Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwa ufupi dakika tano. Nianze kwa kumshukuru mdogo wangu Mlinga kwa kunitaja pengine na mimi kesho naweza kuwa mahabusu kwa amri ya Makonda. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie tu na mimi kwenye sehemu ya dawa za kulevya. Niliwahi kuchangia wakati nazungumzia kuhusu bangi na mirungi, nilieleza Taifa hili lina vyombo vya ulinzi na usalama, tuna Polisi, Usalama wa Taifa, Majeshi, vyombo vinavyoweza kutujua tabia zetu na vina utaalamu wa kuweza kumfuatilia mtu na kugundua kama kweli hiki kilichosemwa anahusika nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata mshtuko sana kwa hiki kinachoendelea, ni haki yangu kuzungumza kama Mbunge, kama Waziri Chikawe akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alisema ana orodha ya wauza unga, ameingia Mheshimiwa Kitwanga akatuaminisha mwezi mzima anataja, amewapa siku 21, hawakutaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Taifa linafanyia kazi orodha ya Makonda, napata wasiwasi. Hii ndiyo tulikuwa tunaisubiri awamu zote kuanzia kwa akina Marehemu Amina Chifupa kwamba hawa ndiyo waliofanyiwa uchunguzi wakakutwa kweli wanauza dawa za kulevya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli ndivyo, basi hili Taifa tunakokwenda hatuendi sawasawa. Hivi kweli Watanzania tunaambiwa kuna msururu wa wauza dawa za kulevya wamekamatwa anatajwa Chid Benz na Ray C, watu ambao Taifa hili limeingia gharama ya mabilioni kumsaidia Ray C na watu walichanga kwenye M-pesa, mgonjwa unamchukua unamtia mahabusu, hatuko serious kumaliza suala la dawa za kulevya. (Makofi)
Mhehimiwa Mwenyekiti, hili tuongee lugha moja wote kwa pamoja kuondoa hata uvyama, wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata wengine walio vigogo wa kukamata wenzao wanashinda nao na wanawasafirisha kwenda Marekani. Kwa nini vyombo vya ulinzi na usalama visimhoji Makonda, mtu ambaye siyo mfanyabiashara ameenda Marekani, Paris, Dubai kwa mshahara wa u-RC huu? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani ndugu zangu hiki kitu lazima tupate muda tuzungumze. Mheshimiwa Rais mimi nakuunga mkono, inawezekana Mheshimiwa Rais ana uchunguzi sahihi kuliko wa Makonda. Kama amesema kila mtu akamatwe hata mke wa Rais akamatwe na Makonda aanzie wa kwake aliowapangishia majengo. Kwa nini wa kwake wako nje na wametajwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Dar es Salaam mitaa ya wauza unga inajulikana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Musukuma, muda wako umemalizika.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Makao Makuu ya CHADEMA ndiyo wauza unga wamejaa pale mateja.
Tunaenda kuchukua mateja tunajaza magereza.