Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya TAMISEMI. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanafanya kwenye Taifa letu. Niseme kwamba walikuja kwenye Mkoa wangu wa Songwe na hakika wameacha alama ambayo
haiwezi kufutika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, moja kwa moja naomba nielekeza mchango wangu katika kuchangia masuala ya elimu. Nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wake Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza
kusimamia vizuri Sheria ya Haki ya Mtoto ya mwaka 2009 inayohusu haki ya mtoto kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake yamekuwa ni makubwa kwa sababu tumeshuhudia kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi idadi ya wanafunzi ambao wameandikishwa darasa la kwanza mpaka kidato cha nne imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ukisoma hotuba
ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amesema kwamba katika mwaka huu 2017 zaidi ya wanafunzi 300,000 wamedahiliwa ukilinganisha na idadi ya wanafunzi ambayo walidahiliwa kwa mwaka jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali hii kwa sababu unaweza kujiuliza kwamba endapo hawa watoto wasingepata hiyo haki yao ya msingi ya kupata elimu bure wangekuwa wapi. Sera hii imesaidia sana kwani vilevile imepunguza matabaka katika jamii yetu kwamba kwa sasa hivi mzazi ambaye hana uwezo na mwenye uwezo watoto wao wanakuwa na haki ya kupata elimu, lakini vilevile imepunguza mimba za utotoni hususani kwa mabinti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi huwa nashangaa sana napoona Mbunge katika Bunge hili anasimama na kuponda Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba imeshindwa kusimamia elimu bure. Hilo jambo si kweli na uzuri ukiangalia hao watu ambao kila siku wamekuwa ni watu wa kuponda wao wenyewe mpaka leo hii wameshindwa kujenga jengo moja la makao makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kusitisha sana, kama umeshindwa kujenga Ofisi ya Makao Makuu utaweza kutoa elimu bure? Ni kitu ambacho hakiwezekani. Kwa hiyo, niseme kwamba Wabunge tujifunze kusimamia ukweli na tujifunze kusifia pale ambapo Serikali inafanya vizuri. Vilevile tujifunze kushukuru hata kwa kidogo ambacho Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi mimi kama Mbunge nilitegemea mtu anapokuja kuponda Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuona hata kwenye zile Halmashauri ambazo wao wanaziongoza wangefanya vizuri, lakini matokeo yake sioni jipya lolote kwenye hizo Halmashauri. Hata ukiangalia kwenye suala la madawati, wamesubiri mpaka Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefikiria namna gani ya kuweza kuhakikisha kwamba wanafunzi wa nchi hii wanapata madawati. Ni vema Watanzania wakaelewa kwamba hizi ni porojo tu ambazo
tumeshazizoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naomba nielekeze mchango wangu kwa masuala mbalimbali ya elimu na wote tunafahamu kwamba kinachosababisha mwanafunzi akafeli ni mazingira magumu ya mwalimu na wala sio mazingira magumu ya mwanafunzi.
Nasema hivyo kwa sababu kama mwalimu akirekebishiwa mazingira yake na akipewa motisha ya kutosha mwanafunzi hata kama anatoka kwenye mazingira magumu lakini akikutana na mwalimu ambaye ameandaliwa vizuri ni rahisi sana kwa mwanafunzi huyo kufanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo limejidhihirisha hata katika hotuba hii ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ukurasa wa 31 ambapo amezunguzia motisha kwa Walimu Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata. Hotuba hii imesema kwamba katika mwaka wa fedha 2016 kuanzia Julai mpaka Machi, 2017, Serikali imeanza kupeleka fedha kwa ajili ya kutoa motisha kwa Walimu Wakuu wa Shule. Mpaka sasa
Serikali imepeleka shilingi bilioni 25.7 kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi lakini imepeleka shilingi bilioni 7.20 kwa ajili ya walimu wa sekondari lakini imepeleka shilingi bilioni 7.79 kwa ajili ya Waratibu wa Elimu Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha kwamba tunaboresha viwango vyetu vya elimu. Hata hivyo, kwa utaratibu huo, ni kwamba sasa kila Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari anapata kiasi cha shilingi 250,000 kwa kila mwezi lakini vilevile Mratibu pia anapata shikingi 250,000 na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi anapata motisha ya shilingi 200,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mafanikio makubwa, lakini nataka kushauri machache. Nimejaribu kusoma sana hiyo hotuba ya TAMISEMI lakini sijaona mahali ambapo Serikali imezungumzia kuwapa motisha wale walimu ambao ni wa hali ya chini, walimu ambao ni wa kawaida.
Sote tunafahamu kwamba unapozungumzia Idara ya Mwalimu Mkuu, Mwalimu Mkuu ni taasisi. Unapozungumzia Mwalimu Mkuu, unazungumzia mwalimu wa taaluma, mwalimu wa nidhamu, mwalimu wa michezo pamoja na mambo mengine. Serikali kupeleka fedha hizi moja kwa moja kwa Mwalimu Mkuu peke yake, mimi kama Mbunge limenipa shida kidogo. Ni vema Serikali ikaangalia namna nzuri
ambayo inaweza kuhakikisha kwamba hata wale walimu wengine wa masomo ya kawaida wanapata hii motisha ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunatambua kwamba Walimu Wakuu hawa ndiyo ambao hata semina mbalimbali ambazo huwa zinafanyika zinawalenga wao moja kwa moja.
Waratibu wa shule, semina hizi zinawalenga moja kwa moja.Hata ukija kwenye masuala ya nyumba za walimu, wanufaika wa kwanza ni hao Walimu Wakuu wa Shule, lakini wale walimu ambao wanafundisha masomo ya kawaida, walimu ambao kimsingi wao ndiyo wanabeba jukumu kubwa la kuhakikisha wanaboresha mifumo ya elimu, ndiyo wanaohangaika na wanafunzi asubuhi mpaka jioni, naona kama Serikali imewasahau kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ushauri wangu kwa Serikali kwamba iweze kuangalia suala hili.
Afadhali hii fedha ikapelekwa katika shughuli za uendeshaji wa ofisi. Kwa kupeleka fedha hiyo kwenye uendeshaji walimu wote wataweza kunufaika. Vilevile tunatambua kwamba walimu wana changamoto ambazo zinafanana, fedha hii ikipelekwa katika shughuli za ofisi naamini kwamba walimu wote pamoja na Walimu Wakuu wataweza kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ulikuwa ni huo, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Simbachawene atakapokuja kutoa maelezo aniambie ni kitu gani ambacho wao wamekitumia
katika kuona kwamba motisha hii ipelekwe kwa Walimu Wakuu wa shule peke yao.