Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili na mimi nichangie, lakini kabla sijachangia naipongeza Ofisi ya Bunge kupitia Katibu wa Bunge kwa kitendo cha kuiwezesha Ofisi ya Mbunge wa Ukonga kuwa na fenicha. Kwanza ameonesha uzalendo kwa kuwa fenicha zenyewe zinatengezwa pale Ukonga kwenye Jimbo langu, vilevile kwa kutengeneza mahusiano akaanzia kwangu, hivyo nawapongeza sana waendelee na moyo huo. Nawashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, sitaunga hoja kama CCM, kwa sababu wanaunga mapema halafu asilimia 95.5 wanalalamika! Huu mtindo haupaswi kuwa entertained kwenye Bunge, mimi nitaenda tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, taarifa ya Upinzani Bungeni imempa maswali wala asiyabeze ni mambo ya msingi kweli, kwa rekodi tu nataka nikumbushe mambo machache ambayo nataka ayazingatie kama atapenda, maana yake anaweza akakaidi tu.
Kwa mfano, nchi hii inataka kuwa nchi ya viwanda, lakini Watanzania wanataka kuhakikishiwa na Serikali hii, mimi siiti Serikali Tukufu sasa Mungu atakuwa nani! Wanasema hivi viwanda vilikuwepo……
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Hiyo kengele ni ya mtu mwingine wewe endelea tu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako hivi vitu vinachanganya hapa.
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. MWITA M. WAITARA: Naomba unilinde, hizi kengele na kelele uzuie kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa inaonesha kwamba viwanda viliuzwa, sasa wakati tunaenda kuleta huu Mpango ambao ni mzuri sana kwa Watanzania, lazima Watanzania wahakikishiwe tukianzisha havitauzwa tena, kutolewa bure au kugawanywa kama shamba la bibi? Hilo ni jambo la msingi kabla ya kwenda kwenye mpango wenyewe, hatuwezi kuweka hela mahali ambapo anaweza akaja mtu mwingine hapa, hapa Mheshimiwa Magufuli amekuja na habari ya viwanda, anaweza akaja mwingine na ajenda zake akaanza kuvigawa tena bure, unakuta nchi inapiga marktime. Sheria inasema nini juu ya hayo mambo ambayo yamefanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana, watu waligawana viwanda, waliovunja utaratibu hawajashughulikiwa, hawajawajibishwa, hakuna mtu yupo Mahakamani, tunaleta mpango mwingine! Sasa nadhani hili jambo ni muhimu sana likazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwenye ukurasa wa tatu, napitia ile taarifa ya Upinzani, wamesema fedha zilizotolewa ni asilimia 26, ni muhimu Waziri akatuonesha kama mipango iliyopangwa ilikamilika kwa asilimia 26 kwa eneo hili, hivi hizi zilizobaki asilimia takriban 74 amekuja na miujiza gani tena mingine mipya ambayo itawasaidia ili iweze kuwa sustainable, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote iliyopangwa haikuzidi nusu tangu imeanza kuzungumza Serikali hii mpya ya CCM sababu haya ni majina tu, alikuwepo Mheshimiwa Nyerere, amekuja Mheshimiwa Mwinyi amekuja Mheshimiwa Kikwete, sasa ni Mheshimiwa Magufuli. Sasa haya ni majina tu lakini Serikali ya Chama kilekile asilimia 60 ya mipango ya maendeleo haijawahi kufikiwa nchi hii .
