Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Waziri Mkuu, Mawaziri pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimwambie kaka yangu Mheshimiwa Khatib, kwamba ugomvi wa mke na mume mara nyingi huwa wanamalizia chumbani. Mnapogombana huko chumbani, mkitoka nayo nje, hayo mambo yanakuwa yako hadharani, kila mmoja anayaingilia.
Sasa msilichukulie kwamba Serikali ya CCM ndiyo inayowafitinisha ninyi. Ugomvi huu ninyi mmeutoa chumbani, mmeuleta hadharani. Sasa naomba sana, msiizungumzie Serikali kwamba ndiyo inayowahujumu ninyi. Hebu mkakae mmalize matatizo yenu, msiingize Serikali kwenye matatizo yenu. Sasa nimekujibu basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze na bajeti ya Mfuko wa Bunge. Niungane na maoni ya Kamati ya Bajeti kwamba Mfuko wa Bunge unakabiliwa na changamoto nyingi za kutokupata fedha kwa wakati; na hata zinapopata hizo fedha, hazipati fedha yote. Naiomba Serikali iangalie huu Mfuko wa Bunge, kwani huu mhimili wa Bunge ndiyo unaopitisha bajeti zote hizi za Serikali ambazo zinakwenda kufanya shughuli za maendeleo. Ni mhimili huu wa Bunge. Sasa Mhimili huu, ndio huu huu tena ambao haupewi fedha za kutosha kuhakikisha kwamba zinatimiza majukumu yake ya kibunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti ili iweze kuhakikisha kwamba inatoa fedha za kuhakikisha zinaendesha shughuli za Bunge bila kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, safari hii Bunge limefika mahali Waheshimiwa Wabunge wamesafiri kwenda kwenye Kamati bila malipo kutokana na kutokuwa na fedha katika Mfuko wa Bunge. Sasa naiomba Serikali, pamoja na kwamba mihimili yote ina umuhimu wake, lakini mhimili huu una umuhimu zaidi kwa sababu ndiyo unaokaa kupitisha mambo yote haya ambayo hata wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu huwezi kwenda kukagua shughuli za maendeleo kama fedha hazijapitishwa na mhimili huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, katika mapendekezo yaliyotolewa kwenye kitabu cha bajeti ukurasa wa 14, tusipoangalia hili Bunge linaweza lisifike mwezi wa Sita. Wameomba mapendekezo pale wanasema, Kamati inaishauri Serikali kuridhia maombi ya bajeti ya shilingi bilioni 21 ili Bunge liweze kutekeleza majukumu yake mpaka kufikia mwezi Juni. Kwa hiyo, naiomba Serikali basi iweze kutekeleza hili angalau Bunge liweze kufanya shughuli zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la maji. Naishukuru Serikali, kule kwangu Korogwe nilikuwa na tatizo sugu la maji ambalo bado lipo halijakamilika, lakini angalau sasa limeanza kutekelezwa. Alikuja Naibu Waziri akatembelea akaona. Tuna Mto Pangani unapita katikati ya Mji wa Korogwe, alikuja akazungumza na akaenda kutekeleza, akatuletea fedha angalau shilingi milioni 500, tumeanza kuchukua maji kutoka kwenye Mto Ruvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwaomba Wizara ya Maji kwamba ni vizuri zile fedha ambazo walituahidi, shilingi bilioni mbili kwamba watatupa katika bajeti hii, basi waweze kuzitoa fedha hizo itakapokuwa tumepitisha kwenye bajeti ili ziweze kufanya kazi ya kutengeneza miundombinu pamoja na matenki ili kusudi wananchi wa Korogwe waweze kuondokana na tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya. Pale Korogwe kuna Chuo cha Uuguzi na chuo kile kiko chini ya Wizara ya Afya. Chuo kile hakijawahi kutengewa fedha miaka 10, lakini kina jengo ambalo limejengwa limesimama, ni la muda mrefu, miaka 10 halijawahi kutengewa bajeti. Fedha ambayo imeteketea pale ni fedha ya walipa kodi wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, jengo lile badala ya kuwa limesimama vile, matokeo yake litaanza kupata crack, Serikali itaanza kutenga bajeti nyingine kwa ajili ya kukarabati jengo lile. Naiomba sana Serikali iangalie ni namna gani itakavyomalizia lile jengo la Chuo cha Uuguzi pale Korogwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alitembelea eneo lile siku ambayo nimemwalika kwenye Jimbo langu kwa ajili ya kuja kuona shughuli za maendeleo, hususan ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho ni cha ghorofa tatu. Namshukuru Mheshimiwa Waziri alikuja akaona
