Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora. Kwanza kabisa nawapongeza kwa kuwasilisha hotuba nzuri na kuwasilisha mpango wa bajeti mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia siyo vibaya na ni muhimu tukaweza kutoa maboresho pale ambapo panaonekana panahitaji kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na eneo la kujenga uwezo kwa maana ya mafunzo. Nimemsikia kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene namna alivyoliweka; tunaelewa mlipotoka, tunaelewa maana yake, lakini nataka niseme, mafunzo ya kujenga uwezo ni jambo muhimu sana. Hata ukiwa umesoma namna gani, una Ph.D, umetoka umewiva, una experience nzuri kabisa kwenye eneo lako la kazi, lakini kujifunza ni dhana endelevu. Utajifunza mpaka siku ya kwenda kaburini.
Sasa tunaposema kwenye baadhi ya maeneo kwamba tumechagua watu au tumeteua watu ambao wamekwishawiva, nafikiri pale kidogo tunahitaji tulitafakari upya. Nashauri, jambo hili la wenzetu Wazungu, wanasema “learning is a continuous process.” Mpaka siku ya mwisho
utaendelea kujifunza tu, hautafika mahali ukasema wewe umekamilisha, unajua kila kitu, haiwezekani. Ni lazima tuendelee kujifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napendekeza kwamba Wizara, kwa maana ya Serikali, bajeti ya kujenga uwezo iendelee kuwepo na izingatiwe sana. Taifa ambalo halijifunzi, hili litakuwa ni Taifa la namna gani? Kweli mtu anasema nimeshamaliza kujua! Haiwezekani. Ndiyo maana wakati mwingine tunakutana na changamoto za makosa madogo madogo ambayo yangeweza kuepukika kupitia capacity building.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize sana, nimeona kuna bajeti kidogo kwa wale ambao wengine wanawaita maarufu kama wateule kwa maana DED, DC, DAS na Wakuu wa Idara wengine, lakini nataka niseme pia hii capacity building isiishie kwa hawa wateule peke yake,
hata sisi Wabunge, lakini wale Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambao toka wameingia, sehemu kubwa mfano kwa Wenyeviti hakuna chochote walichojifunza. Matokeo yake unajikuta wako tu kule hawajui hata wanakwenda vipi pamoja na kwamba waliomba zile nafasi
wakiamini wana uwezo na zile nafasi lakini kwa kweli wanahitaji kufanyiwa mafunzo ya kujenga uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize kwamba katika bajeti, hili ni jambo la msingi sana na kama tunakwenda na falsafa ya kwamba hakuna tena; kulikuwa na ile dhana ya Semina Elekezi. Naishauri tu Serikali yetu, naamini Serikali yetu ni sikivu, jambo hili tutakuwa tunakwenda kidogo kwa kimakosa. Tujaribu kulitazama upya, tutenge bajeti kwa ajili ya shughuli hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nitapenda nichangie, kumejitokeza kule kwenye Halmashauri zetu ukinzani kati ya maelekezo kutoka Serikali Kuu na vipaumbele kutoka kwa wananchi. Sisi tunaokwenda kwa wananchi tunakutana na changamoto. Tunataka kuzitatua
changamoto kutokana na vipaumbele ambavyo tumefikuta kwa wananchi, lakini mkikaa kwenye vikao vile pale Halmashauri wakati mwingine tayari kuna maelekezo, safari hii kipaumbele ni moja, mbili, tatu, huku kwingine hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hata hii Serikali tumeiweka kwa ajili ya kuhudumia wale wananchi. Tunapoweka one size fits all kwamba katika ngazi ya Serikali, sawa. Kulikuwa na jambo ambalo limeonekana safari hii tufanye operesheni hii twende namna hiyo, lakini vile vipaumbele ambavyo tunakwenda kuviibua kwa wananchi, tusiviache. