Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya niweze kusimama leo kuchangia kwenye Bajeti ya Ofisi ya Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mkanganyiko kwamba watu wanasema tusimtaje Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya TAMISEMI iko chini ya Rais, Ofisi ya Utawala Bora iko chini ya Rais. Wizara tunazozijadili leo zinafanya kazi chini ya Rais. Kwa hiyo,
kutomtaja Rais maana yake hatujadili kabisa hizi Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutuzuia tusiseme, tuishie kwenye kusifia, mimi Mbunge wa Jimbo la Mchinga wananchi hawakunituma nije kusifia hapa. Wananchi wamenituma nije kueleza kero zinazowakabili. Katiba yetu ya nchi imetoa mamlaka ya kazi za Bunge, sasa nashangaa
kama kuna mtu anakuja anasema nyie mnaponda tu. Tusifie! Aah, sisi tuliochaguliwa bwana hatusifii, tunakuja kueleza kero za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze suala la utawala wa sheria. Nchi yetu inafuata utaratibu; tuna Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Waziri Simbachawene, kuna Mamlaka za Serikali za Mitaa Halmashauri ya Wilaya, Vijiji; hizi Serikali nasi tuliamua kutumia mfumo wa D by D, lakini leo vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri zetu tumevihamisha tumepeleka Serikali Kuu. Property Tax ambayo kwenye taarifa
yako mwenyewe umeeleza kwamba haijakusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, makadirio ilikuwa zikusanywe shilingi bilioni 29, zimekusanywa shilingi bilioni nne; nami naamini itakuwa sijui Kinondoni tu. Haijakusanywa kwa sababu hizi shughuli zinahitaji zifanywe na Halmashauri wenyewe. Tunapoteza mapato mengi, mmejilimbikizia kila kitu mmepeleka TRA, mwisho wa siku Halmashauri zetu zitashindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa tumeamua kufuata mfumo huu wa D by D, hizi Serikali ni Serikali zilizopo kwa mujibu wa Katiba, tuzipe mamlaka zikusanye mapato zenyewe, hii Property Tax ni muhimu sana. Jana nilikuwa nafuatilia, nilikuwa najaribu
kuangalia kusoma mifumo ya nchi mbalimbali. Nimeangalia India, Thailand na nchi nyingine ambazo tunafanana nazo.
Hakuna nchi ambayo imechukua Property tax kwenye Halmashauri inapeleka kwenye Central Government, ni sisi tu na sijui kwa malengo gani?
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba sana hili mliangalie. Isiwe kila mpango unaoletwa na Waziri wa Fedha iwe unau-copy na kuu-paste na kuuchukua, mwisho wa siku wewe ndio utalaumiwa. Halmashauri zikifa, wewe ndio utabeba huu msala. Mheshimiwa Mpango ataendelea na
kazi yake ya kukusanya mapato TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka niliunganishie hapo hapo, kumekuwa na tabia isiyoridhisha ya Wakuu wa Wilaya kuziondoa Madarakani Serikali za Vijiji. Imefikia hatua leo Serikali za Vijiji wale Wenyeviti wakisikia Mkuu wa Wilaya anakuja, hawaendi kwenye
Mkutano, kwa sababu wanajua wakienda, wanatumbuliwa. Sasa tunataka tujue ni sheria ipi inampa Mamlaka Mkuu wa Wilaya kuondoa Serikali halali ya Kijiji iliyochaguliwa na wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mifano mizuri mingine hapa Dodoma. Mkuu wa Wilaya Dodoma katangaza tu, Mwenyekiti hapa ondoka! Kwa hiyo, tunahitaji ufafanuzi; haya ni maagizo ya Mheshimiwa Rais? Kwa sababu hizi Wizara ziko chini ya Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la kuajiri Watumishi wa Idara ya Afya. Kwenye Jimbo langu zipo zahanati nne, zimejengwa, zimekamilika. Hazijafunguliwa kwa sababu hazina wahudumu wa afya. Kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Rais alikuja mwezi wa Tatu Lindi, alisimama Mchinga, akaelezwa na wananchi kwamba kero yetu kubwa hapa ni wahudumu wa afya. Mheshimiwa Rais akamwachia
lile suala Mganga Mkuu wa Mkoa, akamwambia shughulikia hilo. Mganga Mkuu wa Mkoa anawatoa wapi? Kila tukiangalia kwenye Halmashauri yetu, hakuna mtu ambaye anaweza kutoka kituo kimoja kwenda kwenye kituo kingine, kwa sababu hata hivyo vituo vyenyewe vina uhaba mkubwa wa watumishi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri, hili alichukulie kwa uzito wake. Tunahitaji Watumishi wa Idara wa Afya waende wakahudumie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la TASAF. Nashukuru Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba upo mpango wa wa kuongeza vijiji vingine. Jambo hili litatusaidia sana. TASAF sasa hivi imekuwa hata kwetu wanasiasa siasa yetu imekuwa ngumu. Kwa mfano, mimi Jimbo langu lina Tarafa nne. Katika Jimbo lenye Tarafa nne, Tarafa mbili zinanufaika, Tarafa mbili hazinufaiki, inatuwia shida na wananchi hawajui; wanachofikiri wao ni kwamba wewe ndio Mbunge, unaamua kwamba hapa wapate hapa wasipate.
Kwa hiyo, naomba sana mtusaidie, vile vijiji ambavyo havijapata hii miradi ya TASAF pelekeni na kama inashindikana, basi bora tuondoke wote tukose wote, kwa sababu haileti maana kwamba wengine wanapata; wana sifa zile zile na wengine wanakosa. Nashauri sana Mheshimiwa
Waziri hili alichukulie very seriously kwa sababu ni suala la kisiasa na linatuharibia siasa huko na sisi wote ni wanasiasa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni muhimu nataka nilizungumzie ni suala la utendaji mbovu usioridhisha wa Wakurugenzi. Watu wamesema hapa, lakini inaonekana kama masihara. Jamani sisi wenzenu, nafikiri hata mwenzangu Mheshimiwa Nape wa Halmashauri moja naye anawezakuja kusema hapa. Wenzenu tuna shida. Tulikuwa tunavumilia lakini sasa tunasema, wenzenu tuna shida. Yaani unamtoa mtu, sijui alikuwepo Afisa nani sijui kwenye Kata huko unakuja kumfanya Mkurugenzi katika Halmashauri kubwa kama ilivyo Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri yetu ni kubwa kuliko Halmashauri zote za Mkoa wa Lindi, zina eneo kubwa!
Unatuletea mtu ambaye ukisoma hivi vitabu, katika Mkoa mzima wa Lindi, internal collection iliyo chini kuliko zote ni Halmashauri yetu ya Wilaya ya Lindi. Ndiyo Halmashauri yenye population kubwa na Halmashauri ambayo ni kubwa. Tatizo ni utendaji usioridhisha wa hao watu mliowateua mkatuletea. Kwa hiyo, tunaomba sana, kama kuna haja ya kubadilisha, tubadilishieni, lakini kama hamna haja ya kufanya hivyo, tunaomba basi muwape mafunzo, kwa sababu wanatuletea umaskini; badala ya kwenda mbele sasa, tunarudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, nilimwandikia jana Mheshimiwa Simbachawene, nami namwamini kwamba hilo, nililomwandikia atalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Walimu, nilipoona taarifa kwamba kumeajiriwa Walimu nilipata faraja sana hususan Walimu wa sayansi. Katika Jimbo langu kuna shule za sekondari saba, nimepata Walimu katika shule za sekondari mbili; Shule ya Mvuleni na Shule ya Rutamu; shule ambazo zina matatizo makubwa zimekosa Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu shule yangu au Halmashauri yetu, Mkoa wa Lindi mnajua matokeo ya mtihani uliopita yalikuwa mabaya; tumekuwa kwenye tatu bora na hatupendi kuwa hivyo. Katika jambo ambalo linatuuma ni sisi kuwa wa mwisho na ni Mkoa uliotoa Waziri Mkuu; lakini moja ya sababu ambayo imepelekea Mkoa wetu kuwa katika kiwango cha mwisho cha ufaulu ni kwa sababu ya idadi ndogo ya Walimu.
Waheshimiwa Mawaziri wanajua historia ya Lindi, hili halifichiki. Zamani watu walikuwa wanagoma kuja kule. Siku hizi wanakuja kwa sababu kuna mambo mazuri; kuna miradi ya gesi, korosho ziko juu, kila kitu kipo. Kwa hiyo, waleteni, hawagomi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilipoona kwamba mmetangaza ajira, nikajua mtatufanyia affirmative action kwa sababu mkoa wetu uko chini, tunahitaji mtusaidie. Kama mtaajiri tena, naomba sana, shule zilizopo katika eneo langu la Jimbo la Mchinga zina uhaba mkubwa
wa Walimu. Shule ya Sekondari Mchinga ambayo ni kubwa, inafaulisha kidogo wastani, lakini ina uhaba wa Walimu wa Sayansi; Shule ya Sekondari ya Mvuleni nimepelekewa mmoja, mahitaji ilikuwa ni Walimu watano; Milola na shule nyingine zote zina uhaba mkubwa wa Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.