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani mambo haya yangetusaidia kwa mfano, yametajwa hapa mambo ya msingi kabisa kwamba Deni la Taifa limeongezeka, nimejaribu kugawa hapa hizi trillion 41536.6 ni kama takriban 923,000 kwa kila Mtanzania hata aliyezaliwa leo, ambazo kama Taifa tunadaiwa katika nchi hii. Sasa nataka kujua, deni likiwa kubwa namna hii athari yake kiuchumi ikoje na watu wategemee nini? Maana tunadaiwa hapa tulipo kila mtu sh. 923,000 kwa mahesabu yaliyotajwa hapa, sasa nikasema haya mambo ni muhimu sana kuyazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye rasimu ya Mheshimiwa Warioba haya mambo yangeweza kujibiwa, sasa mkachakachua Waheshimiwa ndugu zangu CCM mkaleta mambo yenu, figisu figisu nyingi, mkapindisha haya mambo. Ile rasimu ilikuwa inaelekeza ili Taifa likope, ili hiyo hoja ije Bunge lijadili, liruhusu ili tuelezwe unakopa, haya maswali ambayo Mheshimiwa Silinde kwa niaba yetu, anauliza, uliweka dhamana ya nini, mlifanyia kitu gani, mipango ikoje, nani alikopa, vitu vya namna hiyo vingeweza kujibiwa sasa ile rasimu mmeichakachua, sisi Katiba hatuna, haya mambo yangeweza kujibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye hoja hizi ambazo zimezungumzwa. Miundombinu; tumezungumza hapa, mimi nilipo ni karibu na uwanja wa ndege, nitaomba Waziri mwenye dhamana na eneo hili anisaidie, uwanja wa ndege unajengwa terminal III, lakini taarifa ambazo ninazo phase one walikuwa na mkataba, phase two wanaendelea hawana mkataba eneo lile, lakini unazungumza kutengeneza miundombinu, tuimarishe uwanja wa ndege, lakini wako wananchi pale Kipawa walihamishwa kutoka pale wakapelekwa Kata ya Buyuni na Chanika, kuna ugomvi mkubwa wananchi wale hawajawahi kulipwa mpaka leo. Serikali imechukua watu imewahamisha kutoka eneo la Kipawa ikawapeleka Buyuni wakaenda kuwakabidhi maeneo ya watu, hakuna fidia. Kwa hiyo, aliyekabidhiwa eneo hawezi kujenga kwa sababu mwenye eneo hajalipwa, hivyo kuna mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tunapoandaa mipango hii tusitengeneze matatizo kwa wananchi. Unawekeza eneo, unaweka watu pale wanafanya biashara zao lakini wananchi wako wanaishia kulia na kulalamika watu wana makabrasha mezani yamejaa, kesi nyingi na hawajui wazipeleke sehemu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyekiti Lukuvi amelipokea hili, nadhani na yeye kama ataendelea hivi atakuwa mzuri, angalau amesikiliza, ametoa taarifa ameleta ramani ya maeneo yale angalau uweze kuonesha maeneo ya wazi na maendeleo yaweze kwenda vizuri. Sasa hilo ni kwenye uwanja wa ndege, lakini kuna Mheshimiwa mmoja hapa amezungumza habari ya Dar es Salaam kwamba hakuna wakulima, siyo kweli! Zile hela zije.
Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga nawakilisha Kata ya Kivule, Kata ya Kitunda, kata ya Mzinga, Msongola, Uwanja wa Nyani, Ukwende, Zingiziwa kuna maeneo watu wana mashamba makubwa wanalima mihogo na hata Wabunge wote mnaokaa Dar es Salaam mboga nyingi zinatoka Jimbo la Ukonga ziko safi kabisa. Kwa hiyo kuboresha huduma hii siyo dhambi watu wasibeze hapa, kama mtu anaomba huduma kwenye Jimbo lake asibeze Majimbo ya watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme. Ni kweli kwamba tunahitaji viwanda lakini Dar es Salaam pale maeneo mengi ni giza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anachukua hatua lakini kama hata Dar es Salalam ambako hawa Wawekezaji wanapita watu wetu ni giza, umeme ni wa kusuasua mpaka leo tunapozungumza, yaani kuna watu wanakaa pale kama wanakaa kijijini halafu unazungumza habari ya viwanda, umeme wa kawaida wa majumbani hautoshelezi, viwanda itakuwaje? Yaani umeme wa kawaida tu haujitoshelezi viwanda inakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huwezi kuwa na viwanda, huna umeme, mazao ya kilimo na mifugo. Kuna watu wamekataa tamaa, wamezungumza wenzangu wa Mtwara, hata kule Tarime ukienda watu wa kahawa, wananchi wamefyeka mashamba, wengine wanaenda kulima zile bangi ambazo mmesikia watu wamesema na mirungi, wameweka tumbaku haina kiwanda, hamna usaidizi sasa lazima mje na mbinu Mheshimiwa Waziri ya kuonesha watu