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu labda kuwe na maelekezo kwamba panapotokea mambo ya vipaumbele na maelekezo kabisa ya labda miongozo, maana yake hii miongozo ndiyo Watendaji wengi wanafanya nayo kazi hiyo, ili kusiwe na migongano sana katika hilo. Mwenyekiti, Mbunge na Madiwani wengine wanapambana na vipaumbele vilivyoibuliwa huko na wananchi; lakini Watendaji wa Halmashauri, wanapambana na melekezo. Mwisho wa siku hatutafika. Naomba sana Mheshimiwa Waziri hilo tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, napenda kuongelea kuhusiana na suala zima la huduma kwa wazee kwa maana ya kule hospitali. Niko sasa kwenye mpango wa afya kwa maana ya hospitali. Sera ipo vizuri na mipango ni mizuri. Nataka niwaambie, utekelezaji wake kule hospitali hebu tengenezeni mkakati au mechanisms za kuhakikisha unatekelezwa kadri mnavyopanga, kwa sababu utekelezaji kule haupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie kama kwangu kule Hospitali ya Mji wa Kondoa, ukiuliza habari ya Dirisha la Wazee, halipo. Ukiwauliza, sera hii ipo vipi? Wengine hawaelewi. Kwa hiyo, hebu tuhakikishe kuna mikakati mahususi ya kuona hii mipango tunayoiweka katika ngazi ya kitaifa inatekelezwa mpaka kule chini. Tuwe na mechanisms za kusimamia utekelezaji ambao utakuwa makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vitambulisho; hao wazee wa kuanzia miaka 60 wapate vitambulisho ili waweze kuhudumiwa. Siyo tena kila wakati wakija wapite kwa Mtendaji wa Kata waandikiwe barua. Hiyo haijakaa sawa! Ni usumbufu ambao unapunguza ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa hapo hapo kwenye suala la afya, napenda niongelee suala la dawa. Malalamiko juu ya dawa ni mengi kweli kweli. Hapa tunasikia kwamba hela zimepelekwa nyingi kwa ajili ya dawa, lakini kule unakuta hakuna dawa. Tatizo liko wapi hapa? Nataka
nishauri Serikali tufanye utaratibu wa kuweka procurement experts kule kwenye Hospitali zetu ili waweze kujua supply chain ya dawa inakwenda vipi? Inapofika wakati mtu anasema matumizi yake ya dawa ni shilingi milioni 15 kwa wiki, huku analetewa hela tofauti, au ana-order kila baada ya quarter moja wakati dawa zinakatika katikati hapo ina maana hatuna mpango mzuri wa dawa. Tuweke taratibu
ambao kutakuwa na minimum reorder level, ikifika kiasi fulani wana order tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuwa na experts wa procurement kule kwenye hospitali zetu, tutaendelea kusumbuka na haya malalamiko yatakuwepo na hela zipo, zimepelekwa. Ukiangalia kwenye upande hela, zipo dawa hakuna. Naomba na hilo nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye upande huo huo wa afya, kuna baadhi ya hospitali zinakutana na changamoto kubwa sana kama ile hospitali ya Mji, Kondoa. Inahudumia Halmashauri tatu Kondoa Mji, Kondoa Wilaya, Chemba, lakini pia na sasa hivi barabara kubwa ya lami
imepita na dharura zinaongezeka, lakini fungu kubwa la bajeti linakwenda kwa ajili ya Hospitali ya Mji; haitatosha. Hebu tuangalie kama pale tunaweza kuboresha kufikiria mpaka hao wengine watakapojenga hospitali zao za wilaya, lakini kwa sasa hivi wote wanahudumiwa kupitia Hospitali ya Mji, Kondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, niguse kidogo tu kwenye upande wa TASAF. Napongeza mpango huu, ni mzuri na malengo yake yana tija sana, lakini nataka niwaambie, utelezaji wake unahitaji mkakati wa kuusimamia ili ukidhi malengo. Kwa sasa hivi kuna upungufu mkubwa na kunatokea malalamiko mengi…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.