Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi; wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kwa moyo wa dhati kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama, mimi mwenyewe, Dkt. Ndugulile ndio tulioanza kushughulikia dawa za kulevya humu ndani kwa kutunga sheria ya kupambana nao, sio kutafuta sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nizungumze yafuatayo, sipingani na watu wanaopingana na suala la kupambana na dawa za kulevya, wale wote wanaotaka kupambana na dawa za kulevya wasimuongopee Rais, tumshauri Rais amteue Kamishna wa chombo cha Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ambacho tulipitisha sheria yake humu ndani na nilisema kabisa nimempongeza dada yangu Jenista Mhagama na Dkt. Ndugulile sisi ndio tulianza huu mchezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tutakapohakikisha hiki chombo kinapata Kamishna kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais tutakamata wale wanaoingiza dawa za kulevya, wale mapapa, hao wanaokamatwa sasa hivi waathirika wanatakiwa wapeleke Muhimbili na Mwananyamala wakapate tiba, wale ni waathirika sio kwenda sero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ndio nililotaka niliseme na mdogo wangu Makonda akitaka kupambana na dawa za kulevya aende magerezani akakutane na akinamama Leyla atamwambia mapapa ili tuungane wote kwa pamoja na tunamkaribisha katika hili lindi kuhakikisha nchi yetu inapambana vikali dhidi ya dawa za kulevya kwa sababu mimi mwenyewe mdogo wangu anayenifuata yupo Mwananyamala anakunywa dawa methadone. Kwa hiyo, ninachokisema nina uchungu nacho na nimekifanyia utafiti wa kina na nilileta maelezo binafsi katika Bunge hili Tukufu na ninashukuru Mheshimiwa Jenista akalisikiliza alipoingia tu katika hiyo wizara tukaleta muswada na tukatunga sheria nzuri sana ambayo leo hii katika watu watakaokutwa nyumbani kwao wanafunga zile dawa za kulevya kuna fine lakini wanaenda jela zaidi ya miaka 20. Kwa hiyo, tulianza hiyo vita kwa vitendo kwa kutunga sheria kali sio kwa kukamata waathirika ambao wanatakiwa waende wakanywe dawa kama ambavyo inafanyika hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tangu mwaka jana mwezi wa kumi na moja hivi vituo vinavyorudisha watu katika hali yao ya kawaida, hawa waathirika ambao wapo sero sasa hivi, hivyo vituo tangu mwaka jana havijapokea watu wapya. Ningependa kujua kwa sababu gani hawajapokea watu wapya na inasemekana dawa ya methadone haiendi kwa wakati. Lakini pia mkifuata ile hoja yangu binafsi niliiambia Serikali ihakikishe hivi vituo viende nchi nzima, tusiishie Dar es Salaam peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunajua tatizo la dawa la kulevya yanachangia sana katika maambukizi mengine ya magonjwa ya HIV. Kwa mfano, watu tu wa kawaida maambukizi ya ugonjwa wa HIV ni asilimia 5.1; kwa watu ambao wanatumia dawa za kulevya ni asilimia 25 mpaka 50. Kwa hiyo, sio issue ya kuwapeleka waathirika sero, hili janga ni zito. Kwa hiyo, mtu anaetaka kupambana tupambane na mapapa na sio waathirika ambao wanawekwa sero badala ya kuwapeleka katika vituo vya kurudisha katika hali yao ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na haya ni maazimio ya UN ya mwaka 2006 ukitaka kupambana na dawa za kulevya pambana na watu wale mapapa wanaoleta nchini, hilo ndio jambo la msingi. Kwa hiyo, nilitaka niliweke hili sawa; tusifanye siasa katika vita ya dawa za kulevya. Tusimwongopee Rais kwa kutaka kuhakikisha vyeo vyetu, tumwambie ukweli na ili tumsaidie Rais amteue Kamishana wa hii Tume maana tangu tulipoipitisha hii sheria hiki chombo hakina Kamishna. Hilo ndio jambo la msingi ili tuungane kwa pamoja tuhakikishe tunatokomeza vita ya dawa za kulevya hapa katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imesema Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya haina fedha, ni aibu kwa nini hawa watu wengine wasiojua haya mambo wasifanye vitu kienyeji kama hatuwapi pesa za kutosha, tuipe hii Tume pesa ipambane na huu muziki kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna Mahakama ya Mafisadi, niliiomba Serikali hizi kesi zinachukua muda mrefu, kuwe na Mahakama Maalum ambayo itashughulika na hii mipapa ambayo wako ndani na haipelekwi mahakamani. Kuwe na Mahakama Maalum inayoshughulika na hizi kesi za dawa za kulevya, hilo ni jambo la msingi sana katika Taifa letu, lakini sio kutafuta sifa na sio kutaka kuhalalisha vyeo vyetu pasipo sababu katika janga ambalo linaharibu kizazi cha watu cha vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie kabisa Waziri anayehusika, hivi sasa hivi wale mapapa wanaoingiza wanataka kuanza kuangalia soko kwenye hizi centre zinazotoa huduma yaani dawa za methadone, wale ambao Serikali imeamua kuwarudisha katika hali ya kawaida wao sasa hivi wanataka kwenda kuwauzia dawa katika vile vituo. Serikali ina mkakati gani ya kuhakikisha hawa watu hawafanyi hivyo? Ni mbaya sana lakini sasa hivi baada ya kuona hii sheria kali na tumeweza kuhakikisha kwenye ile sheria zile kemikali na zenyewe tumeziingiza katika sheria kuwa ni moja ya makosa, sasa hivi zile kemikali hawa vijana wanatengeneza hapa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mdogo wangu Makonda watafute wale vijana wanaotengeneza hizi kemikali tuanze ku-deal nao, wanatengeneza viwanda vidogo vidogo halafu wale waathirika sasa tuwapeleke kwenye vituo tusiwaweke sero. Ahsante sana.