Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kusema huu mpango haukidhi viwango ambavyo tulivitarajia, wala haukutosheleza matakwa ya Kitaifa na maendeleo tunayoyataka. Kwanza, haujatupa tathmini; tumefikia wapi? Tumekwama wapi? Tuanzie wapi baada ya kupitisha bajeti ndani ya mwaka huu? Huu ni mpango gani usioonesha dira na hali halisi ya mambo yalivyo katika kila sekta?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni mkanganyiko au mgongano wa wazi kati ya kanuni za Bunge na Sheria ya Bajeti kuhusu uwasilishwaji wa mpango na makisio ya bajeti katika mwaka wa fedha unaofuata. Kikawaida, pale panapotokea mgongano kati ya kanuni na sheria, basi, sheria ndiyo husimama, lakini Bunge letu, huipa kanuni kipaumbele. Tukizingatia Kifungu 21(2) cha Sheria ya Bajeti, mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa yalikuwa yawasilishwe katika Bunge la Januari – Februari. Hii ni kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaoendelea na makisio ya hali ya uchumi kwa miaka mitatu ya fedha inayofuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kutoa mchango kuhusu mapendekezo ya Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa, tunashuhudia hali ya kiuchumi ikiyumba sana ndani ya nchi hii. Hii ni kutokana na sababu tofauti tofauti.
(i) Sekta ya Kilimo imeathirika hasa kutokana na mabenki kuzuia kutoa mikopo kwa wakulima kama ilivyokuwa hapo awali; Benki kujitokeza na kutoa mikopo kwa wakulima ili kuendeleza kilimo bora chenye tija;
(ii) Pia uchumi umedorora kupitia Sekta ya Utalii na kukaribia kufa. Hii ni kutokana na Serikali kuongeza kodi ya ongezeko la thamani, hivyo Serikali imesababisha kupungua kwa watalii kuja Tanzania na hivyo kukosa pato la Taifa;
(iii) Serikali kukamata bidhaa na mali za wafanyabiashara wakubwa, hali iliyosababisha wafanyabiashara kufunga biashara zao nchini kwa kuhofia mali zao kuchukuliwa na Serikali, jambo ambalo linazorotesha uchumi, hivyo Sheria ichukue hatua ya kuwawajibisha wahujumu uchumi wa nchi hii jambo ambalo linasababisha uchumi unakuwa tete;
(iv) Serikali imetengeneza watumishi hewa na kusitisha ajira kwa sababu ya kuwa inafanya uhakiki wa watumishi wake. Jambo hili limepelekea kuyumba kwa uchumi na pesa nyingine kulipwa watumishi kama sehemu ya usumbufu wakati kumewafanya wasomi wa taaluma mbalimbali kuishi kama ombaomba ndani ya nchi yao na kudhalilika kutokana na elimu waliyopata. Wananchi wamekuwa wakimbizi kwenye nchi yao hali inatisha. Serikali izingatie hali ya wananchi na raia wake. Serikali bora ni yenye kujali raia wake na kuweza kuwajibika;
(v) Sekta ya Afya ndiyo iko hoi na kuzorota zaidi. Tumeshuhudia kukosekana dawa, chanjo na vifaa tiba katika hospitali zetu nchini, huku maelfu ya wananchi wakipoteza maisha huku tukishuhudia Waziri wa Sekta hii na Makamu kulumbana, mmoja anasema ziko, Mkuu wake akisema hakuna dawa, chanjo na vifaa tiba na hali ni tete. Hivyo Serikali itafakari kauli hizi na kuwapatia wananchi wao huduma nzuri ya afya ili kunusuru janga hili nchini;
(vi) Sekta ya Elimu pia ni changamoto. Elimu imekuwa bure lakini ni bora ilivyokuwa ya kuchangia kwani Serikali ilikuwa haikujipanga kuhusiana na hilo. Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanakosa mikopo hali inayowakatisha tamaa wanafunzi hawa kumaliza masomo yao. Walisomeshwa na wazee kwa hali na mali ili waje kuikwamua jamii na yeye binafsi kutokana na hali duni waliyokuwa nayo. Pia Serikali inashawishi watu wajiajiri wenyewe; hali inajulikana kwamba elimu yetu haifanyi mtu aweze kujiajiri. Hivyo, Serikali ijipange kuwa na mfumo wa elimu hii na ndiyo washawishi watu wajiajiri. Tunatakiwa kujiandaa hivyo, ndiyo tutoe hamasa;
(vii) Tulishuhudia na kuahidiwa viwanda, lakini mpaka sasa hakuna kiwanda hata kimoja, jambo ambalo halikutengenezewa plan nzuri, bali Serikali ilikurupuka bila kujiandaa vya kutosha na kusababisha hali ya uchumi kudorora;
(viii) Suala la Bandari; mizigo imepungua hali inayosababisha uchumi kuzorota na mapato kupungua. Kiukweli Serikali imefilisika japokuwa Serikali haikubali, lakini kuwepo viashiria hivyo ni wazi kuwa imeshindwa. Ila naishauri Serikali kuwa makini na kufanya tafiti mbalimbali ili kuinasua nchi hii ya Tanzania katika giza hili nene; na
(ix) Halikadhalika, tunaishauri Serikali irudishe mamlaka ya kuwa Halmashauri kuchukua kodi za nyumba na vyanzo vingine ili zitumike kwenye Halmashauri kuimarisha na kuanzisha miradi kuliko kupewa TRA hali ambayo inaonesha imeshindwa kutekeleza hilo kipindi cha kwanza na hiki cha pili mpaka sasa.