000,000 ili tuweze kununua ambulance tatu, matokeo yake mwaka wa fedha unakwisha lakini zile ambulance hatujanunua.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maswali yangu ya nyuma nilikuwa nauliza kuhusiana na ambulance ya Mgololo na Serikali ilikuwa inaniahidi kwamba watanunua ile ambulance, wataipeleka pale kituo cha Mgololo lakini mpaka leo hawajapeleka. Nitaiomba Serikali kwenye hilo, ili
kuepukana na hili tatizo watupelekee ambulance pale. Tukifikia kwenye Bajeti ya Wizara ya Afya lazima tuiangalie vizuri, tuiongeze ili ikae vizuri tuepukane na matatizo ya zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine linahusiana na umeme. Bahati nzuri sana Mheshimwia Waziri alitoa hotuba nzuri sana na wana mpango mzuri sana; lakini tumewaahidi wananchi kwamba kila Kijiji kitapewa umeme na wananchi kule wamekaa standby. Niiombe Serikali, kwenye suala la umeme tumesema kila kitongoji, kijiji na kila kaya watapewa umeme. Tunategemea kwenye vijiji, hasa kwenye Jimbo langu, nina vijiji na kata nyingi sana hazijapata umeme; kwamba tutakapomaliza Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 vijiji vingi sana vitakuwa vimeshapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kutaja vijiji hapa ni vingi. Kuna kata karibu nane hazina umeme kabisa na ukizingatia Jimbo la Mufindi Kusini ndilo Jimbo linaloweza kuchangia kwenye pato la Taifa asilimia kubwa sana, lakini ukiangalia kwenye miundombinu ya umeme ni duni. Kwa
hiyo, naiomba Serikali kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kama Waziri alivyoahidi, kwamba mpango wa REA kwa mwaka huu wa fedha vijiji vyote vya Jimbo la Mufindi Kusini vitaweza kupewa umeme.
Mhesimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye upande wa barabara. Kuna barabara Serikali iliifanyia upembuzi yakinifu na ilishamaliza. Barabara kutoka Nyololo, Igowole mpaka. pale Mtwango. Upembuzi yakinifu ulishafanyika miaka miwili iyopita lakini sasa hivi hakuna kitu kinachoendelea na Serikali ilishaahidi kwamba itajenga barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale kijiografia mvua zinanyesha kila siku, kwa hiyo magari yanashindwa kusafirisha chai kule. Kuna viwanda ambavyo ni viwanda vikubwa katika East Africa. Ukisema Kiwanda cha Chai katika East Africa lazima uende pale Mufindi, lakini barabara ile ni tatizo na pato kubwa la Taifa linatoka katika kile kiwanda cha Chai Mufindi. Sasa naiomba Serikali, ile barabara ambayo
iliahidi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, basi iweze kutekeleza ahadi yake hiyo. Bahati nzuri sana hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliwekwa nina imani kabisa watamaliza kujenga ile barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho; niseme kwamba naipongeza Serikali, nasema ikaze mwendo na sisi Waheshimiwa Wabunge tuko nyuma yako ili tuweze kutekeleza ahadi tulizoahidi kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.