Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi na uwajibikaji mzuri na kila Mbunge ndani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakuamini kwa asilimia mia kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia maeneo machache sana katika bajeti hii na kwanza, ni suala la maji.
Ndani ya Mji wa Sumbawanga Mjini tuna mradi mkubwa sana wa maji ambao napenda sana kwa niaba ya wananchi niwashukuruni sana kwa mradi ule. Sumbawanga sio mji peke yake pale mjini, Sumbawanga imezungukwa na vijiji vingi sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mliangalie hili, mtusaidie kupata fedha za kuwezesha miradi ile midogo midogo ili wananchi wanaozunguka Mji wa Sumbawanga waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni la wafanyabiashara. Nataka kuongelea sana wafanyabiashara hususan wa Jimbo la Sumbawanga Mjini wengi ni wakandarasi na wengi wamefanya kazi ndani ya Seri kali, lakini ni muda mrefu sana hawajapata malipo yao. Hao watu
wanaumia sana kwa sababu wanadaiwa kodi, kwenye mabenki na kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo linanishangaza Mheshimiwa Waziri Mkuu tumeunda kamati kila Mkoa ya kudai madeni ya wafanyabiashara ambao hawajalipa kodi. Kamati hiyo wameandika barua sehemu mbalimbali pamoja na kuzuia fedha ambazo wakandarasi
wamefanyia kazi Manispaa au taasisi nyingine, wakizuia fedha zile zote hawa watu wanakwama. Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu hili suala la kamati ambazo mmeziunda mikoani ziongozwe na watu wa TRA kwa sababu wao ni wataalam na wamesomea kazi hiyo. Nilikuwa nataka
nizungumzie hili ili mliangalie kwa uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo, wameongea Wabunge wengi na jana nimekusikiliza ukiongea na hawa mawakala wa pembejeo na umeahidi kwamba ifikapo tarehe 26 at least wachache watakuwa wameshaanza kulipwa wale ambao wamehakikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linaumiza sana, watu hawa wamekopa kwenye mabenki na watu hawa kama mnakumbuka, nataka niweke kumbukumbu sawa wafanyabiashara au mawakala wakubwa walikataa kuikopesha Serikali. Wafanyabiashara wadogo wadogo hao
wakaenda kukopa fedha benki wakaenda ku-supply pembejeo na bahati nzuri tukapita kwenye uchaguzi vizuri sana, lakini baada ya uchaguzi kupita hawa watu hatujawakumbuka.
Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi wana imani kubwa sana na Serikali hii, liangalieni hili kwa jicho lingine watu wanaumia sana, watu wamekufa, watu wana presha na wengine wamejinyonga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni la kusikitisha, mwaka jana kwenye bajeti wakati tunapitisha hapa masuala ya pembejeo na kutoa ruzuku kwenye mbolea tukaichagua TFC iwe mwakilishi wetu. TFC ndiyo wamekuwa walanguzi wakubwa. Mheshimiwa Zitto amechangia hapa amesema umtume CAG, nikuombe kabla hujamtuma CAG msimamishe huyu Mkurugenzi wa TFC ana miaka 20 yupo pale, ana kampuni binafsi ya kwake. Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana kabla hujamtuma CAG kwenda kuhakiki au kuchunguza, kwanza huyu Mkurugenzi wa TFC mumsimamishe kazi. Jana mmemsimamisha mmoja, lakini huyu ni wa pili ili akae pembeni uchunguzi ufanyike. Nikuombe sana na naamini hili unalisikia ulichukulie kwa uzito wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni uwanja wa ndege. Uwanja wa ndege tumepata bajeti, tumeshatafuta mwekezaji, uwanja wa ndege utajengwa ndani ya Mji wa Sumbawanga Mjini, shida kubwa nayoiona ni wale wananchi wanaouzunguka uwanja wa ndege. Wale wananchi
wanaozunguka uwanja ule walifanyiwa tathmini miaka sita au saba iliyopita, gharama za ujenzi zimeongezeka na gharama za viwanja zimeongezeka. Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Simbachawene yuko hapa kwa sababu wanaotakiwa kuwalipa fidia sio Idara ya Ujenzi, hapana, wanotakiwa kuwalipa fidia wananchi ni sisi TAMISEMI kupitia Manispaa. Naomba tufanye tathmini upya kulingana
na wakati uliopo. Nafikiri hili Mheshimiwa utakuwa umelichukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni kuhusiana na umeme. Sumbawanga Mjini tumebahatika tuna umeme na hatuna mgao wowote lakini Sumbawanga imezungukwa na vijiji mbalimbali. Kwa bahati nzuri vijiji vingine vyote vimepata umeme tatizo kubwa ambalo naliona na nilishamwambia Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini na ameahidi kunisaidia ni vijiji ambavyo vinatoka nje ya barabara kilometa
tano kutoka barabarani, wale watu hawakubahatika kupata umeme. Hata hivyo, kwenye REA III nimeona baadhi ya vijiji vipo na niishukuru sana Serikali katika hilo. Niombe tu Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini naye aje azindue mradi huo wa REA III ndani ya Jimbo la Sumbawanga Mjini.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuongelea kuhusiana na minara ya simu. Minara hii ya simu ni michache sana. Yapo baadhi ya maeneo hayana kabisa network.