waliokata tamaa kulima mazao ya biashara kwamba soko lipo na bei itakuwa ni nzuri na makato na manyanyaso mengi ambayo yapo yataondolewa, maeneo yale hata ile kahawa na mahindi, wapo watu ma-settler wachache ambao ndiyo wanamiliki soko pale. Wanapanga bei, pembejeo zile zikienda kwenye Halmashauri wanagawana, kwa hiyo, kuna ulanguzi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makandokando haya yangeweza kurekebishwa, angalau Watanzania mnapozungumza habari ya viwanda, watu wanakwenda njia imenyooka, vizingiti vimeondoka, ubaguzi pale hakuna, mambo ya namna hiyo yangetakiwa yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Ukonga, Ukonga kuna viwanda vya chakula cha kuku, lakini mayai yanapatikana na kuku wa nyama wa kisasa, lakini kule hakuna kiwanda cha kutotoa vifaranga rasmi. Vifaranga vingi vinatoka nje ya nchi na baadhi ya material inatoka nje ya nchi. Sasa wananchi wale wanachukua vifaranga wanawekeza, mtu amedunduliza, mama lishe, kijana wa boda boda pamoja na kupata shida mjini hapa, kukamatwa kamatwa sana, lakini akipata kidogo anawekeza kuku wake 200, 500, wakikua baada ya miezi miwili, mitatu, minne kuku wote wanakufa, ukienda kuulizia unaambiwa kwamba shida ilikuwa ni kiwandani vifaranga vilikuwa na shida ambavyo hatuna viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mambo kama haya pamoja na kwamba tunawekeza tuone ubora wa mali ambayo inaletwa ili watu wetu wasiingizwe kwenye umaskini ambao kwa kweli tunajitengenezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam kwenye biashara kuna habari inaitwa DECI na Malingumu, kwamba watu walikuwa wanapanda pesa. Nimesikia Watanzania wote hapa na Wabunge mnafahamu, yaani pesa ikawa miujiza ya Mungu kwamba pesa unaweza ukapanda ikaota kama uyoga, ikazaa mara mbili, tatu na watu wakavuna na Mawaziri wa Serikali hii ya CCM walishiriki zoezi hili na wakataja maeneo kesi ikaenda Mahakamani. Mpaka leo wananchi wale wanasubiri malipo wamekuwa maskini, wameuziwa nyumba zao. Kwa kweli mnapozungumzia Mpango Mheshimiwa Waziri ungejua hali iliyoko hiyo ungeenda sijui kujifungia wapi kama ni Mungu akutembelee upate miujiza uje na mipango ambayo inatekelezeka. Hizi ni kero ambazo zinaumiza wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afya; sasa mmetangaza kwamba kuna, kwa mfano, mimi kule Ukonga, jana nimejibiwa swali langu na Mheshimiwa nimesikitika majibu, Jimbo la Ukonga na Segerea tunategemea hospitali ya Amana. Tumesema tujenge pale hospitali, Halmashauri imetenga kwa mwaka bilioni moja au milioni 900, hiyo hospitali itagharimu zaidi ya bilioni 600 kwa mpango uliopo, maana Waziri alisoma alichofanya hapa na ndicho mmefanya kuzuia TBC isioneshe na TV zingine watu wasione, watu wa Ukonga walikuwa wanalia. Waziri ametuma mtu hapa ameenda akachukua ame-copy na ku-paste ambacho tulipitisha Manispaa ya Ilala hakuongeza kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana kwa mpango ule ile hospitali itajengwa kwa miaka 26, nimewaambia ile Wilaya kama mpango wenyewe ni ule, ile fedha tuifanyie reallocation, utajenga magofu fedha itapotea haiwezi kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuwa na viwanda, watumishi wetu hawa ni maskini hawana afya, unafanyaje? Mkienda kwenye viwanda vyenyewe, malipo pale pale Gongo la Mboto kuna Kiwanda cha Namela, mwenye kiwanda anawalipa watu wale sh. 4,000/= ambayo imetajwa hapa ndiyo posho ya kufanya kazi. Katika hali ya kawaida Mheshimiwa Waziri, wewe ni mtaalam wa mambo ya finance, hivi sh. 4,000/= Dar es Salaam utaishi kweli? Ndiyo mpango uliopo na Sheria imesema l50,000/= kwenye viwanda. Kwa hiyo, kuna mianya mnatoa wale wawekezaji wakija kwa nia njema tunawapa support, wamechukua ardhi yetu, nguvu kazi ya kwetu, tuna wataalam wanalipwa kidogo sana, lakini mwisho wa siku watatunyonya kweli kweli, sasa mikakati kama hii na mambo haya yangetakiwa yapangiliwe vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli litakuwa jambo langu la mwisho. Reli inayozungumzwa hapa tunahitaji pale Ukonga, huduma ya TAZARA na reli ya Kati kwa maana ya kusafirisha kupunguza misongamano, sasa hili jambo likifanyika itatusaidia.
