Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja hii kwenye maeneo ya maliasili na utalii, elimu, kilimo, viwanda, afya na uchumi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa masikitiko makubwa kuona mpango huu haujaweka Sekta ya Maliasili na Utalii kama moja ya maeneo ya vipaumbele licha ya kwamba sekta hii huchangia zaidi kwenye kuingiza fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutolewa kwa maliasili na utalii katika vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ni fedheha na masikitiko makubwa kuwa sekta hii haipo katika Mpango wa mwaka 2017/2018. Tunaomba Serikali itoe sababu za msingi, ni kwa nini Sekta ya Maliasili haipo ilhali ndiyo sekta iliyokuwa ikichangia kukuza uchumi wa ndani kwa miaka yote na ndiyo inayotoa ajira kwa vijana na haihitaji gharama kubwa sana za uendeshaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, kupungua kwa watalii wanaoingia nchini na hali mbaya ya Sekta ya Utalii; mfano watalii wamepungua kwa 8% kutoka watalii 1,140,156 mwaka 2014 mpaka watalii 1,048,944 mwaka 2015 na bado hali inazidi kuwa mbaya kwani watalii wanazidi kupungua kila siku hasa baada ya uwepo wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za Maliasili na Utalii. Pia kumekuwepo na upungufu wa idadi ya watalii wa hotelini 1,005,058 mwaka 2014 mpaka 969,986.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupungua kwa mapato ya utalii kutoka dola milioni 1,982 mpaka 1,906; na hizi ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014/2015. Vile vile kwa wastani wa siku za kukaa watalii, zimepungua kutoka siku 12 mpaka kumi na kwa sasa hali imezidi kuwa mbaya zaidi baada ya kuwepo kwa VAT, maana Sekta ya Utalii imekuwa na mlundikano wa kodi nyingi sana takriban 32. Hizi zote zinaongeza gharama na kusababisha watalii kuona ni ghali sana kuja kupumzika na kujionea utalii wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kumekuwepo na matatizo makubwa kwenye Sekta ya Utalii yanayochangia kushuka kwa mapato yatokanayo na utalii. Mfano tu, ninavyoongea sasa, Mamlaka ya Ngorongoro imekataza wamiliki na magari binafsi yanayotoa huduma za kitalii kwa kutumia magari binafsi ambayo kimsingi yamesajiliwa kibiashara na yamekidhi vigezo vyote vya magari ya utalii ila tu siyo magari ya Kampuni, yawe ndiyo kama masharti ya leseni ya utalii inavyotaka. Kama barua yenye Kumbukumbu Namba NCAA/D/584/Vol.XIII/20, pamoja na barua TNP/HQ/L.10/22 iliyohusu zoezi la uhakiki wa leseni kwa makampuni yanayofanya shughuli za utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa takriban magari 300 yamezuiwa kufanya kazi za kupeleka wageni ndani ya hifadhi. Makampuni yaliyokuwa yanafanya biashara kupitia magari haya tayari yalikuwa yana wageni ambao wanapaswa kwenda hifadhini, hivyo watalii wengi wanataabika ilhali tayari wameshatoa pesa zao na wanahitaji huduma. Hii ina athari ya moja kwa moja katika soko zima la utalii nchini ambalo mpaka sasa linakumbwa na changamoto lukuki.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua hitaji la kisheria katika kupata leseni ya utalii, lakini tujiulize, tunawasaidia vipi Watanzania hawa ambao wamejichanga na kupata fedha kidogo kwa ajili ya mtaji wa kuanzisha biashara hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa kuwa Waziri Profesa Maghembe na Watendaji wake waliweza kuona ni fursa nzuri za kuendelea kuwaajiri watu kwenye Sekta ya Utalii ya Usafirishaji kwa kulifanyia kazi pendekezo letu tulilolitoa wakati wa bajeti, ambapo tulipendekeza Serikali angalau iweke sharti la magari kuwa matano badala yake yamekuwa mawili au matatu. Kwa taarifa nilizonazo, ni kuwa magari matatu ndiyo hitajio. Hii ni hatua tatuzi kwa vijana maskini wa Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu ni kwamba, kufuatia barua ya Ngorongoro ni kuwa, Serikali ipate uhakika wa uwepo wa magari matatu katika kuanzisha biashara, iwe ni magari matatu bila kuwa na kigezo cha umiliki, bali ieleze kuwa kampuni ni lazima iwe na magari