Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kuanza niipongeze sana Hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na ningeomba basi Serikali ichukue yale mazuri yote ambayo inaona yanaweza yakaisaidia Serikali kufanya kazi zake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu nichangie suala la demokrasia. Hotuba ya Waziri Mkuu inaonesha kwamba, hali ya demokrasia katika nchi yetu inaboreshwa, lakini ningependa Serikali ijitathmini kama kweli Taifa hili sasa linasimamia misingi ya demokrasia. Ni vizuri ijitathmini kwa makini kwa sababu, kuna kila viashiria vya kuporomoka kwa misingi ya demokrasia katika nchi yetu,
kila viashiria vya kukosekana kwa uhuru wa habari, viashiria vya kukosekana kwa utawala unaofuata sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikajitathmini kwa sababu hata yote yaliyokuwa yanatokea asubuhi hii, yanalalamikiwa na Waheshimiwa Wabunge, ni kuonesha namna ambavyo misingi ya utawala bora katika Taifa hili imeshaanza kupotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wananchi wanapiga kelele kuhusu marekebisho ya Katiba walikuwa wanaona kwamba wana haki bado ambazo hazijakaa sawasawa katika dhana nzima na muktadha wa demokrasia katika nchi hii, lakini angalau kipindi hicho walipokuwa wakipiga kelele hali ilikuwa ni nafuu kidogo, lakini leo hali imekuwa mbaya zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inatuonesha kwamba kuna kuboreshwa kwa hali ya demokrasia na misingi yake katika nchi hii. Naendelea kusisitiza ni vizuri Serikali ijitathmini sana katika suala hili. Haiwezekani leo tuseme kuna misingi ya demokrasia katika nchi hii wakati vyama vya siasa haviruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara, likiwa ni jukumu lake la msingi kabisa la kisheria na Serikali imekaa kimya na viongozi wakubwa wa nchi hii wanaunga mkono jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwaje Serikali isijiamini kiasi kwamba leo inakuwa sawa na kumfunga adui yako minyororo mikononi kwenye mti ukampiga kadri unavyoweza halafu ukajisifu kwamba unafanya vizuri. Kwa sababu kama leo unazuia vyama vingine visifanye kazi ya siasa, halafu kuna mtu mmoja peke yake kwa sababu ni Mwenyekiti wa chama kimoja cha nchi hii, kwa kutumia kofia yake aliyonayo ya mamlaka yake anaweza akazunguka nchi nzima akijaribu kuzungumza yale ambayo anatenda yeye, hatakiwi ajibiwe, hatakiwi akosolewe, ni Taifa la namna gani? Demokrasia inakuwa iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo Mheshimiwa Rais anatupa Kauli Mbiu ya HAPA KAZI TU; kwa nini Rais asijue kwamba kazi ya Wanasiasa ni kufanya siasa? Kwa nini hajui kwamba viongozi wa vyama vya siasa wajibu wao, kuanzia kiongozi wa tawi mpaka Taifa ni kufanya siasa? Kwa nini umpangie kiongozi wa kisiasa kufanya vikao vya ndani tu? Kwa nini nchi hii wanasiasa wanaoruhusiwa kufanya kazi wawe ni Wabunge tu, lakini viongozi waliopewa kazi ya kisiasa, Makatibu, Wenyeviti na Viongozi wengine wazuiwe kufanya kazi zao za kisiasa kwa sababu ya kuogopa vivuli vyetu wenyewe?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali ijitathmini kama kweli nchi hii inatimiza misingi ya demokrasia. Kama inajiangalia vizuri, vyama vya siasa viruhusiwe kutimiza wajibu wake wa kufanya kazi za kisiasa kwa sababu chama cha siasa ni lazima kinadi sera zake, ni lazima kinadi falsafa yake, ni lazima vinadi itikadi zao, kikiwemo Chama cha Mapinduzi ambacho kinatakiwa kitetee Serikali yake. Vyama vya Upinzani viikosoe Serikali ili Serikali ijitathmini na ijitazame kama iko sawasawa. Sasa kama vitu hivyo haviruhusiwi katika Taifa hili demokrasia iko wapi ndani ya Taifa hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani si sahihi Mheshimiwa Waziri Mkuu kusema kwamba misingi ya demokrasia katika Taifa hili inatekelezwa; labda atwambie tumerudisha nchi hii nyuma miaka 40 sasa, jambo ambalo si jema na sio lenye afya katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijiulize, Serikali inajipimaje kwa wananchi wake wa kawaida kama haitaki kusikia kutoka kwingine? Haitaki kusikia wananchi wanasema nini. Mnasubiri tafiti za kitaalam ambazo mara nyingine zinatolewa kwa woga wala haziwezi kuwapa picha nzuri ya namna ambavyo Taifa lipo, lakini hamjui wananchi wa chini wanasema nini kuhusu ninyi; mtawajua kama mtaruhusu wing hii ya pili ifanye kazi yake ya kisiasa vizuri, mtasikia malalamiko ya wananchi na mtajua mmekosea wapi na mjirekebishe wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani Serikali inapaswa kutimiza wajibu wake vizuri katika kuhakikisha kwamba inasimamia misingi ya demokrasia katika Taifa hili ili tusije tukaliingiza Taifa hili katika matatizo. Nchi hii yetu sote; tumezaliwa hapa na tutafia hapa, tunapaswa kuipigania katika nyanja zote ili tuhakikishe kwamba wote tunaishi maisha ya furaha katika Taifa la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la usalama wa kiuchumi katika nchi hii. Wananchi wanaumia. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inasema kwamba hali ya uchumi na usalama wake uko vizuri. Lakini leo wafanyabiashara hawana uhakika na biashara zako; wafanyabiashara hawajui kwamba kesho kutatoka tamko gani na nani atazungumza nini. Wakulima vile vile hawajui kwamba wanaishi maisha gani yenye uhakika na wafugaji vile vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inatuonesha kwamba kuna utulivu wa kiuchumi. Leo benki hazikopeshi kwa sababu hazina uwezo wa kukopesha; tunaambiwa kwamba benki zina mitaji na zipo vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Serikali pia katika eneo hili ijiangalie na iangalie vizuri kwamba tulipokuwa na tulipo pana tofauti gani, na kwa nini kulikuwa na hali nzuri ya watu kukopa na kukopesheka na kulikuwa na utulivu wa kufanya kazi. Leo maafisa wa TRA hujui ni wakati gani watafilisi mwananchi, leo hawajui ni wakati gani benki itafilisi wananchi kwa sababu wananchi hawana uwezo wa kulipa. Sasa katika sura hii tunaendeshaje hii nchi na huu uchumi wa viwanda tutaupata kwa namna gani? Ni lazima Serikali ijipime sana katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la utalii; Mkoa wa Kilimanjaro umebahatika kupata Mlima Kilimanjaro. Mlima ambao ndio unaowakilisha Taifa hili katika sura ya vivutio vya utalii ambavyo vina heshima duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeomba Mkoa wa Kilimanjaro Mji wetu wa Moshi upate hadhi ya kuwa Jiji. Nadhani Serikali ingetusikia kilio chetu; haiwezekani Mkoa ambao una kivutio cha utalii ambacho ndio kinachochangia pato kubwa katika sekta ya utalii kuliko kivutio kingine
chochote kile ishindwe kupata Jiji kama yalivyo Majiji mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali isikie kilio chetu cha kufanya Mji wa Moshi uwe Jiji ili tuweze kuongeza shughuli za utalii katika Mkoa wa Kilimanjaro ili tuweze kuongeza watalii na kuongeza pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nilikuwa naomba Serikali isikie kilio chetu cha kukarabati uwanja wa ndege wa Moshi, uwanja ambao umejengwa tangu wakati wa malkia. Lakini leo imekuwa ni kazi kweli kukarabatiwa mpaka umekuwa ni gofu; eneo lile sasa lipo katika mazingira hatarishi na inawezekana hata watu wakalivamia. Kama lingejengwa ni eneo ambalo lingeinua sana utalii kwani ni uwanja wenye
uwezo wa kujiendesha wenyewe. Nilikuwa naomba Serikali itazame kama ina dhamira kweli ya kuinua utalii katika taifa hili na kuinua pato la taifa kupitia utalii na pia kusaidia wananchi wa Kilimanjaro kujiinua katika uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la viwanda. Viwanda vingi vya Moshi vimekufa, na ni vile ambavyo vilibinafsishwa kwa sera mbovu ya ubinafsishaji ambayo imeumiza sana uchumi wa viwanda katika Taifa hili. Sasa naiomba Serikali isimame katika maneno yake,
kwamba kwa muda mfupi uwezekanavyo viwanda ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa na waliobinafsishiwa wakashindwa kuvifanyia kazi basi wanyang’anywe kama hawawezi kuendelea kuviendeleza na kama wanaweza kuviendeleza waviendeleze ili wananchi wapate ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu viwanda zaidi ya kumi na tano Mkoa wa Kilimanjaro vimekufa lakini tunalalamika hakuna ajira; tunaanza kufikiri ajira za kupitia kwenye mifuko ya vijana na akinamama ya Halmashauri, tunawaza kufikia ajira kupitia Mfuko wa Taifa wa Ajira wa Vijana lakini tuna viwanda ambavyo vipo, vilikuwa vinatengeneza ajira leo vimekufa na Serikali haioneshi jitihada zozote za kuhakikisha ajira zinapatikana. Naomba viwanda vile vifanyiwe kazi, vifunguliwe mapema ili viweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.