Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Na mimi niungane na wengine kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo aliamua kwa vitendo kuleta Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma. Kwa kweli ni uamuzi wa kishujaa na busara, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye ndiye aliyeongoza jahazi la Mawaziri kwa maana ya Wizara zote kuja hapa. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista na Ofisi yake maana yeye ndiye aliyetangulia kufungua mlango kumpokea Waziri Mkuu. Kwa kweli pongezi sana Mheshimiwa Jenista kwa kuratibu zoezi hili na kuhakikisha Wizara zote zinakuja hapa
Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza haya kwa sababu Dodoma ni pacha na Mkoa wa Singida. Kwa hiyo, pacha wetu akipata neema na Singida tunapata neema kwa maana ya kwamba Wizara zote na watu wengi watakaoishi hapa Dodoma watatumia bidhaa kutoka Singida. Kwa hiyo, sisi wana Singida tumejiandaa kuleta mazao mbalimbali kwa maana ya kuku, karanga, viazi, vitunguu na mazao mengine mengi pamoja na mafuta mazuri sana ya alizeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kidogo kwamba mara nyingi Makao Makuu ya Serikali jengeni Mji uwe Makao Makuu ya Serikali. Naomba ile miradi mikubwa ya uwekezaji leteni kwenye Mikoa yenu iliyo jirani ukianzia Singida ili Mji huu ujengeke kama Mji wa Kiserikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niwapongeze Mawaziri wote. Mawaziri safari hii mmekuwa wanamgambo kweli kweli. Mmeweza kuchapa kazi hamjakaa maofisini. Sisi wenzenu tunataka tuwaambie, mnapofika mikoani hata wale watendaji wenu waliopo kule hakika wanapata hamasa ya kufanya kazi. Pia wananchi wanapoona Mawaziri mnatembelea miradi na kuangalia changamoto mbalimbali hiyo tunajijengea imani kwa wananchi kwamba Serikali yao inawajali. Pongezi sana Mawaziri wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini alikuja Singida kufungua Mradi wa REA III. Kwa kweli napongeza sana na tunawaomba wale wakandarasi wakatimize sawasawa na mkataba unavyosema ili wananchi waendelee kunufaika na mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoileta hapa nataka kusema iko sahihi kabisa, lakini nataka kushauri katika eneo moja tu. Eneo hilo ni kutokana na diplomasia ya kiuchumi inayofanywa na Mheshimiwa Rais wetu. Marais waliopita wamefanya lakini
na yeye amefanya diplomasia kubwa sana maana tumeshuhudia viongozi wakuu mbalimbali wa nchi wakitembelea nchi yetu, kwa kweli ninampongeza lakini tumeshuhudia mikataba kwa maana ya makubaliano (MoU) zikisainiwa pale Ikulu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuuliza ni nani anayefuatilia makubaliano haya kwa sababu tunahitaji kupata mrejesho kwamba ilisainiwa 20, 60 au mingapi na imetekelezeka mingapi? Pamoja na kwamba tumeona kuna mingine imeshaanza, lakini kwa ushauri wangu kwa sababu nina mfano halisi, tangu Rais wetu ameingia naomba nisitaje Marais au wakuu wa nchi ambao wameshakuja hapa kwetu na kusaini mikataba mbalimbali ni tisa, ni mingi. Kwa hiyo, nashauri kuwe na chombo maalum cha kitaifa ambacho kitaundwa kiwe chini ya Kamishna ambaye ni mbobezi katika masuala ya uchumi na diplomasia. Chombo hiki kiwe na wanasheria, wanadiplomasia, wachumi na kadhalika ili waweze kukaa kuainisha MoU hizi na kuhakikisha zinapelekea kwenda kwenye mkataba unaotekelezeka. Kamishna huyu awe anaweza kucommunicate na taasisi zote zinazohusika kutokana na MoU hizo au makubaliano hayo ili kuleta matokeo chanya ambayo yamekusudiwa na viongozi wetu husasan Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hayo kwa sababu kabla ya awamu hii alikuja Rais kutoka China na viongozi wengi pamoja na wafanyabiashara na Rais wetu akaenda. Alipofika hapa wakaingia MoUs nyingi lakini utekelezaji wake mmoja tulifika pale Beijing China wakatuambia kwamba kulikuwa na makubaliano ya ndege ya China kuja Tanzania kuleta watalii, lakini hakuna aliyeweza kujibu suala lile hatimaye ndege ile ilihamia Kenya. Hii inatia uchungu na ndiyo maana nimeshauri kuwe na chombo maalum kitakachosimamia makubaliano hayo kupelekea kwenye utekelezaji unaoleta matunda chanya katika taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, isije tukaishia tu watu kupiga picha na kumwaga wino, ni lazima tuwe na mkakati huo. Pia kuwe na library ya kutunza mikataba au makubaliano hayo. Ni nani anaweza akatuambia, je, kuna maktaba inayotunza, iko mingapi? Napenda nijue kwa miaka mitatu au minne awamu iliyopita na hii, je, ni mikataba au makubaliano gani ambayo yamefikia kwenye utekelezaji? Naomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kumalizia, tulipotoka ni mbali Taifa hili na Mungu wetu amekuwa akitupenda Watanzania, amependa sana Taifa letu. Naomba kusema anayefikiri na kudhani amesimama na aangalie asianguke. Kwa sababu ufalme ukifitinishwa hakuna atakayebaki salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba anayedhani amesimama na aangalie asianguke. Tusije tukawa kama wale wajenga mnara wa Babeli kila mtu akazungumza lugha yake kwa sababu walitaka kumpandia Mungu kichwani ndio maana Mungu akawasambaratisha. Naogopa Taifa hili tusije tukasambaratishwa kwa kunena na kutaka kupanda kwenye maeneo ambayo hakika sio nafasi yako. Anayedhani amesimama na aangalie asianguke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namtia moyo Rais wangu, endelea kufanya kazi, haukuja kimakosa maana kila utawala ni maridhio ya Mwenyezi Mungu. Fanya kazi tupo pamoja, kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu na Mungu atakuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani niliwahi kusema kuna watu humu ndani wako kama hali ya hewa ya Dar es Salaam. Dar es Salaam jua litawaka leo, kesho ni mafuriko, leo ni mafuriko kesho ni kipupwe. Kwa hiyo, kuna watu ni vigeugeu, leo watasifia jambo, kesho watalibeza, leo watalalamikia jambo, kesho watalibeza. Rais wetu kama nyumba inavuja tia gundi, tia nta, endelea kuchapa kazi kwa maana mvua haiwezi kuacha kunyesha. Naomba nimtie moyo Rais wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema kwamba naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na sisi Wanasingida tumejiandaa sawasawa, michango mingine nitachangia kwenye Wizara zinazofuata. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.