matatu, iwe ni magari ya kukodi au ya kibiashara lakini ni lazima kampuni ioneshe uwezo na uhakika wa magari hayo; na yabandikwe sticker. Msingi wa hoja hii ni kuwa siyo Watanzania wote wana uwezo wa kumiliki magari matatu yenye viwango elekezi, bali wanaweza kukodi magari yenye viwango elekezi na biashara hii ikaendelea na kutoa ajira na kukuza uchumi ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwenye sharti la leseni ya biashara (TALA License) hiyo kuna hitaji la kampuni kulipa dola 2,000 kwa makampuni ya ndani na dola 5,000 kwa makampuni ya nje, havijalishi idadi ya magari ambayo kampuni hiyo inamiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isihakikishe kuwa linalipa dola 100 kwa mwaka bila kujali idadi ya magari? Serikali itapata fedha nyingi zaidi kwa kuwa yapo makampuni yana magari zaidi ya 300 na yanalipa dola 2,000 na mengine yana magari matano na yanalipa kiasi sawa cha dola 2,000. Endapo kila kampuni italipa dola 100 kwa mwaka, ina maana kwamba kwa makampuni yenye magari 300 kwa mwaka watalipa dola 3,000 badala ya 2,000 kama ilivyo sasa. Hii itasaidia wafanyabiashara wadogo pia kuweza kumiliki magari yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nashauri hii Sekta ipewe kipaumbele. Tulishauri kuwa kodi ya ongezeko la thamani ni bomu kwa uchumi wetu na sasa athari imeanza kuonekana. Tuliwaiga Kenya, lakini wenzetu waliondoa hiyo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na nature ya utalii ya Kenya ni kama kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni juu ya zoezi zima la uhakiki wa wafanyakazi hewa ambalo limechukua muda mwingi, nalo linaendelea kuwaacha Watanzania wengi bila ajira na kwa wale waliokuwa wanasubiri ajira pamoja na wale walioajiriwa mwezi wa Nane, 2015 ambapo walisitishiwa ajira kupisha uhakiki tangu Februari, 2016 hadi leo hawapo kazini na hawalipwi mshahara. Unategemea hawa Watanzania wataishi vipi? Tunataka majibu kwenye hili maana Mheshimiwa Rais alisema akiwa BoT kuwa zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hewa kuwa ni kati ya miezi miwili au mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoonekana sasa ni dhahiri Serikali hii haina fedha ama inaelekea kufilisika na hivyo kuamua kwa makusudi kujificha chini ya kivuli cha uhakiki ili kuondoa aibu ya kutokuwa na fedha ya ajira mpya. Fedha za nyongeza kwenye kupandisha madaraja, kuongeza mishahara kwa mujibu wa Sheria na Mikataba, hakuna watumishi kwenda masomoni wakilipiwa na mwajiri wake. Tunaomba majibu katika hili, maana bila Walimu wenye motivation, Madaktari, Manesi na kadhalika, hii nchi tunaiweka kwenye bomb. Hatua stahiki zichukuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya viwanda bila mikakati ya elimu yenye kutoa elimu na wanafunzi wa kada mbalimbali ili waweze kwenda kwenye viwanda tarajia; bila mikopo kwa kada zote kwenye elimu ya juu ni bomb. Bila kuwekeza kwenye motisha za Walimu kama nyumba, ofisi, Transport Allowance and Hardship Allowance; pia bila kuwa na uhakika wa maji ni ndoto kuzungumzia Tanzania ya viwanda kama hakuna umeme, miundombinu imara ya barabara, kuwekeza katika kilimo chenye tija ili kiweze kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda tarajiwa, itakuwa ni ndoto ya Abunuwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni juu ya kutokuwekwa asilimia za pato la Taifa kwenye Mpango wa Maendeleo, sababu na Sheria ya utekelezaji ya Mpango wa Maendeleo. Mpango wa mwaka 2011/2012 – 2015/2016 tuliazimia 35% ya pato la Taifa ziende kwenye Mpango wa Maendeleo lakini kwa sasa mpango hausemi chochote. Hii ni hatari sana maana tunaweza kukuta mpango huu ukitegemea wahisani zaidi, kitu ambacho ni hatari kama nchi tusipowekeza kwenye maendeleo yetu wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni juu ya umuhimu wa kuona review kwenye mdororo wa kutokuwa na mizigo Bandarini ambayo inatokana na tozo mbalimbali, wharfrage tunatoza dola 240 kwa futi 20 lakini wenzetu dola 70 na VAT on Transit na kadhalika.