Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nawapongeza sana wachezaji wa Simba, jana kidogo watulaze na viatu, lakini kwa kweli kazi waliyoifanya ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu, la kwanza nachukua nafasi hii kwa dhati kabisa ya moyo wangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuleta maendeleo ya Taifa letu. Wakati mwingine maneno haya ni kwa sababu mnafanya
kazi nzuri. Ukiona mtu anakushambulia hivi, ujue unafanya kazi nzuri sana. Na mimi niwatie shime kwamba endeleeni na kazi hiyo ili Taifa letu liweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa, nawapongeza watu wa TAMISEMI vilevile na Wizara ya Afya kwa kutupatia fedha kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Hamai ambacho kwa leo ndiyo tunakitumia kama Hospitali ya Wilaya ya Chemba. Nawashukuruni sana na ninaomba kazi hiyo ya kujenga wodi, nyumba za waganga iweze kufanyika kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie maji. Tuna Mradi wa Maji wa Ntomoko, alisimama Mbunge mmoja hapa akasema ufutwe, lakini mimi nasema ashindwe tu, kwa jina la Yesu. Ni kama amedandia gari katikati, kwa sababu hajui chanzo chake na hajui mwisho wake. Mradi huu una changamoto zake ndogo ndogo, lakini mimi namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kukubali kwenda, kama Mungu akijaalia wiki ijayo ili na wewe ujionee kwa namna moja
ama nyingine changamoto zilizopo kwenye mradi huu ili ziweze kutatuliwa na watu wapate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni suala la kuhamia Dodoma. Kwa namna ya kipekee kabisa sisi Wabunge wa Dodoma tulikuwa na mkakati kabla ya tamko la Mheshimiwa Rais kuleta muswada binafsi hapa Bungeni ili Serikali ihamie Dodoma, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuamua kwa dhati ya moyo wake kuhamia Dodoma, lakini suala hili halipo kisheria. Naiomba Serikali sasa ilete muswada Bungeni hapa ili iwe sheria. Anaweza kuja mtu mwingine kesho akasema Makao Makuu ya nchi anayapeleka kwingine. Kwa hiyo, niwakumbushe hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile pamoja na kuhamia Dodoma, harakisheni ujenzi wa mradi wa maji wa bwawa la Farkwa ambao pia utaongeza maji Dodoma, Chemba, Chamwino na Bahi. Leo tathmini imeanza kule Farkwa, Mombose na Bubutole, vile vijiji vinahama basi wale watu
walipwe fidia zao mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, Serikali lazima iwe active, lakini siyo kuwa active kwa kukosea. Nitoe mfano, samahani sana, jana nilikuwa naangalia mkutano wa waandishi wa habari (press conference) na yule Bwana anaitwa sijui nani yule…Roma Mkatoliki. Hivi Waziri
wa Habari alikwenda kufanya nini? Unajua wakati mwingine unaweza kuambiwa ukweli ukachukia, lakini ni afadhali uambiwe ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Habari amekwenda kwenye mkutano wa Roma Mkatoliki,
anampisha na kiti, anayeongoza press conference ile ni Zamaradi Kawawa, Afisa wa Serikali. Hivi kesho, mtu akikwambia wewe ndio ulimteka Roma, utakataaje? Ni vizuri uchukue ukweli hata kama unauma, lakini take it. At the end of the day unaweza ukafanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine mnamgombanisha Mheshimiwa Rais na wananchi bila sababu ya msingi. Mimi sikuona logic kabisa. Mimi siyo mwanasheria, nimesoma uandishi wa habari na nimesoma uhusiano wa kimataifa, lakini this is wrong. Is not applicable! Kwa hiyo, Serikali wakati mwingine mnaingia kwenye mtego wenyewe bila kujua. Hebu liangalieni hili, ilitokea wapi mpaka Mheshimiwa Waziri anakosa kiti, anahama, halafu huyu mtu binafsi anafanya press conference, wewe unakwenda kufanya nini? What were you doing there? Halafu leo akina Nkamia wakisema ukweli humu, kuna watu wanasema, aah, unajua labda kwa sababu alikosa Uwaziri. No, we have to tell you the reality! This is a principle!
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu suala la kuongeza maeneo ya utawala. Hapo nyuma tumeongeza sana maeneo ya utawala lakini bado tunashindwa kuhudumia yale maeneo tuliyoyaongeza. Hebu angalieni, malizeni kwanza tatizo la yale maeneo mliyoyaongeza ya
utawala ndiyo muanze kuongeza maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo ulipoletwa, idadi ya watu ilikuwa tofauti na sasa. Fanyeni review, Chemba ilikuwa na watu 160,000, leo tuko watu 250,000, lakini bado
kiwango cha Mfuko wa Jimbo kinachotolewa ni kile kile cha wakati ule na wakati mwingine kinapunguzwa, amesema Ngeleja hapa. Hebu angalieni namna gani mnaweza kuongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo. Jana amesema hapa Mbunge wa Kiteto, kuna tatizo kubwa kati ya Wilaya ya Chemba, Kiteto, Kongwa na Gairo. Watu wa Kiteto wanafikiri kama ni Jamhuri ya Wamasai hivi ndani ya Tanzania. Baadhi ya viongozi wanaopelekwa katika maeneo
haya, nao ni shida. Hebu tusaidieni, mtaniwia radhi. RAS wa Manyara, DC wa Kiteto, DC wa Chemba, kabila moja na wanawasiliana vizuri sana. Matokeo yake kumekuwa na crisis katika Wilaya hizi kwa sababu Wagogo, Wakaguru, Warangi hawatakiwi Kiteto. Amekaa miaka 30 anaambiwa ondoka leo. Hivi leo na sisi tukaamua Mrijo tukafunga mpaka, hakuna Mmasai kuingia Chemba… Taarifa...
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ni ushauri, wala siyo taarifa tu. Kwanza hawa niliowasema, ni watani zangu wote, hawa Wakurya wote watani zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema, tunazungumza leadership credibility. Wapo watu wanapewa vitu vidogo vidogo kuwaumiza baadhi ya watu. Mtu amekaa miaka 30, unamwambia ondoka leo, acha nyumba yako, wewe ni Mrangi nenda Chemba. Wewe ni Mgogo toka, nenda Kongwa, wewe ni Mkaguru toka nenda Gairo. Tukae kimya! This is a problem. Ni ndani ya Tanzania hii kaka yangu anayoisema pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tufike wakati sasa tuwe serious ili tuendelee kuishi kwa umoja na amani yetu. Namshukuru kaka yangu pale, namheshimu sana kwa ushauri wake, nimeupokea, lakini pia kwa wakati mwingine nanyi upande wa pili muwe mnaangalia maneno ya kutumia, isiwe upande mmoja tu. Kisu kikate kote kote. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho, mimi ni mwana michezo. Naomba sisi Wabunge tuiunge mkono timu ya Serengeti Boys kwa nia njema kabisa na Serikali nayo iweke mkono wake ili timu yetu ikafanye vizuri, badala ya kulaumu tu wachezaji, na sisi tuoneshe moyo wa upendo kwa timu zetu ili tupate vijana walete heshima kwa Taifa letu.