Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuhusiana na mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali tukifahamu kwamba Waziri Mkuu kwa mujibu wa Katiba ndiyo mwenye udhibiti na usimamiaji wa ujumla wa shughuli za Serikali. Nina mambo manne kama nitapata muda wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo nataka kulizungumzia ni hali ya uchumi. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Mkuu anaonesha kwamba hali ya uchumi ni nzuri, mfumuko wa bei uko chini asilimia 5.2 lakini jana tu NBS wametoa taarifa mpya ya mfumuko wa bei ambao
umepanda kwa kasi sana. Sasa hivi hali ya wananchi kwa kweli ni ya kupoteza matumaini, bei za vyakula zimepanda, sukari imefika mpaka shilingi 2,500 kwa kilo, maharage yamefika mpaka shilingi 3,000 kwa kilo, u nga kuna maeneo ya nchi umefika mpaka shilingi 2,200 kwa kilo. Kwa hiyo, kuna haja ya kuweza kuangalia taarifa ambazo Wizara zinapeleka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu inaonesha kwamba taarifa
ambazo Waziri Mkuu amezitoa katika ibara ya 20 ya hotuba yake ni outdated, siyo taarifa za sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Waziri Mkuu katika ibara ya 26 ya hotuba yake ameongelea ajira na kusema kwamba tumeingiza ajira mpya 418,000 lakini naomba ifahamike kwamba kwa mwaka Tanzania watu wanaoingia kwenye soko la ajira ni milioni 1.6. Kwa hiyo, kuingiza watu 418,000 maana yake ni kwamba kuna zaidi ya watu milioni 1.2 ambao hawajapata ajira na wako nje ya shughuli za kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo kuna ajira zimepotea. Ndani ya Manispaa yako Mwenyekiti, Manispaa ya Ilala jumla ya biashara 2,900 zimefungwa. Maana yake ni kwamba leo Ilala hamuwezi kupata service levy, leo Ilala hamuwezi kupata leseni za biashara, kwa sababu biashara zimefungwa kulingana na sera za Serikali ambazo siyo rafiki kwa watu kuweza kufanya biashara inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia matamko kwa mfano ya viongozi yanasababisha upotevu mkubwa wa mapato.
Mimi nafahamu na natambua juhudi ambazo Rais anazifanya, anataka tukusanye mapato zaidi kwenye madini, lakini Rais hafahamu na wasaidizi wa Rais pia hawafahamu kwamba tamko lake alilolitoa Mkuranga kuhusiana na mchanga limepoteza mapato ya Serikali kuliko mapato yoyote ambayo tungeweza kuyakusanya kwa miaka 20 iliyopita na nitawapa takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 1998 tulipoanza uchimbaji mkubwa wa dhahabu mpaka mwaka 2016 tumeuza nje dhahabu ya Dola za Kimarekani bilioni 18 na makusanyo yetu kwa miaka yote hiyo ya kodi ni dola za Kimarekani milioni 833. Tamko alilotoa Rais Mkuranga, kwa sababu kulikuwa na mazungumzo ya kuuza Kampuni ya Acacia ambayo ingeingiza mapato mengi sana Serikalini kupitia capital gain tax ambapo tulipitisha sheria hapa, tumepoteza Dola za Kimarekani milioni mia nane themanini na nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Rais anazungumza kukusanya mapato, Rais huyu huyu anaipotezea nchi mapato. Haya ni mambo ambayo tunapaswa tuwe makini nayo sana na ningeomba viongozi hasa Mawaziri wajaribu kumshauri. Tunajua ana dhamira njema, lakini tuifanye kwa
namna ambayo haiathiri maslahi ya Taifa kama ambavyo imefanyika sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi hapa kulikuwa kuna mwongozo ambao umeombwa na Chief Whip wa Serikali ametoa maelekezo ambayo wewe umeyakubali.
Maelekezo ambayo Chief Whip ameyatoa na wewe umeyakubali hayaendani na Kanuni za Bunge. Suala la Mtanzania aliyepotea Ben Sanane, ni suala ambalo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa hali ya juu sana, sio suala linalopaswa kuchukuliwa kisiasa. Sio suala linalopasa Wabunge wabebe uthibitisho waulete mezani kwako kwa sababu taarifa ambazo ziko sasa hivi na zipo Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba Novemba 15, Ben Sanane kwenye mawasiliano yake ya simu kuanzia asubuhi alikuwa maeneo ya Tabata, akaenda maeneo ya Mikocheni, akatumia muda mwingi sana maeneo ya Mwenge, akapelekwa au akaenda Mburahati, saa nne usiku tarehe 15 Novemba, simu yake
ikapoteza mawasiliano na toka hapo hajawahi kuwa traced tena na haya maelezo yako polisi. Ukifuatilia Jeshi la Polisi wanakwambia sisi tumefikia mwisho, lakini mwelekeo wetu unaonesha kwamba waliomchukua Ben Sanane ni Usalama wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ume-save kwenye Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama na Mambo ya Nje, unafahamu sheria ya Usalama wa Taifa, kifungu cha 5(2) kinaipiga marufuku Usalama wa Taifa ku-enforce laws.
Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya kukamata, hata wakimwona mwizi hivi, sheria inawakataza, kwa sababu ya kuepuka haya mambo ambayo tunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kumekuwa na matukio hatuyapatii ufumbuzi. Ninyi mnafahamu na mnakumbuka aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, alikamatwa, akateswa, akaumizwa na leo jicho lake moja, halioni lakini mpaka leo hakuna hata
mtu mmoja aliyekamatwa kulingana na tukio kama hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mazingira kama haya, hatuna namna na siyo kawaida ya Bunge hili ninyi wenyewe ni mashahidi ambao mmekaa Bungeni muda mrefu kujadili Usalama wa Taifa. Kwa mara ya kwanza tunaivuka hiyo taboo kwa sababu watu wamechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa mujibu wa Kanuni ya 120 ya Bunge, natoa taarifa rasmi kwamba nitaleta Hoja Binafsi ndani ya Bunge ili Bunge liunde Kamati Teule ya kufanya uchunguzi wa matukio yote ya upoteaji, mauaji na matukio ambayo yanaweza kujenga taswira hasi dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizikumbushe Kamati za Bunge, kuna masuala ambayo Kamati za Bunge hazipaswi kupelekewa na Spika, zinapaswa kufanya zenyewe, ndiyo maana Bunge lina utaratibu wa taarifa maalum.
Mimi ningetarajia Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ingetuletea taarifa maalum kuhusu mambo haya badala ya kusubiri mpaka Wabunge wazungumze, tuanze kujianika na kama nilivyoeleza it was a taboo kuongelea Usalama wa Taifa ndani ya Bunge lakini leo tunaongelea kwa
sababu ya utendaji mbovu ambao unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetoa taarifa kwa mujibu wa Kanuni ya 120 ya kuunda Kamati Teule na ndiyo taarifa ambayo inapaswa kufanyiwa kazi kwa mujibu wa Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nataka nimkumbushe Mheshimiwa George anafahamu, ni rafiki yangu, ni ndugu yangu yaani ndugu kabisa, waliokwenda kuvamia Clouds Media ni Kikosi cha Ulinzi wa Rais na ninaweza kuthibitisha, aliyemtolea bastola Mbunge wa Mtama ni Afisa Usalama wa Taifa na ninaweza kuthibitisha. Kwa hiyo, kama Bunge linaweza likaunda chombo cha kutaka nikathibitishe hayo,
niko tayari kuthibitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie, Mheshimiwa Waziri Mkuu ibara ya 31 ya hotuba yako imezungumzia kilimo na umezungumzia mavuno ambayo tumeyapata msimu uliopita wa 2014/2015. Naomba nikukumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, taarifa ya
Benki Kuu ya Quarterly Economic Review inaonesha kwamba kilimo kimekua kwa asilimia 0.3 tu. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba, wananchi wetu vijijini mwaka 2016, wengi wamekuwa maskini kwa sababu ya ukuaji mdogo katika sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia mbolea ambayo Serikali imenunua tani 30,000. Ni kazi nzuri sana mbolea imenunuliwa lakini naomba nikufahamishe katika kila mfuko wa mbolea ambao umenunuliwa kwa shilingi bilioni 10 Serikali ilizotoa, watu wako ama ni watendaji wa Wizara ya Kilimo au TFC wameongeza shilingi 15,000 kinyemela. Mnunuzi wa kawaida akinunua
mbolea Dar es Salaam ananunua kwa shilingi 55,000 mpaka ifike kwa mfano Rukwa, Kigoma au Katavi mbolea ile inauzwa kwa shilingi 60,000. Leo hii mbolea ambayo imenunuliwa kwa fedha za Serikali, kwa kampuni ya Serikali ikifika Sumbawanga, Mpanda, Kigoma ni shilingi 75,000.
Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, jana nimekuona umechukua uamuzi katika mambo kama haya ya pembejeo, nakuomba umwagize CAG akague…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nimeweka pia kwa maandishi nitayaleta ili iweze kufanyiwa kazi kwa uzuri zaidi. Naomba Ofisi yako
imwagize CAG akague manunuzi ya mbolea ya shilingi bilioni 10 yaliyofanywa na kusambazwa katika msimu huu na taarifa hiyo uweze kuifanyia kazi, kwa sababu kuna shilingi 15,000 zimeongezwa kwenye mbolea zote zilizonunuliwa ile ya DAP na ile nyingine ya kukuzia. Kwa hiyo, naomba jambo hilo uweze kuliangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu ibara ya 17 ameongea maneno mazuri sana kwamba tufanye siasa na naomba nimnukuu, ni maneno mazuri sana, anasema; “Ninatoa rai kwa wadau wa siasa kote nchini kujenga utamaduni wa masikilizano na
kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa za kuunganisha watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu mmetufungia kufanya siasa. Tunafanyaje siasa za kuwaunganisha watu wakati hatufanyi mikutano ya hadhara? Tunafanyaje siasa za maendeleo wakati hatufanyi mikutano ya hadhara? Tunafanyaje siasa za uwajibikaji wakati hatufanyi mikutano ya hadhara na mnafahamu kabisa kwamba ni kinyume cha Katiba. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Waziri ambaye unahusika na suala la vyama vya siasa umshauri Rais.