Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na watendaji wote, nijikite katika kulifikisha hili mbele yenu kwa maana ya hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa ule wa kumi na moja na kwa afya ya kikao hiki naomba nipasome hapa. “Ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini, hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sharia, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa wote nchini kujenga utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa za kuunganisha watu watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi”.
Mheshimiwa Spika, hili limebeba ujumbe wote ambao nilikuwa nakusudia kuusema. Pia nimejaribu kufuatilia hotuba ya Kambi ya Upinzani nikakutana na kauli moja na mimi niliiona sio mbaya, ambayo wanasema kwamba:-
“Wanazuoni wanasema kutofautiana kifikra ni afya ya akili na ili uvumbuzi utokee lazima kuwe na fikra mbadala.” Mheshimiwa Spika, mimi naona niende mbele zaidi na ili twende mbele tusipinge kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, eneo la kwangu kwa maana ya Katavi nikizingatia sekta ya utalii ambayo imeongelewa vizuri katika hotuba ya Waziri Mkuu, naiona sekta ya utalii na usafiri wa anga kama watoto pacha. Utakapoboresha usafiri wa anga unaboresha eneo la sekta ya utalii. Kwa misingi hiyo, hata nilipokutana na habari ya nchi kununua ndege, mara ya mwisho katika kutafuta habari nilikutana na nchi moja ya Ethiopia, uchumi wake mkuu umejikita katika maeneo yafuatayo, ukiacha kilimo, kuna suala la usafiri wa anga, wamekuwa wakifanya vizuri na kuibua fursa nyingine kwa kupitia usafiri wa anga. Leo tunapotamani hata kiongozi wa nchi atoke akaiangalie dunia anakwendaje huko kwingine? Ni lazima atakwenda kwa kutumia usafiri wa anga. Kwa hiyo, ninapoona nchi yangu inakwenda kuzungumzia habari za usafiri wa anga suala hilo naliunga mkono na kupanga ni kuchagua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mtu mmoja hakujenga nyumba, hakufanya kitu kingine, yeye alianza kwa kununua mziki. Kwa kupitia mziki ilimletea utulivu wa fikra akaweza kujipanga akaibua fursa mbalimbali na baadaye akajenga nyumba na vitu vingine vyote vikaendelea. Kwa hiyo, kupanga ni kuchagua. Kila mmoja anaweza akaamua anaanza na kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikizungumzia suala hilo la utalii kwa maana ya Katavi, nimeshukuru katika hotuba ya Waziri Mkuu amezungumzia habari ya kupanua wigo. Eneo lile ni kweli tuna mbuga nzuri ya Katavi lakini pamoja na kuwa na uwanja mzuri, ukiuliza ni kwa nini uwanja ule wa Katavi haufanyi kazi tunaambiwa tatizo hakuna ndege zinazokwenda kule. Mimi niombe, kwa maana ya ndege hizi ambazo zipo, zianzishiwe safari ya kwenda Katavi ili kuibua fursa hiyo ya utalii. Kama kuna tatizo linalotokana na suala la mafuta au kutokuwepo kwa gari la zimamoto, naiomba Serikali yangu sikivu iangalie suala hilo kwa sababu upande ule tukifanya vizuri inakuwa sio kwa ajili ya wana Katavi tu ni
kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo naomba nije upande wa sekta ya madini. Nilifarijika nilipokutana na habari ya kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo. Najua fursa hiyo ya uchimbaji madini na hasa tunapoelekeza kwa wachimbaji wadogo, baadaye watakuja kuchangia pato la Taifa. Kule kwangu kuna maeneo ya Dirif na Kapanda, niombe isiishie kwenye kuandika kwenye vitabu hivi kwamba maeneo hayo yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, twende kwenye hatua ya mbele zaidi ya kuhakikisha kweli maeneo hayo wanapatiwa hao wachimbaji wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna suala zima la kuongeza thamani kwa maana ya madini lakini hata kama tutaongeza thamani naomba twende mbali zaidi na suala la masoko pia. Watu hawa tunaweza tukawahamasisha wakachimba, wakaongeza thamani lakini inapokuwa hakuna soko naona kama ni tatizo pia.
Mheshimiwa Spika, nikitoka kwenye sekta hiyo naomba niende kwenye sekta ya afya. Eneo la sekta ya afya nimeliona likizungumziwa humu kwa maana ya afya ya mama na mtoto mimi naomba niende mbali zaidi. Tunapozungumzia habari ya afya ya mama na mtoto naomba sana ilenge pia kwenye kupiga vita mimba za utotoni na hili naliona ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule kwangu Katavi taarifa zinatuambia 45% ya mimba za utotoni zinatoka kwetu Katavi, naliona hili ni tatizo. Kwa hiyo, naomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, mazingira yaendelee kutengenezwa, namna ya kuirudisha jamii hii kulitambua hili kwamba ni tatizo, inapokuwa mama yeye mwenyewe ni mtoto halafu anakuwa na mtoto hata mipango mingine ya kitaifa hatutaifikia, kwa sababu mama mwenyewe anakuwa hajitambui na huyo mtoto atakuwa katika mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kulisema hilo, naomba pia niende katika suala la elimu. Nafarijika kusikia habari ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu lakini naomba twende mbali zaidi. Katika eneo hili hili la elimu, fursa ambayo nimekuwa nikiiona na wakati huo Watanzania hatufanyii kazi fursa hii kwa maana ya lugha adimu ambayo ni Kiswahili, mimi napata tabu. Huko duniani watu wengine wanaajiriwa kwa kupitia Kiswahili tu. Kuna nchi moja watu wake wengi wanarudisha pato katika nchi yake kwa kupitia wasomi mbalimbali kwenda katika maeneo mbalimbali duniani wanakusanya fedha na kuzirudisha kwenye nchi yao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Watanzania wenzangu katika eneo hili hili la elimu, Kiswahili tusikibeze. Kiswahili kitatoa ajira, kitatoa fursa kwa watu wetu, suala ni kujipanga vizuri. Tunapoambiwa kama ni wazungumzaji wazuri wa Kiswahili lakini unakuta nchi nyingine ndiyo
wanafanya kazi na wanakuwa mbele wakati Watanzania tuko nyuma mimi hapo nakuwa sijisikii vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa suala la michezo. Michezo ni afya lakini shida moja ambayo naiona kwa sisi Watanzania, muda umekuwa ni mrefu tunakuwa kama
kichwa cha mwendawazimu na sababu ni nini? Ni mipango yetu kuwa ya muda mfupi, mara nyingi tunakwenda na mipango ya zima moto. Naomba turudi kwenye mipango endelevu, tuwekeze katika eneo hili. Akina Bayi wa miaka hiyo wako wapi? Tunatamani kuwaona watu hao katika maeneo yote iwe ni riadha au mpira wa miguu. Nimefarijika kuona kwamba tutarudi kuendeleza michezo huko mashuleni na kwenye shule za msingi lakini tuendelee kuwekeza na ukitaka fedha, tumia fedha.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naendelea kusema naunga mkono hoja.