Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi; nami nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia neema kubwa ya uhai na uzima na afya na tukawa hapa. Nimpongeze kaka yangu aliyemaliza kuzungumza Mheshimiwa Maji marefu kwa kutimiza ada muhimu sana. Mafunzo yanasema ukitendewa jema basi mshukuru yule aliyekufanyia jema mpaka ahisi kwamba ameshukuriwa. Naamini Waheshimiwa Wabunge na wote uliowashukuru walihisi kwamba umewashukuru na sisi tunamshukuru Mungu kukurejesha tena hapa hata tukawa na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, babu zangu wa Kimwera wanasema hizi Kamati hizi they have seen it all. Kwa kweli Kamati zimefanya kazi, Wenyeviti wao wametuletea hapa taarifa, hakuna kilichobaki humu; na wachangiaji walionitangulia nao wamechangia, wamesema waliyoyasema, sasa hayo nitakayoyasema mimi itakuwa ni nyongeza tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kuchezea elimu. Elimu nchi hii tunaikoroga, elimu nchi hii tunaichezea na hatujiamini bado kama elimu ndiyo ufunguo wa maisha ingawa huo msemo upo kila mahali, elimu ni ufunguo wa maisha, lakini matendo yetu hayaendani na hilo. Naomba tu kwa msisitizo kabisa, hebu Serikali ibadilike. Waheshimiwa Wabunge humu wameshasema sana kuhusu suala la elimu, its time now.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya CCM miaka yote hiyo iliyopita ni CCM tu hakuna ya Rais huyu, Serikali ya CCM, sasa ibadilike, ione kwamba ina jukumu la kusimamia elimu na elimu ni kweli iwe ufunguo wa mambo yetu yote yanayofuata. Dada zangu mmepewa Wizara hili tutawapima tu! Kwa hiyo, Profesa na Msaidizi wake wajipange kwenye elimu, mabadiliko tunayataka, yenye uweli si haya ya kutubadilishia mara mtaala, mara nini, hapana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la UKIMWI; na hili nalisema kwenye kipengele cha utegemezi. Wataalam wameimba kuhusu madhara ya kutotumia dawa ipasavyo. Mgonjwa wa UKIMWI ukishamkatizia dozi yake, iwe ile ya dozi yenyewe au ile inayoitwa dawa za kuondoa magonjwa nyemelezi, unamuathiri zaidi kwa sababu vile vijidudu vinajenga usugu; sasa tunashangaa nini inapoonekana kwamba haya maradhi hayaondoki na maambukizi yanazidi kwa sababu hata hiyo tiba yenyewe hatuifanyi swa sawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utegemezi; kila mahali Kamati imetuambia hapa; kuanzia utafiti, kutoa hizo huduma zenyewe za madawa tunaambiwa wafadhili ndio wafanye hivyo. MCC hiyo arijojo, imeshaondoka sasa sijui tuna nini mbadala kwenye suala hili ambalo kwa kweli ni janga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake taasisi zetu za huduma muhimu haziko sawa. Tunajua hali za hospitali zetu, zahanati zetu, vituo vyetu vya afya, wamesema hapa na Kamati zimesema; lakini pia tunajua hali ya shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miezi kadhaa nilipita mahali kule Jimboni kwetu, kuna eneo Kaskazini kunaitwa Bweni nilikuwa nakwenda Bweni sasa hapo katikati unapita mahali panaitwa Kirongwe. Tulikuwa tunapita kwa haraka kwa gari lakini nikaona watoto kama wanacheza cheza hivi kwenye majengo mabovu sana. Sasa nikawa nauliza wale wenzangu, hiki hapa ni nini? Wakaniambia ndiyo shule ya msingi Kirongwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema watoto wanakuja kwenye majengo haya? Hizi ndiyo shule zetu lakini hapa Serikali Kuu inatuambia kwamba Halmashauri ndizo zishughulikie hizo, Halmashauri ambazo tayari zimeshaondolewa uwezo wa kusimamia hayo kwa maana ya kupunguziwa vyanzo vyao vya mapato. Sasa sidhani kama kweli tunataka kuleta maendeleo kwenye jamii hii kwa sababu mambo yetu maneno ni mengi kuliko utekelezaji na matendo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wimbo huu wa ufinyu wa bajeti na sasa umekuwa wimbo wa kutopeleka pesa zilizopangwa, sasa kuna haja gani ya kufanya hii budgeting process?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkutano uliopita nilisema hapa kwamba hivi hii bajeti ya nchi yetu kwa nini isiwe mchakato unaojitegemea, yaani uliounganika yaani intergraterd process ya budgeting? Ndiyo maana tunapata haya matatizo. Tunazungumzia hiyo semina elekezi, semina elekezi si lazima tuambiwe A, B, C lakini semina elekezi pia isaidie kupanga pia vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Mawaziri wote wakikutanishwa pamoja waka-brainstorm kwa pamoja jamani vipaumbele mwaka huu ni nini? Haya matatizo, kwamba kule hakukupelekwa, huku hakikutolewa hayatotokea tena, au angalau yatapungua kwa asilimia kubwa; lakini kila mtu hapa anakaa peke yake, anasema ana vipaumbele, vipaumbele vyenyewe vinakuwa zaidi ya 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila anayesimama hapa kipaumbele, kipaumbele mwisho wake tunaimba hii kila siku nenda rudi ni yale yale hatubadiliki, tatizo ni nini jamani? Wasomi ndio hao na kama kuna Serikali imejaa maprofesa ndiyo hii, hebu tuone basi mabadiliko. Hizo elimu na ujuzi wenu wekeni kwenye vitendo ili tuone kweli ninyi mnataka, mnaambiwa mainjinia; tulikuwa tunawaita ma-spanner boys; basi na wao wafanye kazi ya vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa pia suala la kutaka ufafanuzi kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa madawa; tena hili mimi naomba litolewe maelekezo kweli kweli. Huo ufafanuzi uwe ufafanuzi wa kweli. Kwa sababu Serikali ikizungumza kupitia Mawaziri wake iwe wa Afya au wa TAMISEMI unaona pepo kabisa kwenye zahanati, lakini wakisimama wale watumishi wetu walioko kule ma-DMO na wengine unaona ufukara uliokithiri, tatizo ni nini hapa? Mawaziri wanatuambia madawa yamejaa, sijui basket fund imeleta kila kitu, DMO akisimama akikwambia unaona kabisa ana-negative wala hata siyo zero, hili tatizo liko wapi? Hebu watupe maelekezo ya kutosha kwamba dawa zipo au hazipo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie kwa kusema kwamba na mimi ni-declare interest na mimi ni Mwalimu. Dada yangu Mwalimu Susan amesema Walimu wamedhalilishwa kiasi cha kutosha na kuonewa kiasi cha kutosha, sasa huu msemo unaishia kusema na tunasema sasa basi. Hebu Walimu wa nchi hii wapewe hadhi yao, wapewe haki zao, Walimu hawa wanadhalilika. Niliwataja siku moja hapa Walimu walionifundisha toka shule ya msingi wengine wakasema wako hai, wako hai baadhi wa miaka 70 na, lakini ukiwaona unaona huyu mtu aliishi na anaendelea kuishi japo ameshazeeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wetu wa sasa ndio watu dhalili, dhalili mpaka kwenye jamii yenyewe hawathaminiwi. Mwalimu anafika mahali anamwogopa mwanafunzi wake kwa sababu mwanafunzi anatoka kwenye hali ya juu kuliko Mwalimu. Kwa sababu gani Walimu wetu wanafanywa kuwa ombaomba, watu dhalili, watu wasiothaminiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mateso wanayopata Walimu; Mwalimu Susan amesema kama unataka kuboresha elimu anza na Mwalimu. Mwalimu ambaye mmemjali yuko tayari kuchukua watoto wake akawafundishia chini ya mwembe na wakapata elimu bora, lakini Mwalimu ambaye umemdhalilisha, umemdharau, hata ungemjengea chumba ambacho kina feni na viyoyozi hatafundisha na watoto wale wakafundishika. Jamani hebu tuangalie mzizi wa tatizo uko wapi na tuutatue ule, tusihangaikie matawi, matawi hayajengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi uliyonipa na niwapongeze tena Kamati hizi kwa kazi nzuri na niseme naunga mkono hoja yao. Ahsante.