tunafanya kazi nzuri na nategemea Mheshimiwa Waziri kwamba Mwenyezi Mungu akikujalia basi mnaweza mkatupiga jeki katika kile Kituo cha Afya, hasa ikizingatiwa kwamba Halmashauri ya Mji wa Korogwe haina Hospitali. Sasa kwa kuwa haina Hospitali, basi kile Kituo cha Afya ndiyo kitatufanya sisi tuwe na hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa, kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri alienda akaona kile chuo na akaliona lile jengo lilivyo, basi atusaidie zipatikane fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo lile ili ile fedha ya wananchi iliyokuwa imetumika wakati ule isiweze kupotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie tena suala la maji. Kuna miradi ile ya World Bank, ilikuwa itekelezwe pale Msambiazi, Lwengera Relini na Lwengera Darajani. Katika Bunge lililopita kulitengwa fedha, shilingi milioni 560 kwa ajili ya mradi wa Msambiazi na Lwengera Relini na Darajani, lakini fedha zile zinavyoletwa kule, maelekezo yanayofika kule, badala ya kujenga ule mradi wanasema zile fedha zilipe madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Maji na Umwagiliaji, mradi ule, wananchi wa Msambiazi wanachojua wao, wametengewa fedha. Sasa fedha inapokuja inaenda kulipa madeni ya miradi mingine iliyopita. Tunawaeleza nini wananchi wa Msambiazi na Lwengera Relini na Lwengera Darajani?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itenge fedha za madeni, ilipe madeni na zile zinazotengwa kwa ajili ya miradi, zipelekwe kwenye miradi husika. Ni matumaini yangu kwamba, Waziri wa Maji amenisikia. Ni vizuri hizo fedha zikatoka zikaenda kujenga ule mradi wa Msambiazi kama ambavyo ilikuwa imepangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara. Naiomba Serikali, hizi Halmashauri ambazo zinaitwa Halmashauri za Miji, naishauri Serikali kama inawezekana; kwa kuwa tayari inaitwa miji, Halmashauri za Miji au Manispaa, tuanze kutenga bajeti angalau ya kilometa mbili mbili au moja kwa ajili ya lami ili iendane na hadhi hiyo inayozungumzwa kwamba Halmashauri za Miji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pale Korogwe Mji, pale ni sebuleni; ukitoka Dar es Salaam, unakuja Korogwe, ndiyo hiyo inayokwenda moja kwa moja Kilimanjaro, Arusha, inaenda Nairobi, Kenya. Sasa pale sebuleni mkitusaidia kila mwaka tukawekewa angalau kilometa moja au mbili za lami, tutaishukuru sana Serikali angalau mji ule uweze kuwa na barabara za lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, naisema hiyo, inaweza ikasaidia sana kuondokana na zile barabara za changarawe ambazo zinatengewa fedha kila mwaka. Tukijenga hizi za lami zinakuwa na mifereji ambayo imejengewa, lakini hizi za changarawe hazijengewi na mawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali, kwenye miji hii ili tuifanye iwe miji mizuri, tujitahidi basi angalau kila mwaka tukiwatengea hiyo kilometa moja au mbili ili kusudi miji hiyo iweze kuwa mizuri kwa maana ya kuwa na lami katika mji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nishukuru tena, yangu machache yalikuwa ni hayo.
Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.