Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenisaidia na nimeweza kupata nafasi ya kuwa mwakilishi ndani ya Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile naomba nichukue muda huu pia kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwa sababu katika kikao kilichopita niliuliza maswali kutokana na madhara mbalimbali yanayowapata wananchi wa Geita Mjini kutokana shughuli za mgodi na aliwajibika kama alivyoahidi ndani ya Bunge lako Tukufu kufika na kuongea na wananchi, kutembelea sehemu za waathirika.
Mheshimiwa Spika, nina imani hatua tuliyofikia hatimaye hawa wananchi yawezekana wakaondolewa katika eneo husika, lakini pia ataweza kuwasaidia vijana wengi waliojiunga na ushirika na wataweza kupewa maeneo ya kuchimba dhahabu katika maeneo ya Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika huu Mpango, tunazungumzia sana maeneo ya viwanda na katika kuangalia eneo kubwa la viwanda, katika Mpango wanaonesha ni jinsi gani ambavyo Serikali imejipanga na kuwekeza katika maeneo ya viwanda. Wameongelea maeneo ya EPZ na SEZ, wameongelea pia maeneo ya industrial park. Vile vile ukisoma ule Mpango wa mwaka mmoja ulikuwa unazungumzia ni namna gani hizi EPZ na SEZ hazijaweza kuchangia vya kutosha katika pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Spika, tukiongelea masuala ya viwanda, tunaongelea mambo ya EPZ, lakini tunawapa watu maeneo makubwa ya kuwekeza, hawa watu pia tunawapatia misamaha ya kodi. Kwa hiyo, tunawapa maeneo ya kuwekeza lakini bado kama Serikali tunapoteza kodi. Kwa hiyo, ni vizuri pia Serikali ikaliangalia hili suala kwamba tunasema kuweka viwanda lakini kitu cha kwanza tuboreshe vitu vya msingi ambavyo ndivyo vinavyohitajika ili kuweza kupunguza kutoa misamaha ya kodi.
Katika hotuba ya Kambi ya Upinzani, imeweza kuonesha ni jinsi gani katika upande wa nishati ongezeko lilijitokeza katika Mpango uliopita ni kidogo, lakini pia katika miundombinu kwa maana ya barabara na vile vile hata katika kilimo ukuaji bado ni mdogo. Hata hizi EPZ zenyewe, bado wanaagiza hata raw materials wanazozitumia katika viwanda vyao. Kwa hiyo, ni lazima tuangalie kama Serikali kuweza kuwezesha kwanza nishati, tuwezeshe miundombinu na ndipo tukimbilie kwenye viwanda ili tuweze kuondokana na misamaha ya kodi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie upande wa mapato ndani ya Serikali. Serikali imeonesha kwamba kuna upungufu na tunashindwa kutekeleza mambo mengi kutokana na kutokuwepo na mapato ndani ya Serikali yetu. Katika Sheria ya Local Government ya mwaka 1982 inaonesha kwamba Halmashauri zetu (local government), zitaweza kukusanya fedha ya asilimia 0.3 ya Service Levy katika maeneo hayo kutokana na shughuli za mgodi ama shughuli za uwekezaji wowote ule unaokuwa katika maeneo ya Halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika, sheria hiyo pia imetoa kipengele ambacho Waziri ana uwezo wa kufuta kile kipengele cha 0.3 ya Gross Revenue na badala yake wanatoa kiwango ambacho wawekezaji hao wanalipa ndani ya Halmashauri husika. Kwa hiyo, tunapoteza fedha, tunapoteza mapato makubwa kutokana na sisi wenyewe kuzichezea sheria zetu na kutosimamia yale mambo ambayo tumeyapanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Service Levy hata hizo kidogo ambazo zimelipwa, tunashindwa kuona ni namna gani, kama Serikali kuu inaweza kusimamia kule chini ili angalau hii Service Levy inayotolewa 60% ya hiyo Service Levy iweze kutumika katika shughuli za maendeleo. Vile vile bado kama Serikali haiwajibiki kuhakikisha ya kwamba kiwango ambacho kinastahili kulipwa ili 0.3 ya Gross Revenue kuweza kui-determine, Serikali haiwajibiki kuwasaidia Halmashauri katika ku-determine hilo ili kuhakikisha kama Serikali na kama nchi tunapata mapato husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naomba nimpongeze kwa moyo wa dhati sana, kwa jitihada yake ya kusema ya kwamba watu walipe kodi. Binafsi kila nikienda sehemu, tunatafuta risiti tuweze kulipa kodi. Sasa kuna tofauti mbili kati ya Mwalimu Nyerere na Magufuli. Kuna tofauti moja tu, wote wanawapenda wananchi na tunawasikia na wanatamani kuona mabadiliko ndani ya wananchi, lakini Mwalimu Nyerere alianza kwake; kama ni kupunguza mshahara alianza kupunguza wa kwake akafuata wa wengine. (Makofi)
Kwa hiyo, namwomba pia Mheshimiwa Rais kwa kushirikiana na Serikali yake, mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukatwi kodi ya aina yoyote ile. Kwa hiyo, nachukua pia fursa kuiomba Serikali iweze kuliangalia hili suala kwamba inawezekana kabisa kwamba labda fedha ambazo Mheshimiwa Rais anastahili kupata ni kidogo au hizo alizozitaja Shilingi milioni 9.5 ni kidogo, lakini siyo kukwepa kodi au kumwekea msamaha wa kodi kwa maana inaonesha kama ni upendeleo wa aina fulani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuwajibike kama Serikali, tuweke kodi kwenye mshahara wa Mheshimiwa Rais kwanza na kama ni kuboresha, iwe hatua inayofuata ili tupate ile leading by example, wananchi waweze kuwajibika kwenye kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna masuala ambayo yameongelewa katika Mpango, suala la monitoring and evaluation. Katika shughuli zetu za Kamati, mimi binafsi nimeona shida ambayo imejitokeza kule.
