Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niunge mkono hoja za Kamati. Kamati imeeleza mambo mengi na ya msingi, isipokuwa tatizo ni moja, kwamba hizi hoja ambazo Kamati wanazieleza katika Bunge hili la Taarifa za Kamati kwa mwaka mmoja, Kamati hizi hizi zingekuwa zinajenga hoja kama hivi wakati wa bajeti nadhani tungekuwa tuko mbali sana. Lakini inapofika wakati wa bajeti Kamati zote zinajigeuza, badala ya kusimamia na kuishauri Serikali kama ambavyo leo imefanya, zinajigeuza zinakuwa caucas ya vyama, hii ndiyo inakuwa changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukipitia taarifa ya Kamati, imejitosheleza kwa kiwango kikubwa ingawa yako maeneo mimi binafsi ningetaka kupata ufafanuzi zaidi. Kwa mfano kwenye ukurasa wa 33 wa Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii, ukurasa wa 33 kipengele (b) anasema, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kuna ufisadi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mwenyekiti wa Kamati angeeleza aina ya ufisadi huu anayotaja kwenye ukurasa wa 33 ni ufisadi wa nini. Ni kiwango gani cha fedha ambacho yeye anafikiria kwamba watu wamechukua, wameiba na wameiba katika mradi upi. Kwa hiyo, ukiangalia hii taarifa iliyoandikwa hapa katika ukurasa wa 33 haijitoshelezi, imesema tu kwamba, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kuna ufisadi. Kwa hiyo, naomba Mwenyekiti wa Kamati utakapokuja kuhitimisha hoja yako uje na maelezo kwamba ufisadi huu ulioueleza katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ni ufisadi wa aina gani ili Bunge na Watanzania tuweze kufahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu suala la ongezeko la ugonjwa wa kansa. Ukisoma taarifa za Wizara, ukiingia kwenye website ya Wizara ya Afya, ukasoma taarifa inaumiza sana kwamba ugonjwa wa kansa unaenea kwa kiwango kikubwa kabisa. Taarifa zilizopo kwa mujibu wa WHO ambayo taarifa yao waliitoa mwaka 2002 ni kwamba kila mwaka zaidi ya watu 21,000 Tanzania wanapata ugonjwa wa kansa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine taarifa inaeleza kwamba ugonjwa wa kansa za uzazi takribani wanawake 7,515 wanapata ugonjwa wa kansa ya uzazi na kati ya hao 6,009 wanafariki kila mwaka kutokana na kansa ya uzazi. Kwa hiyo, ningetaka kujua na Kamati ingetueleza wao kwa kuwa wanaisimamia na kuishauri Serikali, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na ugonjwa huu ambao kwa sasa unaenea kwa kasi kubwa kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa za kansa namna unavyoenea na namna unavyosababisha vifo ni jambo ambalo linasikitisha sana kuona hatua ambazo Serikali wanazichukua. Lakini kinachosikitisha zaidi ni kuona kwamba hata hiyo Hospitali yenyewe ya Ocean Road katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kile kiwango cha pesa ambacho ilitengewa hiyo pesa haikupelekwa, kiwango kilichopelekwa ni kidogo sana. Kwa hiyo, inaonesha kwamba dhamira ya Serikali ya kupambana na ugonjwa huu ambao ni hatari sana ni ndogo sana, lakini WHO wana-estimate kwamba tunakoelekea zaidi ya asilimia 25 ya Watanzania tuko hatarini kupata kansa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba karibu kwenye Watanzania wanne, mmoja yuko hatarini. Ni jambo la hatari na ni jambo very serious, tunahitaji Kamati kwa kuwa ndio inaisimamia Serikali ije itueleze wapi Serikali imekwama katika kuhakikisha inapambana na ugonjwa huu wa kansa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Uganda naona wamechukua hatua kubwa kabisa na si vibaya Waziri akaenda akajifunza kwa zile measures ambazo Uganda wamezionesha na namna wanavyopambana imeonesha kwamba is a serious issue na national problem na Rais ame-declare kabisa kwamba kansa ni tatizo la Taifa na wameamua kupambana nalo. Sidhani kama Tanzania tumefikia kwenye level ya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la ugonjwa wa UKIMWI. Sisi tunaotoka vijijini siku hizi ugonjwa huu ni kana kwamba umehama mjini umekwenda vijijini. Hali ya maambukizi vijijini ni makubwa kuliko hata mijini mimi nasema. Ukienda kule vijijini, mimi natokea Lindi, ukienda Lindi vijijini kabisa ukielezwa idadi ya watu wanaotumia dawa kule vijijini kabisa, inasikitisha sana. Inaonesha dhahiri kwamba inawezekana kuna tatizo kubwa la elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huu ambayo wanayo wananchi wa vijijini?
Kwa hiyo, mimi naomba Kamati, kwasababu, ninyi ndio wenye hoja mtueleze pia, kwamba katika ushauri wenu kwa Serikali, Serikali wana mkakati gani wa kuongeza utoaji wa elimu vijijini? Suala la ugonjwa wa UKIMWI sasahivi limekuwa kubwa vijijini kuliko mijini; na hii ni kwa sababu, wananchi kule vijijini wamezoea kuishi maisha yao yale ya kawaida. Inasikitisha sana, ukiwa kwenye vikao vya Halmashauri ukapewa takwimu za ugonjwa wa UKIMWI katika Halmashauri inasikitisha na inatisha sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nimeshiriki Vikao vya Kamati ya UKIMWI juzi juzi tu kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Lindi, taarifa iliyopo ni mbaya sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba hili ulichukue kwamba hali ya maambukizi ya UKIMWI vijijini sasa hivi ni kubwa zaidi kuliko hata mijini. Sijui kama takwimu zako zinasemaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni suala la Bodi ya Mikopo. Tulizungumza hapa wakati wa bajeti kwamba bajeti hii ni ndogo, lakini pia, utaratibu unaotumika kupima vigezo vya nani apate na nani akose bado ni utaratibu ambao hauridhishi. Kwa hiyo, tunaomba, Kamati muendelee kuishauri na kuisisitiza Serikali kwamba katika mwaka na ninadhani Kamati mngekuja na orodha ama idadi kwamba ni wanafunzi wangapi ambao walistahili kupata mikopo lakini wamekosa katika mwaka wa masomo 2016/2017. Idadi ni kubwa na waliokosa wengi ni maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda vijijini unawakuta watu ambao walifaulu kwa division one, division two, lakini wanatoka kwenye familia maskini wako vijijini wamekosa mkopo. Kwa hiyo, Kamati tunaomba mngekuja na takwimu walao mkatueleza kwamba kukosekana kwa mikopo kumeathiri kiwango gani cha vijana wetu wa Kitanzania katika mwaka wa masomo wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu umekwisha, nakushukuru na ahsante sana.