Nimeona kwenye Mpango imeonekana, sasa shida ni kwamba na kwa ujumla haya makaratasi ukisoma uko chumbani unafurahi kweli kweli, nendeni mahali sasa myaondoe yaende kwenye vitendo ndiyo mahitaji! Shida ya nchi hii siyo mipango, shida ni kwamba mlichokiandika kiwe transformed kwenye actions, watu waone actions zote zimefanyika, barabara za lami zimetajwa, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ametaja barabara ya Kitunda – Kivule - Msongola mara nne zote akiwa Bungeni hapa sasa imetajwa tena akiwa Rais nataka nishuhudie kama Rais atakuwa mwongo tena, maana yake kama alikuwa ananyimwa hela kugawiwa sasa hivi anagawa mwenyewe, anatumbua majipu na anafanya reallocation nataka tushuhudie mambo haya, ni matarajio ya Wabunge wengi kwamba mipango mliyoileta hapa inatekelezeka.
Halafu Wabunge wa CCM muache kupiga makofi sana huku, mnaunga mkono mwanzo halafu mnalalamika mwanzo mwisho hivi utawala bora unakujaje? Hivi ninyi Viongozi, Mheshimiwa Waziri, Waheshimiwa mnazima TV, mpango mzuri, maneno mengi na majibu mazuri ya Upinzani ya Mheshimwa Silinde hayajaonwa na Watanzania, hoja zetu hazisikilizwi, tuko hapa gizani kama wachawi humu ndani. Watu wamenywea humu ndani, humu ndani hamtaki watu waone kwa nini? Hivi ninyi nani amewaroga! Nani amewaroga? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia hii ya sasa hivi Serikali inakaa kabisa inafunga Vyombo vya Habari, mlisema TV yenu ni gharama siyo? Hizi za watu binafsi zinawahusu nini? Mmeombwa hela? Haki ya Mungu nimesikitika sana, yaani watu wazima, Mawaziri kabisa mnakubali kwenda kuwazuia Watanzania, Ibara ya ndani ya Katiba ya nchi mnaivunja hivi ya haki ya kupata taarifa. Gharama mmesema ni bilioni…! hiyo TBC fungeni ni chombo chenu cha uenezi, endeleeni na mambo yenu, watu binafsi waruhusiwe humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi imekuwa giza tunaongea hapa yaani mwende mchuje, mrekodi muweke mnayotaka ninyi halafu mtuletee tufurahie, halafu mnatuambia habari ya elimu hapa, mnatuambia mambo ya TEHAMA, humu mmeweka mambo ya TEHAMA, sasa TEHAMA maana yake nini? TEHAMA maana yake ni eti watu wafanye kazi, yaani mchukue viboko muwapige watu ambao hawaendi shamba sasa, kawatandike watu ambao hawaendi shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu amemwajiri mtu mzembe anaangalia TV ofisini kwake amfukuze kazi.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Nataka nipate majibu.