Kuna maeneo ambapo Wizara na katika Mpango inaonesha kwamba Waziri wa Fedha anasema, watashirikiana na Wizara nyingine kuhakikisha kwamba usimamizi huu au monitoring and evaluation inafanyika katika maeneo yote na Wizara zote. Hata hivyo, kuna shida ya hii decentralization by devolution. Binafsi naiona kama vile ina tatizo kwa sababu Wizara inashindwa kwenda kuwajibisha watu moja kwa moja kule chini. Kwa hiyo, naomba…
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Taarifa!
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Waziri TAMISEMI....
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, hoja yangu ilikuwa ni kwenye mshahara wa Rais utozwe kodi, lakini pia vile vile kama Mheshimiwa Rais alituambia mshahara wake ni Shilingi milioni 9.5 sijui kama aliupunguza ama ilikuwaje, hilo mtatufafanulia ukoje, mimi binafsi siwezi kulisemea hilo. Hoja yangu ni kwamba mshahara wa Rais utozwe kodi, leading by example, yaani kuongoza kwa mfano. Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee katika hoja zangu nyingine. Nilikuwa nimeishia kwenye upande wa decentralization by devolution, naomba pia hilo liweze kufanyiwa kazi. Huu mkanganyiko uliopo kati ya TAMISEMI na Wizara uweze kuondoka ili Wizara iweze kufuatilia mpaka kule chini tuweze kuona mambo yanaendaje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna upande huu wa maendeleo ya watu. Naomba nizungumzie kipengele cha makazi bora. Naomba niishauri pia Wizara kama inawezekana ipunguze kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili wananchi wapate kujenga nyumba nzuri na badaye Serikali iende ikatoze kodi kwenye kodi za majengo. Tuwasaidie wananchi wetu waishi kwenye nyumba nzuri, wasipate magonjwa wasipate kuumwa na wadudu mbalimbali na waweze kufanya kazi vizuri kwa sababu watakuwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, kuna mahusiano makubwa sana kati ya makazi bora na afya za watu, pia katika upande wa elimu, upande wa wanawake, naomba pia Wizara iangalie kutenga fedha kwa ajili ya wanawake, tuweke suala la equity kwenye elimu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali, imeweka msamaha wa kodi kwenye sanitary towels kwa upande wa wasichana, lakini sasa Serikali iweke fedha ya kusambaza pad mashuleni ili watoto waweze kusoma na wasikose muda wa darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni kwenye upande wa good governance. Ili tuweze kuongoza vizuri kama Taifa, tunahitaji sana kuwa transparency, tunahitaji sana kuwa na accountability.
Mheshimiwa Spika, namwelewa Mheshimiwa wangu Rais John Pombe Magufuli ana nia njema sana, sana; lakini hiyo nia njema lazima iendane na transparency. Hatuwezi kuwa na Bunge ambalo linachuja taarifa! Yaani Bunge ambalo linafanya parental control ambayo inaenda kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa na Bunge ambalo hawataki wananchi waelewe Wawakilishi wao wanasema nini. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali mliopo hapa, mzingatie suala la transparency. Transparency ikiwepo, accountability itakuwepo na utumbuaji wa majipu hautahitaji Rais aende kila mahali, lakini wananchi wakiwa na taarifa husika, watawatumbua wao wenyewe katika maeneo yao, hata Wabunge wasiowajibika na wenyewe wataweza kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia hata Bunge lenyewe, tuchukue zamu zetu, tuwe wazi na tuweze kufanya kazi kwa uzuri na kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia.