Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia afya njema na kuwepo katika kuchangia hii hoja ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe pole kwa familia ya Mheshimiwa Dkt. Macha ambaye Mwenyezi Mungu amempenda zaidi. Kwa muda mfupi niliokaa na Mheshimiwa Dkt. Macha nimejifunza vitu vingi sana na nikikaa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu huwa nawaambia
Mama Macha alikuwa na kipaji maalum kwa walemavu hasa. Hivyo Mwenyezi Mungu amrehemu amuweke katika njia iliyokuwa sahihi na ampe pepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda nitoe pongezi za dhati kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu ni mtu mnyenyekevu, huruma, na mwenye upole. Nataka nimpe usia mmoja kama ndugu yangu, tulichukua Qurani na Biblia tukasema tutatenda haki kwa Watanzania. Nina imani kwa unyenyekevu na upole wake atawatendea haki Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania sasa hivi tunasimama kutaka kutatua migogoro ya Burundi, tunaiacha Zanzibar iko katika mgogoro, Zanzibar ni mwiba. Mwiba ule kwa unyenyekevu kabisa, nakuomba Waziri Mkuu uliapa kutenda haki na kuwatetea Watanzania, basi lile unaloliona wewe litakuwa haki ulisimamie kwa vile Qurani hii itakuja kutuadhibu siku moja. Qurani na Biblia zetu hizi zitakuja kutuadhibu siku moja tutende haki kwa waislam, wakristo
na wote wanaopenda haki katika Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, nataka nimshukuru tena Waziri Mkuu, nilitoa hoja ya kumuomba Waziri Mkuu ashughulikie suala la korosho kuhusiana na tozo. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu nikiwakilisha wananchi wa Mtwara, Lindi na walima
korosho wote kwamba ameweza kulitatua tatizo lile kwa asilimia kubwa sana, sasa hivi tuko katika neema. Neema hii tunaomba iende katika mazao ya tumbaku, pamba na kahawa. Naamini Mheshimiwa Waziri Mkuu una uwezo mkubwa, ahsante sana na Mwenyezi Mungu atakujalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka katika Mkoa wa Lindi. Mkoa wa Lindi ni wa mwisho katika maendeleo lakini ni wa kwanza kwa kuwa na resource nzuri, lakini bado keki ya kugawiwa Lindi inapelekwa ndogo sana. Nataka niongelee tatizo la maji Lindi na ni karibu miaka 10 tunazungumzia, leo Manispaa ya Lindi imetumia shilingi bilioni 51 lakini hakuna maji. Hata hivyo, nataka nitoe sababu ya msingi inayosababisha miradi ya maji kufeli. Tunawapa
wakandarasi kutoka India na hela zinapelekwa shilingi bilioni 51, mkopo wa Watanzania, mkopo wa walipa kodi, kwa nini zipelekwe India? Tunaagalia mradi wa maji wa Chalinze,
shilingi bilioni 51 hela zote kunapelekwa katika Benki ya India sio Bank of Tanzania. Tujiulize, maji hakuna tayari mabilioni yanakwenda India, kwa faida ya nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ana meno na macho ya kuangalia, nashauri akaangalie hili suala la maji Tanzania nzima. Kila ukija humu ndani watu wanalalamikia maji lakini mabilioni ya pesa ya maji yamepotea kwa ajili ya wazembe wachache ambao wamefanya wanawake wanatoboka utosi kwa ajili ya kutafuta maji kisa wao wananufaika na kuzichukua zile pesa kuzipeleka India. Inakuwaje mkopo wa World Bank unachukua pesa za Mtanzania, zinawekwa Benki ya India na sisi wenyewe tumenyamaza? Cha kushangaza miradi hii yote wamepewa Wahindi, kuna syndicate hapa. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kabla hujamaliza kuhitimisha uandae Tume ujiulize ni akaunti ngapi za maji zimepelekwa nje? Akaunti ngapi za ujenzi wa barabara zimepelekwa nje na kwa faida ya nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Lindi mpaka leo haujafika hata shilingi bilioni mbili lakini tayari shilingi bilioni 51, nilikuwa Mjumbe wa Bodi ya Maji, alipewa MS Jandu shilingi bilioni 13.7 maji hayakupatikana Lindi. Akapewa tena shilingi bilioni 16 maji hayakupatikana Lindi. Amepewa shilingi bilioni 29 maji Lindi hamna. Je, hizi hela za walipa kodi tunazifanya nini? Ni madeni ambayo yangeweza kuzuilika lakini haiwezekani kutokana na watu wachache wanaifanya hii nchi isitawalike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia uhifadhi wa wanyamapori. Mimi ni mdau wa wanyamapori, ni Mwenyekiti wa Kupambana na Ujangili. Kwa idhini yako, nataka nimuombe ahakikishe mpaka wa Gorogonja ambao unaunganisha Serengeti na Masai Mara usifunguliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Waheshimiwa Wabunge wengi hawaelewi ni wapya, nashauri wapewe semina wajue kwa nini mpaka wa Gorogonja usifunguliwe. Mtalii akija Tanzania atarudi kwenda kulala Kenya, uchumi wote utapelekwa Kenya. Ni lazima tuhakikishe kuwa tunajitambua kuwa ule mpaka ni sumu kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mzigo muda mrefu nataka niutue, lakini leo nataka nimtulie Waziri Mkuu mzigo huu. Mjusi ameanza na Mheshimiwa Mudhihir akashindwa mahali pa kuupeleka yule mjusi. Akaja Mheshimiwa Mama Mikidadi na Mheshimiwa Riziki, dinosaur
ambaye yuko Ujerumani nimeshindwa kulitua. Hapa simtulii Mnyamwezi wala Mndengereko mzigo huu namtulia Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato yanayopatikana na dinosaur yule ni makubwa sio ya kubeza ndani ya Bunge hili. Leo watu wa Lindi hatuna mirahaba ya TANAPA, hatupati tozo yoyote ya Ngorongoro lakini tungepata pato la mjusi, shule za Mipingo, Matakwa, Namapwia, tungepata
barabara, tunajiuliza kigugumizi kiko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema tena, sitamuuliza swali hili Mheshimiwa Maghembe, nitauliza Ofisi ya Waziri Mkuu mpaka Mwenyezi Mungu aniondoe katika Bunge hili, suala la mjusi limefikia wapi? Naomba suala la mjusi huyu ulipokee wewe na unijibu wewe siyo mtu mwingine tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja tena katika masuala ya uwiano wa maendeleo katika Mikoa ya Kusini, Lindi na Mtwara. Mradi ambao ni mwiba katika Mkoa wa Lindi ni huu Mradi wa TASAF. Bahati nzuri nilimpelekea document kuonesha shule zilizojengwa Lindi ziko chini ya viwango,
hospitali zilizojengwa Lindi ziko chini ya viwango, vyoo vilivyojengwa Lindi viko chini ya viwango, maji yaliyopelekwa Lindi hayapatikani, yote ilikuwa ni miradi ya TASAF, lakini nataka nitoe sababu na yeye kwa vile yuko humu ndani akalisimamie, tuko pamoja kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya viongozi wamekuwa miungu watu ndani ya Wilaya zetu, hawa wanaitwa Makatibu na Wenyeviti. Wale wanawatisha Madiwani wasifanye kazi zao, wasikague miradi, matokeo yake nafikiri umeona. Choo cha TASAF kimejengwa kwa
karibu shilingi milioni 100 hakuna choo. Darasa limejengwa limeshaanguka. Je, tutaendelea na TASAF III wakati TASAFIā€¦ Kuhusu Utaratibu....
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniongezee muda wangu. Mheshimiwa Waziri Mkuu mjusi namhamisha kutoka kwa Mheshimiwa Riziki, Mheshimiwa Bobali, nakukabidhi tupate mapato na tozo liende Namapwiya, Mipingo na Nangaro. Wakati Mheshimiwa Rais anakuja Nangaro alisema atatuletea mapato katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nashukuru na nawapenda Watanzania wote, Mungu ibariki Tanzania na Mungu mbariki Waziri Mkuu. Ahsante sana.