Niwaombe Wizara inayohusika na jambo hili lichukulie kwa uangalifu mkubwa na kwa nguvu kubwa kuhakikisha sasa Tanzania nzima inafikika na Tanzania nzima mawasiliano yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hili hili ni kuomba tu Serikali iwekeze TTCL, iache maeneo mengine iongeze nguvu TTCL ili na yenyewe iwe kama kampuni nyingine tulizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mengi ya kuongea lakini mengine nimeamua kuyaacha kwa sababu maalum. Nimalizie tu na suala la Bunge Sport Club.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ulikua kocha wetu. Kwenye bajeti ya mwaka huu tumeona mmetujali kidogo lakini ikumbukwe sisi tuna ugeni mwaka huu kwa sababu sisi ni wenyeji wa mashindano hayo.
Mheshimiwa Mwenyeki, nikuombe sana bajeti tuliyonayo japokuwa mmetuongeza haitutoshi kulingana na ugeni mkubwa ambao tutakuwa tumeupokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama taifa tusiingie aibu. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu uliangalie hili kwa sababu wewe ulikuwa kocha wetu.
Mashindano yakianza tutakuomba rasmi uombe likizo kidogo uwe kocha ili tuweze kuchukua kikombe kwa sababu kidogo tumeshuka kiwango baada ya wewe kutoka ndani ya mashindano haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba kuna mengine nimeyaacha lakini kuna kitu ambacho kinaniuma lazima nikiseme. Mimi ni miongoni mwa watu waliotishwa tena mimi sikutishwa kwa maneno nimemuona yeye mwenyewe, nimekutana naye uso kwa uso vis a vis,
akiniambia kwamba Wabunge mmezidi unafiki na baya zaidi maneno haya ameyatamka mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Alisema hivi; “Wabunge mmezidi unafiki na nitadeal na nyie nikianza na wewe.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo Dar es Salaam sikanyagi na naiogopa yaani nilikuwa nimei-miss mno lakini baada ya kutishwa nimeogopa inabidi nikae Dodoma na Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niliarifu Bunge na familia yangu ijue kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam miongoni mwa watu wanaowatisha watu ikiwa ni pamoja na nini. Mengine mabaya siyasemi wala mazuri yake siyasemi nasemea hili kwa usalama wa nafsi yangu.
Najua yapo mazuri aliyoyafanya na yapo mabaya
aliyoyafanya, lakini mimi naomba niseme hilo moja tu
kwamba ni bora tukaliangalia kwa makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo tayari kuhojiwa, nipo tayari kuja kusema na nitatoa ushahidi kwa sababu nilikuwa kwenye hoteli inaitwa Colosseum, niliitwa mbele ya Mkuu wa Wilaya na akanitisha. Sasa mimi sisemi mengi, naomba hili niseme kulitaarifu Bunge kwamba na mimi ni miongoni mwa watu ambao tunatafutwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja.