Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa busara na hekima kwa kunipatia angalau hizi dakika tano na mimi nipate kuzungumzia masuala kadhaa ambayo yananikera katika maisha ya Watanzania, hususan Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia kwa makini hiki kitabu cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, muda hautoshi, lakini kuna mambo mengi ambayo yanaizingira nchi yetu. Kwa mfano, ukurasa huu wa 33 wanasema umuhimu wa uzalishaji wa mbegu bora nchini, sasa katika Wilaya ya Kilombero pale Ifakara tangu mimi sijazaliwa kuna kituo cha utafiti Katrin pale Ifakara, lakini mimi sijawahi kuona katika maisha yangu matokeo ya Kituo hiki cha Katrin kwenda angalau katika Wilaya ya Kilombero tu siyo Tanzania, kwenda kuwaelimisha wakulima ni mbegu gani sahihi wanatakiwa watumie na kuna magonjwa yanayokabili mpunga na kile kituo kinasema kinafanya utafiti pamoja na mpunga, lakini wananchi wa Wilaya tu ya Kilombero hawajafaidika. Sasa sielewi, Serikali naomba mtupe maelezo kwa nini kituo hiki hakina matokeo chanya? Ama hamuwapi hela au kuna kitu gani, yaani tunasikia tu lakini hatuoni faida yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu manunuzi ya mpunga; wakati nakuja Bungeni nikapishana na Waziri tena nikasikia na wananchi Waziri anakuja wapi Mngeta, KPL, anakuja kufanya nini huyu kwa wawekezaji, amekwenda kule usiku kwa usiku, nikampigia simu akasema hata saa moja nitafika. Kaenda usiku wa manane, kaenda kuangalia KPL, kaenda kuangalia ghala la chakula, sijui ndiyo uliambiwa ufanye utafiti wa chakula kiko wapi, watu wanasema mna njaa ninyi hamna, lakini usiku kwa usiku mnaingia pale mnaenda kuangalia ghala la chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, KPLni eneo ambalo linazalisha mpunga na mahindi, sasa nauliza hivi, hivi akiba ya chakula ni kwa mahindi tu, je mpunga sisi tunaolima mpunga hiyo siyo akiba ya chakula, kwa nini Serikali hamuweki katika mpango kununua mazao mbalimbali ya chakula kama mpunga. Mmedharau sana lakini ndiyo kilimo ambacho kipo katika nchi hii. Kwa hiyo hata kwenye upungufu wa chakula mnaweza mkapeleka mpunga watu wapate kula. Sasa nataka majibu ya Serikali, je mpunga lini mtauingiza katika bajeti upate kununuliwa kwa ujumla? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masuala ya maji, maji Kilombero na Jimbo la Mlimba yanatokea wakati wa mafuriko, lakini mafuriko yakiisha na maji yanaondoka, lakini kuna mito ya ajabu. Sasa Wizara ya Maji hebu chukueni angalau kuwe na Wilaya moja ya mfano, maana kila Mbunge hapa akisimama maji, hebu chukueni hata Wilaya moja ya mfano muoneshe kwamba mmefanya kwa asilimia fulani na angalau Mbunge mmoja akifika hapa awapongeze, basi muende kwa awamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali njooni Kilombero ambako ni ghala la chakula, kuna mito karibu 39 lakini wananchi wa Kilombero hawana maji, wananchi wa Mlimba hawana maji, naomba mje. Naibu Waziri wa Maji ameahidi akihamia Dodoma baada ya Bunge hili atakuja kutembelea Jimbo la Mlimba, tumuoneshe miradi mbalimbali ya umwagiliaji na maji ya kunywa, miaka na miaka hela zinaingia lakini miradi haiishi, naomba mje mtagundua ufisadi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa wenyekiti, kuhusu wafugaji na wakulima. Wafugaji na wakulima ni kero ndani ya nchi hii, lakini hawa wote wanategemeana, mfugaji anafuga mkulima analima. Hawa watu wanaowagombanisha ni Serikali kwa kutokupanga mipango bora ya ardhi ili kuwatengea maeneo wafugaji wafuge na wakulima walime, hawa wote wanategemeana, lakini katikakati kuna Serikali ndiyo inayoleta uchonganishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Kilombero…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.