Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kusema kuwa naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze jitihada za Serikali na za Rais katika kuitakia neema nchi yetu, nimpongeze Waziri na Serikali kwa ujumla. Mimi nitajikita sehemu moja tu, sehemu ya mapato na hasa nitajikita kwenye sehemu ya makampuni ya simu nchini mwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo tu, ukichukua watu milioni 10 kwa mwezi, katika hawa kila mmoja wao akitia vocha sh. 1500 kwa wiki, natumia kiwango cha chini sana, sh. 1500 kwa wiki, kodi ya Serikali ni sh. 450 kwa watu milioni 10. Kwa wiki hiyo ni bilioni nne na milioni mia tano, kwa wiki nne kwa sh. 6,000 tu ambazo anachangia yeye kwa kupiga simu kwa mwezi, Serikali inakosa bilioni 216. Pesa hizi zinakwenda kwenye Makampuni ya Simu, pesa hizi hazirudi Serikalini kwenye excise duty na VAT ya 30%. Mfano mdogo, ukinunua bundle ya sh. 20,000/= unapewa package ya shilingi 19,000/=, sasa najiuliza VAT na excise duty ya Serikali inakwenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaelekea pesa za Serikali zinatumika kunufaisha makampuni haya, huku Serikali yenyewe haipati kitu. Udhaifu upo kwa regulator. Regulator anatakiwa aingie katika mitambo ya makampuni haya ajue namna gani kodi ya Serikali inapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanalipa 10,000/= kwa mwezi, 10,000/= kwa mwezi kodi ya Serikali ni shilingi 3000/=, kwa mwaka ni bilioni 360 zinaondoka, hakuna mtu anaye-monitor pesa hizi. Makampuni ya Simu wanapolipa kodi zao hawaweki separation za aina za kodi, corporate tax, VAT, excise duty na kodi zingine zote wanaziweka pamoja wanasema tunalipa bilioni 100, bilioni 50, lakini kuna pesa nyingi za Serikali zinapotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka majibu, tunataka watu wa TCRA na Waziri wa Fedha yuko hapa, haya tumeyasema miaka yote, mwaka huu tunamwambia mwenyewe Mheshimiwa Rais, udhaifu ambao upo kwenye kukusanya mapato ya Serikali kwenye Makampuni ya Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Management fee three percent, matangazo ya makampuni haya ya simu yanapewa mpaka asilimia10 ya mapato yao. Kwa hiyo, kama kampuni inachukua asilimia10 kama kampuni inatangaza mapato yake kwa mwaka mathalani bilioni 100, bilioni 10 inakwenda kwenye matangazo. Matangazo yapi ya kwenda nchi hii kwa bilioni 10 kwa kampuni moja? Nataka nipate maelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la frequency za 4G, nataka Serikali iniambie nchi nyingi duniani 4G ambayo ni long term evolution, baada ya hii 4G sasa hivi itachukua miaka mingi sana kuleta mtandao huu wa 4G. Wenzetu wanapiga mnada, wanampa mtu mmoja, yeye ndiye anawapa wengine, anapewa mnada, Waingereza wanauza 4G mpaka milioni 300 pound, 600 billion. Nchi ya jirani hapa walijaribu jaribu wakapata bilioni 110, nataka kujua TCRA masafa haya wanampa nani na wanapata nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mtambo wa Call Accounting System, tunataka kuwa na forensic audit ya mtambo huu tujue unafanya kazi vipi. Haiwezekani wenye Makampuni ya Simu wanakuwa na ujanja zaidi ya mtambo huu na katika lugha ya kitaalam wanasema garbage in, garbage out, anaye-feed mtambo huu tunataka atueleze anafuatilia vipi mapato ya Makampuni haya ya Simu. Nchi yetu ina uwezo wa kukusanya mapato makubwa sana kwenye Makampuni ya Simu kama regulator TCRA atafanya kazi yake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kudhibiti mapato ya Serikali na hasa nazungumzia VAT na excise duty, lazima sasa TCRA waweke utaratibu. Makampuni haya ya Simu sasa waweke software system ndani ya mashine zao, ili wakati mtu ana- top up simu yake, ukiweka 10,000 kwenye simu yako, pale pale mashine ya simu yako ifanye kazi kama EFD ioneshe asilimia 30 ya Serikali. Hii ndiyo njia peke yake ya kudhibiti wizi unaofanywa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiweka sh. 10,000 na simu ikakuambia sh. 3,000 ya Serikali, sh. 7000 yako na operator kila mtu atajiona ufahari namna gani anachangia pato Serikalini. Hili kama halikufanywa tunamwambia tena Mheshimiwa Rais, hili ni jipu. Tunapoteza mapato mengi sana, TRA wanashindwa kudhibiti pato hili, TCRA wenyewe wanashindwa kudhibiti pato hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri wa Fedha yuko hapa tena huyu Waziri wa fedha tulikuwa naye kwenye Kamati ya Kodi, haya yote tuliyasema wakati akiwa mshauri wa uchumi, Ofisi ya Rais, sasa umeingia hapa Mzee, fanya hii kazi naomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa wazo hapa kwenye Bunge Januari mwaka huu kuhusu sekta isiyo rasmi. Sekta isiyo rasmi nchi ya jirani inakusanya kodi pato la Serikali trilioni nane, daladala hizi, bodaboda hizi, wafanyabiashara wadogo wadogo wote hawa walelewe, najua haitawezekana kwa mwaka mmoja, jibu lililotolewa hapa na wataalam ni bughudha kwenda kukusanya hela hizi, ni bughudha kwenda kukusanya trilioni nane? Wakati nchi inahitaji mapato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji wa Serikali wana tabia ya kuwa na uvivu kwenye kukusanya hizi pesa. Naomba Waziri wa fedha yuko hapa na Waziri wa Mawasiliano, Naibu nafikiri yuko hapa, tujaribu na tufanye tu-embark na process hii ya ku-collect revenue kwa kiwango kikubwa ili nchi hii isiingizwe mkenge kama ilivyoingizwa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo hii ya kuweza kuthibiti mambo haya ipo TCRA wanajua ipo, tatizo linakuja ni willingness ya kutaka kufanya shughuli kama hii. Kwa hiyo, mimi sina mchango mkubwa sana, nimezungumzia 4G, nimezungumzia mapato, nimezungumzia na kipato cha display ya 30% ya Serikali ioneshwe kwenye simu zetu ili tujue mchango ambao Serikali inapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itawafanya TRA wala wasipate tabu, wanakwenda tu kwenye system ya EFD wanajua kila siku tunapata shilingi ngapi kwenye 30%. Udhibiti wa credit card tuelezwe, udhibiti wa hizi credit card uko vipi, consignment ikiingia inatolewa bandarini au airport kama mzigo au inatolewa kama value ya airtime inaingizwa nchini, TRA inatakiwa sasa ijue kama consignment imeingia bilioni tano, asilimia 30 ya bilioni tano tayari ni fedha ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumai leo nasema suala hili nafikiri labda ni mara ya saba au nane toka niingie kwenye Ubunge, sijaona mabadiliko yoyote. Natumaini sasa leo pamoja na Serikali hii na Rais wetu huyu, haya mambo sasa yafanywe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.