Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Magufuli, lakini kwa namna ya kipekee, naomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake. Pia niwapongeze ndugu yangu Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kuwawezesha wananchi kiuchumi. Katika kampeni yetu ya uchaguzi ya mwaka 2015, Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliahidi kupeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji na kwenye kila Serikali ya Mtaa. Huu ni mwaka wa pili sasa toka tulipotoa ahadi ile. Ni vyema tukatekeleza ile ahadi. Tumebakia na mwaka mmoja tu wa kufanya kazi, mwaka 2018, 2019 tutaenda kwenye uchaguzi, tusipotimiza ahadi ambazo tumeziahidi wenyewe itakuwa vigumu sana mwaka 2019 kuomba kura hasa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakuomba, kupitia kwenye Serikali yetu ya Chama chetu cha Mapinduzi tutekeleze ahadi hii muhimu kwa sababu wananchi waliokuwa wengi kule vijijini na kule kwenye Serikali zetu za mtaa walikuwa wanategemea wapate shilingi milioni 50 hizi kusudi ziweze kuwatoa kwenye stage moja kwenda kwenye stage nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kuchangia ni suala la kilimo. Watanzania kati ya 67% mpaka 70% wameajiriwa katika eneo hili. Tumekusudia kwenda kwenye uchumi wa viwanda, lakini hawa wananchi ambao wameajiriwa kwenye eneo hili hatuwapi facilities za kutosha. Ukiangalia pembejeo sasa hivi ni ghali sana kuliko siku za nyuma. Kwa hiyo, ule uchumi wa viwanda ambao tumekusudia kwenda utakuwa mgumu sana kwa sababu malighafi ambazo tumekusudia kuzipata hatutazipata kwa sababu wakulima hawa watakuwa hawana uwezo wa kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu aliangalie sana hili eneo la pembejeo hasa mbolea kwa wakulima wetu zisiendelee kupanda bei. Mheshimiwa Waziri Mwigulu kipindi kilichopita alituahidi kwamba mbolea itauzwa bei rahisi, itauzwa kama
soda, lakini haya yaliyokuwa tumeahidiwa hayafanyiki na hatuyaoni. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iliangalie sana eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili hili la kilimo Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna hawa wenzetu mawakala wa pembejeo ambao wanaidai Serikali takribani shilingi bilioni 68. Huu ni mwaka wa nne wanadai hela zao na hawajalipwa mpaka leo. Kuna baadhi ya watu wameshaanza kuuziwa nyumba zao na wengine wanakufa. Kwa hiyo, tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu atengeneze utaratibu wa kuhakikisha hawa watu wanaodaiwa hela zao katika maeneo haya wanalipwa baada ya kuwa wamehakikiwa vizuri. Kuendelea kuwaacha na madeni, watakufa na hali zao zitaendelea kuwa mbaya. Serikali yetu ni sikivu, nina uhakika hawa watu watalipwa hela zao haraka iwezekanavyo baada ya uhakiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuchangia ni suala la maji. Maji ni tatizo kubwa na kule kwenye jimbo langu kuna tatizo kubwa sana la maji. Cha kusikitisha ni kwamba tatizo hili limekuwa kubwa na linaendelea kuwa kubwa siku baada ya siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Mwaka jana katika mambo mengi ambayo sisi Wabunge tuliishauri Serikali kwenye bajeti iliyopita hayakutekelezwa likiwepo la kuongeza tozo ya kutoka shilingi 50 kwenda shilingi 100. Tulikuwa na uhakika kama tungeweza kuongeza tozo kwenye eneo hili Mfuko wa Maji ungeendelea kuwa mkubwa na hatimaye watu wengi wangepata huduma ya maji katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kupitia Waziri Mkuu, muwe mnatusikiliza na sisi Wabunge. Hakuna Mbunge ambaye anataka kero ya maji iwepo katika maeneo yake. Kwa hiyo, tunaomba sana Waziri Mkuu kwenye jambo hili atusikilize na sisi Wabunge. Sisi Wabunge wenyewe tumekubali kwamba ile shilingi 50 iende kwenye shilingi 100 na tutatolea majibu kwa wananchi kwa nini tumeamua kuongeza tozo katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka kuchangia katika sehemu ya maji ni kwamba katika Jimbo langu la Mufindi Kaskazini kuna vyanzo vikubwa viwili vya maji. Katika Tarafa ya Sadani kuna vyanzo vya maji vya Mto Kihata. Hili eneo linahitaji shilingi bilioni mbili tu ili eneo hili liweze kusaidia kutoa maji katika vijiji 19. Tumeshaleta maombi mara kwa mara katika Wizara ya Maji lakini mpaka leo halijashughulikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo lingine la pili ni Tarafa ya Ifwagi. Tuna taasisi ya RDO ya watu binafsi imetusaidia kutoa maji kwa kata takribani tano na wanalisha vijiji takribani 30. Serikali haijatia mkono wake wowote katika eneo hili. Ni wakati umefika sasa kwa Serikali yetu kutia mkono. Kwa masikitiko makubwa kwenye eneo hili inafika wakati hawa wanatozwa VAT, kwa hiyo, badala ya kuwapa moyo wanakosa moyo wa kushughulikia eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni barabara. Tuna barabara kubwa mbili katika Jimbo langu la Mufindi Kaskazini ambazo nataka mziangalie
kwa macho mawili. Barabara moja ni kutoka Kinambo A – Isalavanu – Saadani - Madibila - Lujewa. Mwaka 2010 na 2015 barabara hii iliingia kwenye Ilani ya uchaguzi, kwa maana ya vipindi vyote vitano imeingia kwenye Ilani ya Uchaguzi lakini hata kilometa moja haijawahi kutengenezwa. Kwa hiyo, tunakosa majibu ya kuwajibu wananchi kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuomba sana Waziri Mkuu kwenye jambo hili aliangalie. Nakuomba Waziri Mkuu ufanye ziara katika Wilaya ya Mufindi kwa sababu hakuna kiongozi yeyote wa kitaifa ambaye amekuja katika Wilaya ya Mufindi kujionea hali halisi. Nataka nikuambie miongoni mwa maeneo ambayo tunapata kura nyingi CCM ni Wilaya ya Mufindi. Wananchi wa Wilaya ya Mufindi wasije wakakata tamaa kwa sababu yale mambo ambayo tumeyaahidi hayafanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine tulilokuwa tunaomba mtusaidie ni barabara ya kutoka Johns Corner - Mgololo na barabara ya kutoka Mchili – Ifwagi – Mdabulo – Ihanu - Tazara - Mlimba. Barabara hii inaunganisha Wilaya mbili na mikoa miwili. Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi haina uwezo wa kuitengeneza barabara hii. Kwa hiyo, tunaomba sana ipandishwe hadhi na tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kupeleka barua kupitia kwenye Road Board ya Mkoa, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo Waziri mhusika hajawahi kutujibu kwenye eneo
hili.