Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake kwenye busara wa kuhamisha Wizara zote kuja Makao Makuu Dodoma. Pili, vile vile nimpongeze Waziri mwenye dhamana ndugu yetu Jenister Mhagama kwa kusimamia vizuri wizara hizi; zinaturahisishia sisi kama Wabunge kuweza kupita katika maofisi ambayo yako jirani, kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze na Wizara ya Afya; niiombe sana Serikali ione namna ya kuboresha maboma mbalimbali ambayo tumejenga huko kwenye majimbo yetu hasa zahanati na vituo vya afya ili yaweze kumalizika na kufanya kazi kama ambavyo sera inaelekeza
kuwa kila Kijiji na Mtaa kuwa na zahanati na kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na kwenye Jimbo langu; mimi na Waheshimiwa madiwani wenzangu na Serikali tumeweza kujenga zahanati 13 na kituo cha afya kimoja kizuri sana ambacho kimesimamiwa na diwani mmoja anaitwa Mlumbe kutoka pale Yamkeno. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ione namna ya kuboresha vituo hivi ili kusudio lile la kuwa na zahanati na Kituo cha Afya Kilonani iweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niishukuru sana Serikali kwa eneo langu la Makambako kwa kutupa vifaa vya upasuaji; naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo imetupa vifaa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maji. Naomba nipate majibu juu ya miradi ile mikubwa ya Miji 17 kwa Wizara hii ya Maji, fedha ambazo zinatoka India, katika miradi hii 17 mikubwa, mmojawapo upo katika Jimbo langu la Makambako. Kwa hiyo, naomba nipate majibu kutoka kwa Serikali, kwamba ni lini sasa fedha hizi zitakuja ili wananchi wa Makambako wawe na matumaini kwamba watapata mradi huu wa maji kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba Waziri mwenye dhamana atakayemteua ataanza kuja Makambako na nashukuru sana Waziri alikuja kama
ambavyo Rais alisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo. Niiombe Serikali ione namna ya kuboresha Wizara hii ya Kilimo hasa pembejeo hizi za ruzuku kwa sababu Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi juu ya pembejeo za ruzuku. Nadhani Serikali ione namna ya kupunguza tozo na kodi mbalimbali hasa kwa pembejeo hizi za mbolea ili kusudi kila maduka yauze na mkulima aende kununua kwa bei ambayo ni ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile Serikali ione namna ya kuboresha mbegu. Wako watu ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kuchakachua hizi mbegu; wakulima wetu wanapopanda mbegu hizi zimekuwa hazioti. Niiombe sana Wizara kwamba ifufue maeneo ambayo
walikuwa wanapanda mbegu kama pale Uyole, Njombe tulikuwa na pale NDC, tuna maghala pale na mashamba walikuwa nayo, wafufue suala hili la pembejeo ili wananchi wetu waweze kupata. Kwa hiyo, suala la mbolea nimeshalizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, pamoja na kazi nzuri anayoifanya, ingawa wapo watu wengine hata ungefanya kazi watasema hakuna kinachofanyika; unajua mtoto wa kambo hata ungemlea namna gani atasema hakuna kazi
zinazofanyika; Waziri unafanya kazi nzuri kupitia Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwamba katika ahadi zile za rais za kilometa sita za kujenga lami katika Mji wa Makambako, nikuombe sana na ile kilometa moja ambayo ulisema ingeanza mwaka huu wa 2016/2017 na muda
uliobaki ni mfupi, nimwombe sana Waziri ahakikishe kwamba, kilometa sita zile ambazo Rais alisema, mwaka wa 2017/2018 zinajengwa, ile ahadi itekelezwe ili wananchi wangu wa Makambako waweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme. Nikupongeze sana Mheshimiwa Profesa Muhongo, Naibu Waziri wako pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo tunaiona mnaifanya, hongereni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme, kwenye jimbo langu, maana kipindi kilichopita ilikuwa nipate awamu ile ya pili ya REA; lakini yule mkandarasi ambaye mlinipa, Lucky Export na baadaye mkamwondoa, kwamba hakuwa anakidhi vigezo, sasa mmeniambia mnaniletea mwingine kutokana na majibu ambayo nilimuuliza hapa Naibu Waziri. Niombe sana ahakikishe safari hii mkandarasi huyo anakuwa site kule Makambako katika vijiji vile nilivyovitaja ili shughuli hii ya umeme wananchi wangu waweze kupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fidia. Waziri wa Viwanda yuko hapa na Waziri wa Fedha yuko hapa, Waziri Mkuu alipokuja Makambako aliwaona wale wananchi, yaani mimi Mbunge wao silali. Chonde chonde, niwaombe sana kuhakikisha kwamba tunawapa fidia wananchi hawa kwasababu wameteseka zaidi ya miaka 18. Nikuombe sana, fedha hizi kwa Serikali ni hela ndogo, ili tuhakikishe sasa; kwa sababu na kwenye Bajeti ya Mwaka 2016/2017 walishawekwa; nimwombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Mpango tuhakikishe kwamba fedha hizi zinatolewa ili
wananchi wangu wa Makambako waweze kupata kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliwaahidi kwamba jamani suala la fidia tutakwenda kulimaliza. Nimwombe sana na mimi namwamini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, michezo. Ndugu yangu Mheshimiwa Mwakyembe uko hapa, Rais alituahidi kutuboreshea uwanja wetu wa michezo, nimwombe katika Mpango wake wa Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ahakikishe anaweka bajeti kwa ajili ya kuanza kutengeneza uwanja wetu wa michezo pale Makambako.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu. Niipongeze sana Serikali, tangu ilipokuwa inatoa fedha kwa ajili ya elimu bure watoto wameweza kuongezeka na kadhalika, lazima tuipongeze Serikali kwa kazi nzuri. Tumwombe Waziri mwenye dhamana kuhakikisha mnapeleka vifaa vya maabara ili watoto wetu waweze kupata elimu yenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fedha; tuhakikishe zinakwenda kwa wakati katika halmashauri zetu ili na sisi kama Madiwani tukiwa huko tuweze kusimamia zifanye shughuli za maendeleo kama ambavyo zimepangwa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini liko jambo hapa lazima niliseme, nisipolisema hapa nitasema wapi. Wapo Wabunge wenzangu wamesema, hivi iko sheria gani inayosema wewe Mbunge kwa sababu una kinga ukiitukana Serikali usikamatwe, sheria ya wapi? Kama umeitukana Serikali ni lazima ukamatwe upelekwe kwenye vyombo husika ukahojiwe kwa nini umeitukana Serikali. Kwa hiyo tusiweke kama kinga kwa sababu tuna kinga basi tuitukane tu Serikali halafu tusikamatwe, mimi sikubaliani kabisa, lazima tukamatwe, chombo kinachohusika kitufikishe mahali panapohusika. Unajua wako watu walizoea Serikali iliyopita kazi yao ni kuitukana Serikali, lazima tukubaliane na mabadiliko! Wewe unaitukana Serikali wakuache tu, unapita unaitukana Serikali wakuache, haiwezekani! Haiwezekani! Serikali inafanya kazi nzuri, tunaona (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.