Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kupongeza kwa dhati kabisa Serikali kwa mambo manne makuu yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, Serikali kutekeleza uamuzi wa miongo minne iliyopita wa kuhamia Dodoma, naipongeza sana. La pili, viongozi wa sekta za muungano na zisizo za muungano kuendeleza mashauriano chanya yenye nia ya kudumisha Muungano. Tatu, Serikali kukamilisha Kituo cha Kuhifadhi Taarifa na Takwimu za Serikali (Government Data Centre) ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali. Hii ni pamoja na program ya kielektroniki ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na ahadi za Rais na viongozi wakuu wengine wa Kitaifa. La mwisho, hatua za kuboresha usimamizi kwenye sekta za mazao ya biashara ya korosho, pamba na tumbaku. Hili nampongeza kwa dhati sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kauli mbiu ya HAPA KAZI TU inaendelea kuthibitika, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina mchango katika maeneo machache, nikianza na afya. Uamuzi wa Serikali wa kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya ni wa takribani miaka 10 iliyopita. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu haijasisitizwa wito huo wa kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Nilitegemea Serikali ije na mkakati wa makusudi wa kusaidia Halmashauri angalau vijiji vitano kila mwaka viwe na zahanati na angalau kata tatu kila mwaka zipate kituo cha afya. Angalau hiyo inaweza ikaonesha utekelezaji lakini naamini hata kwenye bajeti ya Wizara ya Afya mkakati huo haupo. Naomba sana kama uwezekano upo wa kurekebisha hapo, tuweze kufanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, sekta ya kilimo. Sisi kule Sikonge tunalima sana tumbaku. Kitu ambacho nataka niongelee hapa pekee ni kiwanda cha kuchakata tumbaku cha Morogoro. Kiwanda hiki kilibinafsishwa na waliopewa kiwanda hiki na Serikali ni TLTC na Alliance One ambao kwa bahati mbaya sana hao nao ni wanunuzi wa tumbaku. Kwa hiyo, huwezi kupata good governance na fair competition ambapo wanunuzi hawa wawili wanamiliki kiwanda halafu kuna kipengele cha sheria ambacho kinawalazimisha wanunuzi wote, wao wenyewe pamoja na wengine kwamba hawaruhusiwi kusafirisha nje tumbaku hadi ipelekwe pale kwenye kiwanda cha Morogoro kuchakatwa. Kwa hiyo, ina maana kwamba, hiyo inazuia fair competition kwa wanunuzi wengine ambao sio wamiliki wa hicho kiwanda kwa sababu kuna uwezekano wakapewa rate ambazo ni tofauti na zile ambazo wanazitumia wao wenyewe ambao ni wamiliki wa kiwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suluhisho hapo kwa Serikali ni moja tu, aidha kukitaifisha kile kiwanda kirudi mikononi mwa Serikali au apatikane mtu mwingine akinunue tena kile kiwanda ambaye sio mnunuzi wa tumbaku au kufuta kile kipengele cha sheria ambacho kinalazimisha wanunuzi wote kuchakata tumbaku pale ili wengine wapate sehemu nyingine ya kupeleka kuchakata tumbaku badala ya pale. Hapo ndiyo wanunuzi wengi wa tumbaku watakuja Tanzania hapa na mkulima atanufaika kwa kuongeza ushindani kwenye zao la tumbaku, huo ni ushauri wa pili.
Mheshimiwa Spika, wa tatu ni kwenye eneo la utawala. Wilaya yangu ya Sikonge ina eneo kubwa sana. Kuna watu kule Matagata ili aweze kufika Sikonge Makao Makuu ya Wilaya analazimika kutembea kilometa 400. Ile Tarafa ya Kitunda ina wakazi 85,000 na wako mbali kwelikweli
na Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, mimi nilisoma Marekani, niliwauliza Abraham Lincoln alitumia kigezo gani kikubwa kuanzisha county ambayo ni sawasawa na wilaya zetu hapa? Alitumia uwezekano wa mtu kutembea na chombo cha usafiri cha kawaida cha wakati ule, farasi, atoke nyumbani kwake saa 12.00 asubuhi, aende Makao Makuu ya Wilaya amalize shida zake arudi nyumbani kabla jua halijatua, ndiyo kigezo ambacho alitumia. Mheshimiwa Spika, kama usafiri wetu wa kawaida ni baiskeli, tunamtegemea na mwananchi wa Matagata atoke Matagata aende kwa Mkuu wa Wilaya akamalize shughuli zake arudi nyumbani kabla jua halijatua. Ingawa kigezo kile hatuwezi kukifikia basi tumpunguzie mzigo huyu mwananchi. Kwa hiyo, ombi letu litakapokuja kwa Waziri Mkuu la kuanzisha Wilaya Mpya kwenye Tarafa ya Kitunda naomba lipate support ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la nne ambalo napenda nilizungumzie ni elimu. Tunaomba Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha tunakuwa na usawa wa uwiano wa walimu na wanafunzi katika nchi nzima. Ipo mikoa hapa Tanzania ina ziada ya walimu, ipo mikoa kama Tabora ina upungufu mkubwa sana wa walimu. Kule ambako kuna ziada inatakiwa isawazishwe na kule ambako kuna upungufu ili ule uwiano wa 1:40 upatikane kwa mikoa yote badala ya mikoa mingine kuwa na walimu wengi mpaka na wa ziada ambao hawana kazi, wanasukana nywele tu kwenye shule na mikoa mingine ina upungufu mkubwa wa walimu. Naomba sana hili lisimamiwe na Waziri Mkuu, maana Wizara ya Elimu
wameshindwa kulitatua kwa miaka 10 iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka nilizungumzie ni eneo la barabara. Sisi kule kwetu tuna barabara mbili za kiwango cha changarawe ambazo ni muhimu sana. Barabara ya Ipole–Rungwa kilometa 182 na Sikonge–Mibono–Kipili kilometa 280. Barabara ya Ipole–Rungwa ilitengenezwa tu pale ambapo Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Sikonge akatembelea Kitunda, tarehe 10/3/2010. Akatoa amri, nataka hii barabara itengenezwe kwa vyovyote vile. Wewe Regional Manager hakikisha unapata hela za kutengeneza hii barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba basi Rais apange safari ya kuja Sikonge ili aende Kipili ili na hiyo barabara ya Sikonge – Kipili nayo itengenezwe. Maana hao watu wa Wizara ya Ujenzi wanatwambia hakuna hela.
Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapo. Ahsante sana.